Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa
hafla ya makabidhiano ya vitanda vya wodi ya watoto wanaohitaji
uangalizi maalumu (PICU) ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, vitanda hivyo
vimetolewa na Benki ya NMB.
Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi MNH Bi. Zuhura Mawona akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Mwakilishi wa Benki ya NMB Bw. Juma Kamoli akikabidhi rasmi vitanda hivyo kwa Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy Mwalimu akiwa kwenye
picha ya pamoja na baadhi ya Madaktari na Wauguzi wa wodi ya watoto
wenye kuhitaji uangalizi maalumu (PICU),pamoja na wawakilishi wa Benki
ya NMB.
………………..
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ameziomba sekta
binafsi ikiwamo benki ya NMB kuelendelea kushirikiana na Serikali katika
kuboresha huduma za afya nchini.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo
wakati akipokea msaada wa vitanda vitano kutoka Benki ya NMB vyenye
thamani ya shilingi milioni 35 kwa ajili ya wodi ya watoto wanaohitaji
huduma ya uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) na vitanda 10 pamoja na magodoro 10 kwa Hospitali ya
Muhimbili-Mloganzila vyenye thamani ya shilingi milioni 10.
Amesema sekta ya binafsi ina
wajibu mkubwa katika kuchangia shughuli za maendeleo ikiwamo huduma za
afya kama ilivyofanya Benki ya NMB.
“Nawapongeza NMB kwa jitihada zake
kwani msaada vitanda vya ICU ni msaada mkubwa kwa watoto na pia NMB
inafanya vizuri kurejesha fedha zake kwa jamii,” amesema Waziri Ummy
Mwalimu.
Pia, Waziri Ummy amesema kutokana
na juhudi za Serikali ya awamu ya tano, Muhimbili inaendelea kutoa
huduma za ubingwa wa juu ikiwamo huduma ya kupandikiza figo, huduma ya
kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto wenye matatizo ya kusikia.
Naye mwakilishi wa Benki ya NMB,
Bw. Juma Kimori ameipongeza Muhimbili na serikali ya awamu ya tano kwa
kuboresha huduma za afya.
Bw. Kimori amesema NMB imeweka
utaratibu kutoa misaada katika sekta ya afya kwa kutenga fedha kwa ajili
ya kutoa misaada mbalimbali kwa jamii.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za
Uuguzi MNH, Bi. Zuhura Mawona ameishukuru NMB kwa msaada huo kwa kuwa
umekuja wakati ambapo MNH kwa kushirikiana na wahisani imejenga wodi za
uangalizi maalumu kwa watoto wenye umri kati ya siku 1 hadi siku 28
(NICU) na wenye umri wa siku 29 hadi miaka 14 (PICU), hivyo kuwa na
uhitaji wa vitendea kazi mbalimbali ikiwemo vitanda.
“Vitanda hivi vya kisasa
vinatumia umeme na vinaweza kurekebishika kwa kupandishwa juu na
kushushwa kulingana na uhitaji, hivyo vinasaidia mgonjwa kulazwa katika
mlalo unaofaa na pia kupunguza maumivu ya mgongo kwa wauguzi na
madaktari wakati wa kutoa huduma,”amesema Bi. Zuhura.
Bi zuhura amesema kuwa vitanda
hivyo pia vimesaidia wauguzi kutoa huduma kwa urahisi na ufanisi zaidi
ikiwamo kumwezesha mgonjwa kupumua (Intubation) kwa urahisi.
Pia. Bi. Zuhura ameshukuru NMB kwa
kutoa msaada huu na pia ameiomba kuongeza vitanda vingine kwani
mahitaji ya vitanda ni makubwa kwa watoto wanaohitaji uangalizi maalumu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇