Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Sweden nchini, Bw. Anders Sjoberg
wakisaini mikataba ya msaada wa dola za Marekani milioni 90 sawa na shilingi bilioni
240.95 kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE) kwa ajili ya
kugharamia Sekta Elimu, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Sweden nchini, Bw. Anders Sjoberg
wakionesha mikataba ya msaada wa dola za Marekani milioni 90 (shilingi bilioni
240.95) zilizotolewa na wadau wa maendeleo kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa
Elimu Duniani (GPE), katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Sweden nchini, Bw. Anders Sjoberg
(katikati) wakionesha mikataba ya msaada wa Dola za Marekani milioni 90 (
shilingi bilioni 240.95) kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE),
kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard
Akwilapo na kulia ni mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. John Cheyo, katika hafla iliyofanyika
jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Fedha za Nje,
Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Sauda Msemo akiteta jambo na mwakilishi wa
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw.
John Cheyo, katika hafla ya uwekaji saini mikataba ya msaada wa dola za Marekani
milioni 90 (shilingi bilioni 240.95) kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu
Duniani (GPE), iliyofanyika jijini Dar
es Salaam.
Baadhi ya washirika wa
maendeleo wanaochangia katika Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE),
wakifuatilia kwa makini matukio mbalimbali yaliyokua yakiendelea katika hafla
ya utiaji saini mikataba ya msaada wa dola za Marekani milioni 90 (shilingi bilioni
240.95) kutoka GPE kati ya Serikali ya
Tanzania na Sweden, ambayo ni wakala wa
mfuko huo, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watumishi wa
Wizara ya Fedha na Mipango wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,
Bw. Doto James (hayupo pichani) wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya
msaada wa dola za Marekani milioni 90 (shilingi bilioni 240.95) kutoka Mfuko wa
Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Sweden nchini, Bw. Anders Sjoberg,
(katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na wadau wa maendeleo waliochangia
fedha za msaada wa dola za Marekani milioni 90 (shilingi bilioni 240.95)
kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), baada ya kumalizika kwa
halfa ya utiaji saini wa mikataba hiyo, jijini Dar es Salaam.(Picha na Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango).
Na Farida Ramadhani, WFM, Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imepokea msaada wa Dola za Marekani milioni 90 sawa na
shilingi bilioni 240.95 kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), kwa
ajili ya kugharamia miradi miwili ya Sekta ya Elimu.
Mikataba ya msaada huo
imesainiwa katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es Salaam, na
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Doto James kwa upande wa Serikali na Balozi wa
Sweden nchini, Bw. Anders Sjoberg, ambaye nchi yake ni Wakala wa Msaada huo
kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la nchi hiyo (SIDA).
Akizungumza katika hafla ya
utiaji saini mikataba ya msaada huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango,
Bw. Doto James alisema msaada huo ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya Mpango
wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP) 2016/17 – 2021/22 na nyongeza ya Mpango wa Elimu kwa Matokeo
(EP4R).
“Kati ya fedha hizo za
msaada, dola za Marekani milioni 38.89 (Sh. bil. 88.55) zitatumika kughagharamia
Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP) 2016/17 – 2021/22 na dola za
Marekani milioni 51.11 (Sh. bil. 116.40) ni kwa ajili ya nyongeza katika
mchango wa Sweden katika Mpango wa Elimu kwa Matokeo (EP4R) ulioanza tangu
mwaka 2015”, alifafanua.
Alisema fedha za kugharamia
Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu zitatumika kutimiza malengo mahsusi ya
programu za Sekta ndogo za elimu ya msingi, elimu jumuishi na watu wazima
pamoja na elimu nje ya mfumo rasmi.
Alibainisha kuwa utekelezaji
wa miradi hiyo utachangia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya Mapango wa Pili
wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano ambao pamoja na mambo mengine unalenga
kuboresha Sekta ya Elimu kupitia Mafunzo ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu
(LANES), kuongeza udahili wa wanafunzi pamoja na kuboresha mazingira ya kusomea
kwa kujenga madarasa.
Aliishukuru Serikali ya
Sweden kwa kuratibu upatikanaji wa fedha hizi ambazo zinafanya uwekezaji wa
nchi hiyo hapa nchini kufikia zaidi ya shilingi trilioni 1.25 zilizowekezwa kwenye
miradi mbalimbali ikiwemo mapitio ya matumizi ya fedha za Umma, maliasili na
hifadhi ya jamii, elimu, nishati, utafiti, na kusisitiza kuwa uhusiano wan chi
hizo mbili utaendelea kuimarika.
Aidha, Bw. James amempongeza
Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
kwa jitihada zake kubwa za kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo
maboresho makubwa katika Sekta ya Elimu, ikiwemo utoaji elimu bila malipo
kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
Naye Balozi wa Sweden
Tanzania, Bw. Anders Sjoberg,
aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada mbalimbali iliyochukua
katika kuboresha elimu hususani katika awamu ya kwanza ya programu ya Mafunzo
ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES) pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Sekta
ya Elimu (ESDP) 2017 – 2021.
Aliishauri Serikali ya
Tanzania kuangalia kwa karibu suala la maendeleo ya elimu ya mtoto wa kike hasa
kipindi cha kutoka elimu ya msingi kwenda Sekondari pamoja na kuboresha matokeo
yao.
Alibainisha kuwa Sweden na
washirika wengine wa maendeleo wapo tayari kushirikiana na Tanzania katika
kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo elimu.
Kwa upande wake Mkuu wa
Shirika la Misaada ya Maendeleo la Uingereza (DFID), Bi. Beth Arthy akizungumza
kwa niaba ya washirika wengine wa maendeleo, ameipongeza Serikali ya Tanzania
kwa kupiga hatua katika Sekta ya elimu ambayo matokeo yake yanaongezeka kila
mwaka.
Alisema matokeo hayo
yanatokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa katika Sekta hiyo ikiwemo mpango
wa elimu bila malipo ambao umeongeza idadi ya wanafunzi na kuiwezesha Tanzania
kujizolea umaarufu duniani.
Pamoja na maendelo hayo, Bi.
Arthy aliishauri Serikali kuongeza idadi ya walimu mashuleni ili waweze
kuhudumia wanafunzi kwa ufanisi na kuongeza ufaulu zaidi.
“Tangu kuanzishwa kwa
programu ya elimu bila malipo idadi ya wanafunzi mashuleni imeongezeka kwa kasi
tofauti na idadi ya walimu waliopo hali inayowafanya walimu kufanyakazi kubwa
zaidi ya uwezo wao” aliongeza Bi. Arthy.
Akipokea msaada huo kwa
shukrani, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard
Akwilapo, alisema kuwa Wizara hiyo itahakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili
kuhakikisha Elimu bora kwa wote inapatikana Tanzania.
Msaada huoumechangiwa na
washirika mbalimbali wa maendeleo wakiwemo UNICEF, UNESCO, Benki ya Dunia,
Umoja wa Ulaya, Australia, Canada, Denmark, Ufaransa, Korea, Uholanzi, Norway,
Hispania, Uswiss, Marekani na Uingereza kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu
Duniani (GPE).
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇