LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 18, 2019

KUWAIT, MWENYEJI WA MKUTANO WA SHIRIKA LA NATO

Mkutano wa NATO nchini Kuwait umefanyika katika fremu ya mpango uliopewa jina la "Ubunifu wa Ushirikiano wa Istanbul". Katika kipindi cha Vita Baridi, shirika la NATO lilikuwa likifanya harakati zake katika eneo la bara Ulaya, lakini baada ya kumalizika vita hivyo shirika hilo la kijeshi limepanua shughuli zake hadi katika maeneo mengine ya dunia. 
Kupanuliwa shughuli na harakati za shirika hilo katika maeneo mengine ya dunia kumefanyika kupitia mipango mipya ukiwemo ule uliopewa jina la "Ubunifu wa Ushirikiano wa Istanbul." Mpango huo ulibuniwa mwaka 2004 katika kikao kilichofanyika Istanbul nchini Uturuki kama njia ya ushirikiano wa kiusalama na nchi za Ghuba ya Uajemi zinazojumuisha nchi za Imarati, Kuwait, Qatar na Bahrain. Mkutano wa jana nchini Kuwait uliofanyika kwa mnasaba wa kutimia miaka 15 tangu baada ya kuanza kutekelezwa mpango wa "Ubunifu wa Ushirikiano wa Istanbul", umeshirikisha wawakilishi wa nchi hizo nne za Kiarabu na maafisa wa masuala ya usalama wa nchi za Saudi Arabia, Oman na Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (GCC).  
Kutokana na umuhimu wake makhsusi wa kijiografia na kisiasa, eneo la Ghuba ya Uajemi daima limekuwa na nafasi muhimu kwa madola makubwa hususan yale ya Magharibi ambayo yana mchango mkubwa katika kuzusha na kuibua mizozo na migogoro katika eneo hilo. Nchi hizo zinafanya jitihada za kuzidisha satua na ushawishi wao katika eneo hilo muhimu kupitia miungano na mashirika ya kijeshi. Ni kwa msingi huo ndipo kukatolewa fikra ya kuanzishwa muungano wa kijeshi wa baharini katika eneo la Ghuba ya Uajemi ambao ulianza kazi mwezi Novemba mwaka huu wa 2019. 
Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) ni miongoni mwa mashirika makubwa ya kijeshi yanayotumiwa na madola makubwa ya Magharibi kwa ajili ya kuzidisha uwepo na ushawishi wao katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Mpango huo wa madola ya Magharibi ulitekelezwa kivitendo katika mkutano wa mwaka 2004 mjini Istanbul uliobuni mpango wa ushirikiano uliozijumuisha nchi nne za Kiarabu kati ya 6 wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi.
Lengo lililotangazwa na NATO la mpango huo ni eti kuunganisha usalama wa nchi hizo na ule wa nchi za Ulaya. Kwa msingi huo ofisi ya kwanza na NATO katika Ghuba ya Uajemi ilifunguliwa nchini Kuwait Februari mwaka 2017. Ofisi hiyo inajishughulisha na masuala ya kutoa mafunzo ya kisasa katika nyanja za usalama mtandaoni, usalama wa nishati, kemikali, biolojia na silaha za nyuklia.
Uzinduzi wa ofisi ya NATO nchini Kuwait
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, mpango wa Ubunifu wa Ushirikiano wa Istanbul ni wenzo wa kudhamini maslahi ya kisiasa ya madola makubwa wanachama wa NATO. Hii ni kwa sababu kwa upande mmoja, mpango huo unazidisha satua na ushawishi wa madola ya Magharibi katika nchi hizo kwa kisingizio cha kulinda usalama wao; na katika upande mwingine unasahilisha kuvuka na kupita majeshi na zana za kivita za NATO katika ardhi ya nchi hizo.
Kuhusiana na suala hilo Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg anasema: Mpango wa ushirikiano wa Istanbul unarahisisha kuvuka na kupita majeshi na NATO na kutumwa silaha za shirika hilo nchini Afghanistan.    

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages