Na Mwandishi wetu
Alipohojiwa
mnamo January mwaka juzi, Dkt. Muhammed Seif Khatib alikuwa na mengi
ya kuzungumzia kuhusu umuhimu wa kuhifadhi historia, ambapo aliweka
bayana kwamba wakati umefika wa kujenga makumbusho ya Taifa ya Mapinduzi
ya Zanzibar, ili kizazi cha sasa na kijacho kiweze kujifunza na
kuipitia historia muhimu kwa Watanzania na wageni kutoka nje.
Dkt.
Khatib anasema ni vema kuonesha katika picha, filamu, maandishi na
sura halisi za historia ya Zanzibar ya wakati huo uliopita wa
utawala wa wageni wa Waajemi, Wareno, Waarabu, Waingereza na hadi hivi
sasa wakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Waafrika inaongozwa na walio
wengi.
“Kwa
kuweka makumbusho na usahihi wa historia ya nyuma ya kabla, wakati na
baada ya Mapinduzi kadhalika na yanayotokea hivi sasa, hayo yote yakiwa
katika makumbusho hio, yatakuwa msingi wa historia ya Zanzibar hatua
ambayo itasaidia kuwekwa wazi mambo yaliyowahi kutokea, hivyo sio rahisi
kwa mtu yoyote ambaye ana agenda ya kupotosha umma kufanya hivyo”,
alisema Dkt. Khatib ambaye unapokutana naye bado anaonekana ni mwenye
nguvu zake na afya tele.
Ila
kwa vile wazo lake la kuwa na kituo cha historia halijafanyiwa kazi,
bado Dkt. Khatib tu anasikitika kwamba hivi sasa ni kweli kabisa mtu
yoyote anaweza akasema vyovyote atakavyo kwa kuwa haijui historia vema
na wala hana mahali pa kurejea historia ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Wengi
hawajui kwamba watu walitoka Kongo, Malawi, Kigoma na Tabora
wakibebeshwa pembe za Ndovu na kusafiri kwa mguu, wakifuata njia ya reli
ya kati, mpaka Bagamoyo na kusafirishwa na jahazi mpaka Unguja na
kuwekwa sokoni kuuzwa kama samaki katika soko la watumwa. Huu
ndio ukweli ambao sio tu wengi hawaujui, bali pia yapasa waujue” anasema
Dkt. Khatib.
Anatoa
mfano wa Rwanda iliyokumbwa na mauaji ya kimbari mwaka 1994,
na kwamba kwa kutambua kuwa hicho siyo kitu kizuri kutokea tena hapa
duniani nchi hiyo imeweka makumbusho ya kitaifa ambayo japo
yanahuzunisha lakini ndio ukweli wenyewe.
“Ukweli
kwenye makumbusho hayo mjini Kigali utajionea maelfu ya mafuvu ya
vichwa vya watu waliouwawa yalivyopangwa kiasi hata huwezi kuamini kama
hiyo ndiyo iliyokuwa hali halisi ya mauaji ya kimbari yalivyotokea hapa
duniani.
“Kwa
Wanyarwanda na watu wengine duniani, makumbusho ya kimbari ni sehemu ya
Utalii ikizingatia msemo wa waswahili wanasema kuona ni kuamini”,
anasema Dkt. Khatib.
Anaongeza
kwamba siyo Rwanda tu, bali hata nchi ya Namibia kuna jumba la
makumbusho la mauaji yaliyofanywa na Wajerumani kwa kabila la Waherero
ambao anasema waliuwawa katika vita ya kwanza ya dunia, ambapo takribani
Waherero nusu ya milioni waliuwawa na hivi karibuni Waherero wa Namibia
walikuwa wanaomba fidia kwa Serikali ya Ujerumani, ingawa Ujerumani
wameomba msamaha kwa mauaji hayo ya kimbari.
Dkt.
Khatib anasema kwamba Uingereza ni nchi inayoongoza duniani kwa kuweka
kumbukumbu zake katika makumbusho za kifalme, Kimataifa, Kitaifa, Vita,
Silaha, Bahari, Mtu Binafsi, Jiji au Mji husika, ikiwa ina zaidi ya
makumbusho 55 ambayo yanafahamika duniani. Mfano ikiwa ni British Museum
London, Natural History Museum London, National Gallery London, Science
Museum London, Victoria ana Albert Museum, National Maritime Museum,
Museum of London City, National Portrait Gallery, National Army Museum,
Sir Johns Soanes Museum, Wallace Collection London, National War Museum
na kadhalika.
“Kujengwa
kwa kituo cha makumbusho Zanzibar pia kitasaidia kuingiza fedha ikiwa
kama sehemu ya Utalii wa historia kama wanavyofanya nchi zingine, ambapo
mtu anayehitaji kuijua historia hiyo atapata kila kitu mahala pamoja
bila kusumbuka”, anamalizia Dkt. Khatib.
Yote
hayo tisa, mimi baada ya kufanya utafiti wa kina nikakuta kumbe hata
yeye mwenyewe Dkt. Muhammed Seif Khatib ni mmoja wa watu ambao watafaa
kuandikwa historia zao na kuwemo kwenye kituo hicho cha kumbukumbu,
maana kwa kweli kapita kwingi na kufanya mengi na kuishi kwingi na kuona
mengi.
Na
endapo mtu akipata kibarua cha kuandika hiyo historia yake yeye kama
yeye, hakika utapata taabu uanzie wapi ama fani ipi kati ya nyingi
alizopitia na ambazo anazo hadi hii leo - kama ambavyo mimi nimepata
shida kuandika hii sehemu tu ya historia yake hapa.
Baada
ya kuongea nae kwa kina, nikawa najiuliza sijui nianze na hili jina la
Daktari ambalo alilipata rasmi mnamo Novemba 25, 2011 pale alipotunukiwa
Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Mkuu wa Chuo
hicho, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa.
“Hii
ilikuwa Shahada ya Kwanza ya PhD kutoka katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
Ni bahati ilioje mimi kuipata Shahada hii ya juu kitaaluma” anasema Dkt.
Khatib huku akiikumbuka vyema siku hiyo katika viwanja vya UDOM, wakati
aliposimamishwa na kwenda kupiga goti na mbele ya Mhe. Mkapa na
kutunukiwa Shahada hiyo.
Anasema
Mada yake ya kuupata udaktari huo wa Falsafa ilikuwa ni ulinganisho wa
washairi Shaaban Robert wa Tanga (wa karne ya 20) na Muyaka bin Haji wa
Mombasa (wa karne ya 19), akichambua jinsi wanavyomsawiri mwanamke kwa
“chanjo za matakwa ya mwanamume”.
“Nilifarijika
kufikia kiwango hicho cha elimu na kutunukiwa na Rais Mkapa ambaye
niliyefanya kazi nae kwa muda wa miaka 10, akiamini kuwa mmoja wa
mawaziri wake aliowaita “Askari wa Miamvuli”, anasema huku akitabasamu.
Nikajiuliza
labda nianze na historia yake ki-elimu, baada ya kuniambie yeye alisoma
hadi darasa la nane lakini alijiendeleza mwenyewe na hatimaye kupata
Shahada yake ya Kwanza, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1978
na Shahada ya Pili aliipata mwaka 1982 Uingereza SOAS.
Kwa
kweli Dkt. Khatib, ambaye baada ya kuhudumu kupitia Umoja wa Vijana
kama mbunge wa viti maalumu baadaye akahudumu kama mbunge wa Uzini kwa
miongo kadhaa, ni changamoto kubwa kumwelezea.
Hasa
ikizingatiwa kwamba yeye pia Mwenyekiti wa BARAZA LA KISWAHILI LA
ZANZIBAR (BAKIZA), Mwenyekiti wa Mapitio ya Kamusi Fasaha la BAKITA
lilochapwa 2010, huku akiwa Mhadhiri wa Muda kwa wanafunzi wa Shahada ya
Uzamili (Masters) katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).
Na
kama hayo yote hayatoshi, hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein alimteua kuwa Mjumbe wa
TUME ya UTUMISHI WA UMMA katika Ofisi ya Rais, Zanzibar.
Tukija
alikokopita huko nyuma, utakuta Dkt. Khatib amewahi kushika nyadhifa
nyingi na kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa
Vijana (1978-82), Katibu Mkuu Umoja huo (1982 - 88) ambapo hapo kwa
vijana amekuwa kiongozi kwa miaka 10.
Amekuwa
Waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu
ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi, na awamu ya Tatu ya Mhe. Mkapa na ya
nne ya Dkt. Jakaya Kikwete (1988-2010), safari hiyo akianzia toka akiwa
mbunge wa viti vya Vijana na baadaye wa Jimbo la Uzini tokea mwaka 1988
hadi alipostaafu mwaka 2015.
Vile
vile amekuwa Mjumbe wa NEC ya CCM tokea 1978 hadi 2017, Mjumbe wa
Kamati Kuu ya chama hicho (1995-2017), na baadaye Katibu wake wa
Oganaizesheni 2012-2017.
Licha
ya kuwa mwanasiasa mwenye nyadhifa mbalimbali, Dkt. Khatib katika muda
wake wa ziada alikuwa mwandishi wa makala za michezo katika gazeti la
Serikali la Daily News, gazeti la chama Uhuru na katika Mzalendo akiwika
na makala yake mashuhuri KIPANGA.
Na
hakuishia magazetini pekee. Huyu bwana pia ni Mwandishi mashuhuri wa
vitabu vikiwemo “Fungate ya Uhuru”, “Wasakatonge”, “Chanjo”, “Vifaru
Weusi”, Utenzi wa Ukombozi wa Zanzibar” na “Taarab Zanzibar”.
Nilipoongea
nae hivi karibuni, Dkt. Khatib amenambia kwamba amehamasika sana na
kitendo cha Mhe. Mkapa kutoa kitabu cha historia ya maisha yake, na
kuongezea yeye pia tayari yuko mbioni kufuata nyayo za kiongozi huyo
mahiri kwa kuandaa kitabu cha maisha yake.
Hapana
shaka kwamba kitabu chake hicho kitatuhadithia sio tu alivyokiuwa na
kipawa cha kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, bali pia jinsi
alivyokuwa mwanasoka hodari wa timu ya Kikwajuni almaarufu kama “KISK”
na timu ya Taifa ya Zanzibar - bila kusahau alikuwa pia Nahodha wa timu
ya soka ya Chuo cha Nkrumah.
Dkt.
Khatibu, ambaye anasema hobby zake kubwa ni kufanya jogging, kusoma
vitabu na makala mbaklimbali, pia ameshatunga nyimbo kibao za taarabu
zinazoimbwa na wasanii wa bendi mbalimbali ikiwemo Culture. Baadhi yake
ni "Nia yangu sigeuzi", "Paka shume", "Wewe peke yako," "Nakupenda" na
nyingine kibao.
Hadi nafikia hapa, bado sijajua nianzie wapi kumwelezea huyu mwanasiasa, mwanamichezo, mwanahabari, mshairi, ambaye kwa sasa anasimamia kwa karibu kampuni ya familia ya Zanzibar Media Corporation akiwa Mkurugenzi wa Zenj Fm na Zenj Tv.
Mie
nashauri tusubiri tu hicho kitabu cha maisha yake ili tumjue kwa
undani, na vile vile mamlaka zinazohusika, zikipendezwa, zianzishe hicho
kituo cha kumbukumbu na historia ya Zanzibar kama anavyoshauiri - na
kujumuisha kitabu chake kuwa miongoni mwa vitu vitavyowekwa humo. Ama
hakika, kwa maoni yangu, anastahili kuwemo kama ambavyo Wazanzibari
wengi wa aina yake wanavyostahili.
Dkt Muhammed Seif Khatib aliposimamishwa ili kwenda kupiga goti Novemba
25, 2011 pale alipotunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu
cha Dodoma na Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe.
Benjamin William Mkapa. Hii ilikuwa Shahada ya Kwanza ya PhD ya Chuo Kikuu cha Dodoma toka kianzishwe.
Dkt Muhammed Seif Khatib alipotunukiwa
Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Mkuu wa Chuo
hicho, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa, Novemba 25, 2011. Hii ilikuwa Shahada ya Kwanza ya PhD ya Chuo Kikuu cha Dodoma toka kianzishwe.
Dkt Muhammed Seif Khatib katika tafrija ya kifamilia baada ya kutunukiwa
Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Mkuu wa Chuo
hicho, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa, Novemba 25, 2011. Hii ilikuwa Shahada ya Kwanza ya PhD ya Chuo Kikuu cha Dodoma toka kianzishwe.
Akiwa
Nahodha wa timu ya Chuo cha Nkrumah Dkt. Khatib akipokea kikombe cha
ubingwa toka kwa Raisw wa kwanza wa Zanzaibar Sheikh Abeid Amani Karume
Dkt. Khatib akimkabidhi Mwalimu Nyerere
Tunzo ya Kimataifa akiwa Katibu Mkuu wa Vijana mbele ya Rais Ali Hassan
Mwinyi. Anasema hakumbuki mwaka ila ilikuwa ni kabla ya mwaka 1988.
Dkt Muhammed Seif Khatib wa pili kushoto waliosimama mbele. Hili lilikuwa baraza la mawaziri la kipindi cha pili cha Rais wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa. |
Picha
ya pamoja ya viongozi wa BAKITA na BAKIZA baada ya kikao cha
mashauriano. Kutoka kulia waliosimama mbele ni Bi Mwanahija (Katibu
Mtendaji - BAKIZA), Dkt.Muhammed Seif Khatib (Mwenyekiti - BAKIZA),
Dkt.Sewangi (Katibu Mtendaji- BAKITA) na Dkt.Samwel ( Mwenyekiti -
BAKITA) na wajumbe wengine.
|
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇