Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema kuwa mtu yeyote atakayepata virusi vya Corona nchi humo, atatibiwa katika maeneo yaliyotengwa ya mikoa mitatu ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza.
Akizungumza mjini Dodoma leo Waziri Ummy amesema: “Maeneo hayo ni Mawenzi (Kilimanjaro), Buswelu (Mwanza) na Kigamboni (Dar es Salaam). Wizara inaendelea kujiandaa kukabiliana na tishio la ugonjwa huu endapo utaingia nchini. Tutahakikisha tunapata vifaa kinga, dawa na vifaa tiba vya kutosha.” Amsema. Aidha amebainisha kwamba serikali inafanya uchunguzi kwa wasafiri wote kutoka bara la Asia, kwenye mipaka na wanaoingia nchini kupitia viwanja wa ndege vilivyopo Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza. Ameendelea kubainisha kuwa, katika bandari ya Dar es Salaam, wiki mbili zilizopita waliwachunguza watu 1520 walioingia Tanzania kutokea China kupitia maeneo hayo na waliotumia mipaka mbalimbali na viwanja vya ndege. Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto nchini Tanzania amefafanua kuwa, Wizara inavyo vipima joto 140 (vya mkono 125 na vya kupima watu wengi kwa Mpigo 15 ) ambavyo tayari vimefungwa kwenye mipaka.
Wakati huo huo shirika moja la China limeunda kifaa kinachogundua haraka virusi vya Corona. Shirika la Teknolojia ya masuala ya Biolojia ya 'Sansure Biotech' ya China imetangaza leo kwamba, imefanikiwa kuunda kifaa hicho cha kugundua haraka virusi hivyo vinavyozidi kusambaa duniani. Kwa mujibu wa shirika hilo, kifaa hicho kinaweza kugundua virusi vya maradhi hayo katika kipindi cha dakika 30. Kifaa hicho cha mfumo wa sanduku ambacho kimethibitishwa na idara ya taifa ya usimamizi wa vifaa tiba ya China na kupata kibali pia, kinaweza kuwa na taathira ya kuzuia ongezeko la maradhi hayo. Kamisheni ya kitaifa ya tiba nchini China imetangaza leo kwamba, idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na virusi vya Corona imefikia 132 na watu wengine elfu sita tayari wameambukizwa. Virusi vya Corona viliibuka mwishoni mwa mwaka jana katika soko la vyakula vya baharini la mji wa Wuhan na hadi sasa vimeshaenea katika nchi nyingine 14 za dunia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇