Ni kawaida ya Binadamu kutokuwa na shukrani. Historia hapa nchini inaonyesha ni kawaida kwa Marais wanapokuwa madarakani kudhihakiwa, kutukanwa na kubebeshwa kila aina ya lawama. Lakini hukumbukwa sana pindi wanapotoka madarakani.
Tuweke kumbukumbu zetu sawa. Mwalimu Julius Nyerere wakati akiwa madarakani alimwagiwa lawama na tuhuma lukuki kwani wapo waliosema Mwalimu haambiliki na wengine wakadai anaendesha nchi kwa “remote” akiwa Butiama (kijijini kwao). Lakini mara baada ya kung’atuka kwa hiari Urais ndipo sifa za kinafki zilianza kummiminikia huku tukianza kumuita “Baba wa Taifa”. Mara baada umauti kumkuta ndipo unafki ulizidi kwake na leo hii kila kitu kibaya kinachotokea tunasema laiti Mwalimu Nyerere angekuwepo haya yote yasingetokea. Lakini angali hai ama madarakani hatukuyatambua haya zaidi ya kuuendekekeza unafki.
Ama Alhaji Hassan Mwinyi wakati akiwa Rais wa awamu ya pili walimwita mbinafsi, muuzaji nchi kutokana na ubinafsishaji lakini leo hii ni mstaafu wanaanza kummwagia sifa teletele na hata kumwita “Mzee wetu” huku wakijivunia kuchota hekima na busara kutoka kwake lakini angali madarakani hatukuliona hilo. Huu ni unafki mtupu.
Pia Benjamini Mkapa alidhihakiwa kweli kweli wakati wa uongozi wake hadi kufikia hatua ya kumwita ‘ukapa’ badala ya Mkapa kutoka katika neno la ‘ukata’. Lakini leo hii kila anapokatiza ni shangwe, makofi, vifijo, na vigelegele na tukisema afadhali ya Mkapa kuliko wote na wengineo tumewaona wakimpa hata tuzo ya heshima. Jamani! Kama huu si unafki, basi tuuiteje?
Hata Dk. Jakaya Kikwete (JK) alipokuwa madarakani walimuita majina mengi ya hovyo hovyo. Wapo waliomuita “Mzee wa kutabasamu”, Serikali yake ni dhaifa na legelege! Lakini hekima na busara kubwa aliyojaaliwa Dk. Kikwete hakuweza kuwajibu lolote waliokuwa wakimkejeli na badala yake aliwaambia mtanikumbuka.
Kikwete alisema: “Mtaumbuka baada ya 2015”. Dk. Kikwete aliwaambia wanaombeza sasa wataona aibu baada ya kumaliza kipindi chake. Naam! Ni kweli Watu waliokuwa wakimbeza wameanza kuumbuka na kunza kupayuka hadharani kuwa wana mkumbuka.
Wale waliokuwa wakidai JK ni legelege na dhaifu wanataka Rais mkali ndio hao hao hao walisema Rais Magufuli ni dikteta; Wale waliokuwa wanasema JK hawezi kuchukua maamuzi magumu ya kutimua wanaoharibu, ndio hao hao waliosema kuwatumbua “kuwafukuza” wanaoharibu ni kinyume na haki za binadamu; Mara JK hakamati mafisadi Papa ama hawakamati wauzaji madawa ya kulevya walipoanza kukamatwa wanaanza kuwatetea kwa kusema si vyema kuwataja watu majina, mara si vyema kuwakamata waliolitumikia Taifa letu!
Huu ni unafki mkubwa unaoliangamiza Taifa kwa sisi Watanzania kutokuwa wakweli na kuamua kujivisha sura ya undumila kuwili.
Hata haya yanayotokea sasa kwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania kusemwa, kudhihakiwa na kutukanwa tuliyatarajia maana Watu ni wale wale Wanafki na Wazandiki wakubwa na midomo ni ile ile iliyojaa lugha chafu ambao wamekubali kuacha kufikiri kwa ubongo na akili.
*Rais Samia ameyafanya yale tuliyoyatarajia*
Rais Samia ndani ya kipindi kifupi ameweza kufanya mambo makubwa sana yanayogharimu mabilioni kama sio matrilioni.
1. Ameendeleza na kukamilisha miradi yote ya kimkakati yaliyoachwa na mtangulizi wake Hayati Dk. Magufuli. Tumeona SGR ikifanya kazi vyema; Mradi Bwawa la Nyerere umeshaingiza megawatts 2115 kwenye gridi ya Taifa nk.
2. Amesimamia Mradi wa kuhamia Dodoma makao makuu ipasavyo na Serikali imeendelea kubakia Dodoma
3. Amejenga Barabara za juu (flyovers) zote kama zilivyoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi CCM 2020 -2025
4. Anatoa Elimu Bure kuanzia shule ya msingi mpaka Sekondari pamoja na kujenga miundombinu mipya ya kielimu. Kwa wasiojua Rais Samia ndio Rais pekee aliyejenga shule nyingi za msingi na sekondari kuliko Rais yeyote yule. Mpaka sasa amejenga zaidi ya shule 4,050 rekodi hii haijawahi kutokea hapo awali.
5. Ameboresha sekta ya Afya kwa kiwango kikubwa. Leo hii kuna hospital na Wataalamu bingwa wanaofanya operesheni kubwa hapa nchini ambazo awali nilikuwa zinapatikana nje ya nchi, Leo hii upatikanaji wa madawa ni wa kuridhisha mahospitalini kwa kiwango kikunwa
6. Ameimalisha diplomasia baina ya Tanzania na nchi ama mataifa mengineyo.
7. Ndani ya muda mfupi kero ya ukosefu wa madawati iliyodumu kwa muda mrefu imebaki historia shuleni.
8. Serikali yake inajitahidi kulipa madeni ikiwemo kulipa deni la Taifa na kupunguza madeni ya ndani kwa Wataalamu na Watumishi wa umma.
9. Amefanya maboresho makubwa ya kidemokrasia na kutoa uhuru wa kisiasa kwa wote wanaofanya siasa za kistaarabu pasipo kuvunja Sheria, Taratibu na Kanuni za nchi
10. Ameanzisha miradi mikubwa ya kuzalisha umeme nchini na kuhakikisha umeme unaenda mpaka vijijini kupitia mradi wa umeme vijijini wa REA.
Narudia tena kusema Rais Samia anatukanwa, anadhihakiwa, anasulubiwa kwa Kila aina kwa Kila namna wajisikiavyo lakini kamwe hajawahi kukata tamaa, kulipa kisasi Wala kurudi nyuma bali anasonga mbele kwa sababu amejitoa kwa hali na Mali kuhakikisha Watanzania wanapata Maendeleo na Taifa la Tanzania anaendelea kulikomboa kiuchumi, kisiasa na kijamii.
*Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni*
Rais Samia ni Mzalendo, Shujaa, Mpenda haki, Mtetezi wa Wanyonge na Mjenzi imara wa Taifa letu wa kipindi chote.
Na SHILATU, E.J
**
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇