Diwani wa kata ya Maganzo, Lwinzi Mbalu Kidiga (CCM) ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madiwani wa kata zinazozunguka mgodi wa Mwadui akiwatangazia wananchi kuhusu taarifa za kuzuiwa kwa mkutano wao.
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Katika hali isiyotarajiwa mkutano wa wananchi wanaozunguka mgodi wa almasi wa Williamson Diamond LTD ‘Mgodi wa Mwadui’ ulioandaliwa na Madiwani wanaozunguka mgodi huo kujadili hatima ya Masalia ya mchanga wa madini ya almasi ‘Makininikia’umepigwa marufuku dakika chache kabla ya mkutano kuanza ambapo ghafla viti viliondolewa huku spika zikizimwa wakati diwani wa Maganzo Lwinzi Mbalu Kidiga akizungumza.
Tukio hilo limetokea leo Alhamis Januari 2,2020 majira ya saa sita mchana ambapo madiwani wa kata zinazozunguka mgodi huo pamoja na wananchi waliokusanyika katika soko la kata ya Maganzo ‘Mji wa Maganzo’ wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kutakiwa kutawanyika mara moja kwa madai kuwa ni ‘Order’ Agizo/Amri kutoka juu.
Tukio la kuzuiwa kufanyika mkutano wa hadhara ni kielelezo cha mgogoro uliozuka kati Wachimbaji wadogo wanaozunguka mgodi wa Mwadui na Chama cha Wachimbaji Madini mkoa wa Shinyanga ‘Shinyanga Region Miners Association – SHIREMA’ siku chache baada ya Mgodi wa Williamson Diamond Ltd kuamua kutoa mchanga wa Makinikia ya Almasi bure kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Katika kikao hicho pia kilihudhuriwa pia na Waziri wa Madini Dotto Biteko baada ya wachimbaji kuomba wapewe makinikia ili kuondoa mgogoro kati yao na mgodi ambapo SHIREMA walipewa jukumu la kusimamia utaratibu mzuri wa kugawa mchanga huo.
Akitoa taarifa kwa wananchi kuhusu kusitishwa kwa mkutano huo leo Januari 2,2020 wakati tayari viti na meza kuu vikiwa vimetolewa kwenye soko la Maganzo palipotakiwa kufanyika mkutano wa hadhara, Diwani wa kata ya Maganzo, Lwinzi Mbalu Kidiga ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madiwani wa kata zinazozunguka mgodi wa Mwadui, ghafla spika zilizimwa na watu ambao hawakujulikana mara moja hali iliyozua gumzo kwa wananchi waliokuwa wamejiandaa kusikiliza nini kinajili kwenye mkutano huo.
Kidiga alisema wameahirisha kufanya mkutano huo hadi siku nyingine kutokana na Amri kutoka juu iliyowataka waahirishe mkutano huo vinginevyo watawekwa ndani.Alisema chanzo cha kuzuiwa kufanya mkutano ni watu wachache waliojipanga kuhujumu uchumi wa watu wa Maganzo ili wapate asilimia za chini kwenye makinikia huku akibainisha kuwa yeye kama diwani hakubali.
“Ndugu wananchi mmeiona sura ya hapa, sura ya hapa haijakaa vizuri tulikuwa tumeweka viti kwa ajili ya mkutano wa hadhara lengo na madhumuni ilikuwa ni kuzungumza changamoto zilizopo katika hata hii na kata za jirani lakini cha kushangaza hapa meza zimetolewa. Mkutano wetu ulikuwa ni mzuri tu wa kupeana habari haukuwa na ashki yoyote.,huu mkutano umeahirishwa..kwa Kiswahili kingine Tumezuiwa”,alieleza Kidiga.
“Nimezuiwa lazima niseme ukweli..Huu mkutano wangu upo ndani ya kisheria na nina mamlaka ya kuitisha mkutano bila kuuliza kwa mtu yeyote,sheria na katiba ya nchi inanilinda. Kwa Order kutoka Juu mkutano huu nimeambiwa nisifanye mara moja..Sasa mara moja maana yake huwezi kuuliza lakini wanasema chelewa chelewa mwishowe ukweli utaonekana.
“Sisi hapa ni wakweli,tunataka tuzungumze ukweli na ukweli wenyewe ni kutetea watu walio chini wapate maslahi siyo waingilie watu wachache,hiyo biashara haipo.”,alisema Kidiga huku akishangiliwa na wananchi.
“Mmetuchagua kwa ajili ya kusimamia haki zenu siyo baadhi ya watu wanufaike,hiyo biashara haipo..Tumezuiwa sawa,sisi tuko chini ya sheria hakuna mtu aliye juu ya sheria lakini ilikuwa halali yetu tufanye mkutano huu na madiwani wa kata jirani, tulikuwa tumepanga tuzungumzie kuhusu Makinikia basi.
Tumeambiwa tukifanya mkutano tutawekwa ndani na tukiendelea ku – force udiwani ndiyo basi tena. Ndani tutakwenda kwani waliomo ndani siyo watu?. Tukiwekwa ndani basi Rais Magufuli atakuja kutuwekea dhamana kwani tunatetea wanyonge. Tumetii amri,tutafanya mkutano siku nyingine .Nilitaka niseme hilo ili msisambae kienyeji kwani tuliwaita kwenye mkutano na wengine mmetoka mbali”,alieleza Kidiga.
Kidiga alisema SHIREMA imekuwa ikifanya vikao vyake na kufanya mambo bila kuwashirikisha madiwani wa kata zinazozunguka mgodi wa Mwadui akidai kuwa haina nia nzuri ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini wilayani Kishapu.
Hata hivyo baada ya mkutano huo uliokuwa umezungukwa na askari polisi wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wilaya ya Kishapu Emmanuel Galiyamoshi kuahirishwa,Madiwani wanaozunguka mgodi wa Mwadui,waliamua kufanya mkutano na waandishi wa habari ‘Press Conference’ ili kueleza lengo la mkutano wao.
Katibu wa Jumuiya ya Madiwani wanaozunguka mgodi wa Mwadui Abdul Ngolomole ambaye ni Diwani wa Kata ya Songwa (CCM) alisema hawakubaliani na kitendo cha SHIREMA kumpatia Mkandarasi anayesafirisha mchanga wa madini kutoka Mwadui kupewa asilimia 75 ya mauzo ya almasi na wachimbaji wadogo kupewa asilimia 15.
“Tunataka Mkandarasi wa kusafirisha makinikia atangazwe hadharani kupitia zabuni kwani mkandarasi aliyepo sasa ni Mkandarasi wa mfukoni ambaye ni Junior Construction ya Mbunge wa Kishapu Suleiman Nchambi,ni mkandarasi ambaye amebuniwa na SHIREMA ,huyu ni mtu mkubwa sana, mamlaka zipo lakini kwanini hazisemi?. Sisi tunapotaka kufanya mkutano kuwaeleza wananchi ukweli tunaonekana tunataka kuzuia maslahi ya watu flani”,alisema Ngolomole.
“Baada ya kulalamikia hizo asilimia 15 SHIREMA wameongeza asilimia kwamba mchimbaji mdogo apate asilimia 37.5 ambayo haiwasaidii wanyonge.Sisi madiwani tumekubaliana wananchi wapate zaidi ya asilimia 60 ili kuwasaidia wanyonge,ndicho anachokitaka Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwani hajatoa Makinikia haya ili wachache wanufaike nayo”,alifafanua Ngolomole.
“Sisi madiwani tunawataka wananchi wasikubali kufanya kazi chini ya SHIREMA kwani inanyonya wananchi wamejiwekea fedha kwenye makinikia haya na wamekuwa wakiwatoza wachimbaji wadogo shilingi 200,000/= tena bila risti ili wapewe usajili SHIREMA. Tunataka wananchi wapewe mamlaka ya kuchagua viongozi wa kuwasimamia kutoka kwenye vikundi vyao vya uchimbaji”,alisema Ngolomole.
“Tumezuiwa kufanya mkutano kwani inaonekana tunaingilia maslahi ya watu binafsi.Kwenye mkutano tulitaka tuwaeleze wananchi mapendekezo ya madiwani na kupokea maoni ya wananchi kuhusu makinikia”,alisema.
Ngolomole alimuomba Rais Magufuli wakati anatoka kwenye mapumziko yake Chato mkoani Geita apitie Maganzo kukutana na wachimbaji wadogo wa madini ili kutatua mgogoro huo wa makinikia.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mwadui Luhumbo Paul Magembe, William Luhende Jijimya wa kata ya Mondo walisema hawapo tayari kuona wananchi wananyonywa na hawatarudi nyuma huku wakimuomba Rais Magufuli kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini wilayani Kishapu.
Nao wananchi waliozungumza na waandishi wa habari,akiwemo Ramadhani Amani,Bala Masanja na Hamis Sizya walisema zoezi la kupewa makinikia lilitolewa bila asilimia hivyo wanashangaa kuona baadhi ya viongozi wanatumia fursa hiyo kujipatia kipato na kuomba serikali kujali wanyonge.
Kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi pamoja madiwani kuhusu SHIREMA,Viongozi wa Chama cha Wachimbaji Madini mkoa wa Shinyanga (SHIREMA) ambao ni Hamza Tandiko (Mwenyekiti) na Gregory Kibusi (Katibu) walikataa kuzungumza na waandishi wa habari wakidai kuwa watatoa taarifa kuhusu Makinikia kwenye kikao chao na vikundi vya wachimbaji wadogo wa madini Januari 3,2020.
Diwani wa kata ya Maganzo, Lwinzi Mbalu Kidiga ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madiwani wa kata zinazozunguka mgodi wa Mwadui akishangaa baada ya spika kuzimwa wakati akiwatangazia wananchi kuhusu taarifa za kuzuiwa kwa mkutano wao katika Soko la Maganzo wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga leo Januari 2,2020. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Katibu wa Jumuiya ya Madiwani wanaozunguka mgodi wa Mwadui Abdul Ngolomole ambaye ni Diwani wa Kata ya Songwa (CCM) akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari 'Press Conference' baada ya kuzuiwa kufanya mkutano wa hadhara uliolenga kujadili kuhusu Makinikia ya almasi yaliyopo katika Mgodi wa Mwadui.
Diwani wa kata ya Maganzo, Lwinzi Mbalu Kidiga ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madiwani wa kata zinazozunguka mgodi wa Mwadui akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari 'Press Conference' baada ya kuzuiwa kufanya mkutano wa hadhara uliolenga kujadili kuhusu Makinikia ya almasi yaliyopo katika Mgodi wa Mwadui.
Mchimbaji mdogo wa madini akizungumza na waandishi wa habari.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇