Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kupata uwezo wa kurusha satalaiti zake katika anga za mbali pamoja na kuwepo vikwazo vya madola makubwa.
Hayo yamedokezwa na msemaji wa Shirika la Viwanda vya Sekta ya Anga katika Wizara ya Ulinzi ya Iran Sayyed Ahmad Husseini ambaye amefafanua kuhusu mpango wa kurusha satalaiti mpya ya Iran iliyopewa jina la Zafar ambayo itarushwa angani kwa kombora maalumu la kubeba sataliti linalojulikana kama Simorgh. Bw. Husseini ameongeza kuwa, kombora la kubeba satalaiti linatumika kwa malengo ya kisayansi na kiraia pekee na haliwezi kuliganishwa na makombora ya kijeshi.
Husseini ameongeza kuwa, hivi sasa kote duniani kuna vituo karibu 22 vya kurusha satalaiti katika anga za mbali na kuongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo ina kituo kimoja cha kurusha satalaiti katika anga za mbali kinachojulikana kama 'Kituo cha Anga za Mbali cha Imam Khomeini MA'. Ameongeza kuwa kituo hicho kiko katika mkoa wa Semnan kaskazini mwa nchi na kinajulikana kwa hivyo si kituo cha siri.
Msemaji wa Shirika la Viwanda vya Sekta ya Anga katika Wizara ya Ulinzi ya Iran ameashiria pia uwezo wa juu wa makombora wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: "Katika uga wa makombora ya kijeshi, Iran ina uwezo wa juu na wakati huo huo imeingia katika duru mpya ya uwezo wa makombora ya kurusha satalaiti katika anga za mbali kwa lengo ya ustawi wa kisayansi."
Inatarajiwa kuwa katika muda usio mrefu, satalati ya Iran inayojulikana kama Zafar itarushwa katika anga za mbali kwa kutumia kombora la kubeba satalaiti la Simorgh. Satalaiti ya Zafar itarushwa katika umbali wa kilomita 500 kutoka ardhini na itakuwa na majukumu mbali mbali kama vile kuchunguza akiba ya mafuta na madini, utunzaji mazingira na pia masuala ya maafa ya kimaumbile.
Kombora la Simorgh ambalo limeoundwa kikamilifu na wataalamu Wairani lina uwezo wa kubeba satalaiti yenye uzito wa kilo 250.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇