Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamii-Dodoma
WAZIRI wa Kilimo na Chakula Japhet Hasunga amesema umefika wakati kwa Watanzania kujikita katika kilimo hai kwani kuna ardhi ya kutosha na kilimo hicho kikifanikiwa nchi itakuwa imepunguza gharama kubwa ya uzalishaji unaotokana na kilimo kinachotumia kemikali huku akisisitiza Serikali itashirikiana na wadau kuhakikisha chakula kinacholiwa kunakuwa salama .
Pamoja na mambo mengine Waziri Hasunga amesema Serikali inatambua umuhimu wa kilimo hai nchini na kwamba katika mabadiliko makubwa ya sekta ya kilimo kuna mchakato wa kutungwa kwa sheria ya kilimo ambapo kilimo hai kitapewa kipaumbele na msukumo mkubwa.
Waziri Hasunga ameyasema hayo leo Novemba 26 mwaka 2019 wakati anafungua Kongamano la Kimataifa ambalo limewakutanisha wadau wa kilimo hai ndani na nje ya Afrika ambapo ametumia nafasi hiyo kutoa maelezo ya kina kuhusu kilimo hicho huku akiwataka Watanzania kujihusisha nacho.
Amesema kongamano hilo limekuja wakati muafaka kwasababu Wizara iko katika mabadiliko hayo makubwa yakiwemo ya mkachakato wa kutunga sheria inayohusu sekta ya kilimo.
"Watanzania kila siku wanaongezeka na hivyo lazima kuwe na uhakika wa kuzalisha kilimo cha uhakika, kabla ya miaka mitano hii kumalizika lazima tuwe na sheria ya kilimo ambayo mbali ya kujadili mambo mengine itajikita pia katika kukiendeleza kilimo Kilimo hai,"amesema.
Ameongeza katika mabadiliko makubwa ambayo yanafanyika ndani ya Wizara hiyo pia Wizara itakuwa na kanzi data ambayo itawatambua wakulima wote nchini na aina ya kilimo wanachofanya tofauti na sasa kila mtu anajiita mkulima na Serikali haijui analima nini.
Amesisitiza Serikali inatambua umuhimu wa kilimo hai nchini Tanzania. "Nawapongeza Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM) kwa kazi mnayofanya katika kuendeleza kilimo hai. Nitumie nafasi hii kukushukuru Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) linavyowekeza katika kilimo hai ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti."
Hata hivyo amesema mazao ya kilimo hai yanasoko kubwa Duniani na Tanzania haiwezi kujiweka nyuma,hivyo nayo inakila sababu ya kujikita katika kilimo hicho kisichotumia kemikali. Amesema kuna faida nyingi za kilimohai likiwemo soko la uhakika kwani mahitaji ni makubwa na hiyo inatokana na ukweli uliopo vyakula vitokanavyo na kilimo hicho havina madhara ya kiafya tofauti na mazao ya kilimo kinachotumikia kemikali ambacho kimesababisha magonjwa mengi kiafya.
Hata hivyo amesema kwamba amemsikia Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge kutaka kuwepo na Idara maalumu ambayo itajihusisha kusimamia kilimo hai nchini ambapo katika hilo amesema hayo kwake ni maagizo na hivyo si kuanzisha Idara bali kuwa na Kurugenzi itakayokuwa na mamlaka kamili.
"Kwa kutambua umuhimu wa kilimo hai Serikali kupitia Wizara ya Kilimo tutaweka mikakati wa kukiendeleza kilimo hai ambacho mbali ya mazao yake kuwa na soko,kinafaida kubwa kiafya.Katika Dunia ya sasa eneo la chakula ni muhimu kuwa na uangalizi kwani watu wanaweza kutumia chakula kuwamaliza wananchi.Hivyo Serikali iwe makini kwa kuhakikisha chakula tunachozalisha kinakuwa cha uhakika na hili ni jukumu letu,"amesema Waziri Hasunga
Amesisitiza kwa mkakati ambao Serikali imeuweka katika kilimo hai wanaamini nchi ya Tanzania itakuwa kati ya nchi zitakazokuwa zinazalisha law wingi chakula kinachotokana na kilimo hai.
Amezungumzia umuhimu wa ubora na usalama wa mbegu nchini kwa kuhakikisha Hazina madhara kwa walaji huku ukitumia nafasi hiyo kueleza hakuna sababu ya wakulima kutumia mbolea ya kiwandani kama ardhi inajitosheleza law hotuba.
Kwa upande wake Rais wa Kilimo Hai Afrika ambaye pia ni Rais waTaasisi ya Kuendeleza Kilimo hai Tanzania (TOAM) Jordan Gama amesema pamoja na mambo mengine kongamano la wadau hao wa kilimo hai unalenga kujadili kwa kina changamoto na mafanikio yaliyopo.
"Dhumuni la kongamano hili litakalofanyika kwa siku mbili ni kuwaleta wadau mbalimbali wakiwamo watunga sera, wasimamia sheria,kanuni na miongozi, wanasiasa, watoa uamuzi, wazalishaji, wanunuzi pamoja na wadau wengine kutumia nafasi hiyo kwa kina kujadiliana, kupeana habari na kubadilisha maarifa kuhusu kuendeleza kilimo hai nchini,"amesema.
Pia katika mkutano huo mkuu wa wadau wataangalia kwa kina kuhusu kilimo hai kwa Tanzania , Afrika na Duniani kwa ujumla ili kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji wa mazao kupitia kilimo hicho ambacho kimsingi kina mafanikio mengi makubwa na wakati huo huo kunachangamoto zake.
Amesema baada ya majadiliano, wadau hao watatoka na mapendekezo ambayo yatapelekwa kwa Serikali kwa ajili ya kupata mfumo mzuri wa kuendeleza kilimo hai nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati Bunge ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mahmoud Mgimwa amesema kuwa kwa niaba ya wabunge wanashukuru kupata fursa ya kushiriki katika kongamano la kilimohai na kwamba wao ndio mara yao ya kwanza kushiriki.
Hata hivyo amesema sera ya kilimo hai ipo lakini hakijafanikiwa vya kutosha na ni amani yao Waziri wa Kilomo na Chakula atatoa muelekeo mzuri kuhusu kilimo hicho na kufafanua kuwa ndani ya Wizara ya kilimo hakuna Kitengo rasmi cha kilimohai.
Amesema kilimo hai kinafaida kubwa na kwamba ni matarajio yao Serikali itaangalia namna nzuri ya kuendeleza kilimo hai na kwamba wakulima zaidi ya 200,000 wanajihusisha na kilimo hicho kisicho na shaka,hivyo inahitajika mkakati madhubuti huku akifafanua pamoja na faida za kilimo hicho bado Serikali imekuwa kimya.
'Kupitia mkutano huo , wabunge tunatoa ombi kwako Waziri wa Kilimo na Chakula kuwekeza katika kilimo hai.
Amesema kna nchi kama India wameamua kujikita katika kilimo hai ambacho.mazao yake ni salama na Bora kiafya na hivyo tukiwekeza katika kilimo hicho hata magonjwa yatapungua,"amesema.
Mmoja wa Champion wa TOAM Dk.Mwatima Juma ambaye amejikita katika kilimo hai amefafanua kuwa Taasisi ya TOAM ilianzishwa mwaka 2005 kwa kushirkisha wadau mbalimbali katika kuangalia kilimo hicho katika mnyororo wa thamani wa mazao yatokanayo na kilimo hicho.
Waziri wa Kilimo na Chakula, Mhe Japhet Hasunga akiwa kwenye mabanda ya maonesho katika kongamano la kilimo jijini Dodoma leo.
Waziri wa Kilimo na Chakula, Mhe Japhet Hasunga akizungumza na washiriki wa kongamano la kilimo hai lililofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.
Wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Nchi wakiwa wamejitokeza katika kongamano la kilimo hai lililofanyika jijini Dodoma leo na kuhudhuriwa na Waziri wa Kilimo na Chakula, Japhet Hasunga.
Champion wa TOAM, Dk Mwatima Juma akielezea umuhimu wa kilimo hai katkma kongamano la Kilimo lililofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Mahmoud Mgimwa akitoa mchango wake kwenye kongamano hilo la Kilimo hai.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇