Muungano eti wa kupambana na kundi la Daesh unaoongozwa na Marekani umehamisha makao yake makuu kutoka Iraq na kuyapeleka Kuwait kufuatia mauaji ya Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Naibu Kamanda wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq, al Hashdul Shaabi Abu Mahdi al Muhandes, na sisitizo la Iran la kulipiza kisasi mauaji hayo ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani.
Habari hiyo imetangazwa na shirika la habari la Iraq la al Forat ambalo limesema kuwa muungano huo wa majeshi ya nchi kadhaa ulichukua uamuzi wa kuhamisha makao yake kutoka Iraq na kwenda Kuwait jana Jumanne.
Habari hiyo imetangazwa siku kadhaa tu baada ya Bunge la Iraq kupasisha muswada unaowataka wanajeshi wa Marekani kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo baada ya ndege za kivita za Marekani kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Naibu Mkuu wa harakati ya al Hashdul Shaabi, Abu Mahdi al Muhandes.
Siku moja baada ya uamuzi huo wa Bunge la Iraq, Waziri Mkuu wa muda wa nchi hiyo Adil Abdul Mahdi alikutana na balozi wa Marekani mjini Baghdad na kuitaka Washington kuanza kuondoa majeshi yake nchini Iraq.
Viongozii wa ngazi za juu na makamanda wa jeshi la Iran wameapa kwamba watalipiza kisasi dhidi ya mauaji ya kigaidi ya Jenerali Soleimani na wenzake.
Vilevile Naibu katibu Mkuu wa Harakati ya al Nujaba ya Iraq, Nasr al-Shammari amelaani mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Jenerali Soleimani na Abu Mahdi al Muhandes akisisitiza kuwa, harakati za wananchi zinajipanga kuunda muungano mpana zaidi wa kukabiliana na wanajeshi wa Marekani katika eneo la Asia magharibi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇