Charles James,Michuzi TV
SERIKALI
imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu
kwa watu wenye uhitaji maalum ili kuweza kuwanasua katika kundi la
ombaomba na kuwafanya wawe tegemezi kwa kuwa na miradi yenye kuwapa
kipato.
Kauli
hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe Stella Ikupa wakati alipokua
akifunga mafunzo ya Ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu katika Kata ya
Buigiri Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Mafunzo
hayo yalianza toka Novemba 29 ambapo yaliandaliwa na Taasisi ya NAKUA
NA TAIFA LANGU kwa kushirikiana na Diwani wa Kata hiyo Mhe Kenneth Lindi
ambapo yalihusisha watu wenye ulemavu na wanawake.
Elimu
iliyotolewa ni Elimu ya kujitambua, Elimu ya usindikaji bidhaa kwa
vitendo, Elimu ya masoko, Athari ya matumizi ya rushwa katika
upatikanaji wa huduma, Umuhimu na utaratibu wa kuunda vikundi vya
walemavu na wanawake pamoja na Elimu ya matumizi sahihi ya fedha za
mikopo.
Akizungumza
na wahitimu hao, Naibu Waziri Ikupa amempongeza Mkurugenzi wa Taasisi
hiyo ya NAKUA NA TAIFA LANGU, Jessica Mshama kwa uzalendo aliouonesha
kwa kuamua kutoa elimu kwa watanzania wenzake ambayo itawaondoa kwenye
lindi la umaskini.
"
Nikupongeze sana Jessica umefanya jambo kubwa siyo tu kwa Wananchi wa
Buigiri bali kwa Taifa lako kwa ujumla. Elimu hii uliyowapa ina manufaa
makubwa kwao wenyewe na hata kwa kizazi chao. Niwaahidi Serikali
itaendelea kushirikiana na wadau wote wa maendeleo katika kuwakomboa
watu wetu," Amesema Mhe Ikupa.
Amesema
ili kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda ni lazima kila kundi nchini
lihusike katika uzalishaji na kuwapongeza wahitimu hao kwa kuelewa
mafunzo vizuri na kuanza kutengeneza bidhaa zao ikiwemo Ubuyu, Siagi ya
Karanga pamoja na Sabuni.
Nae
Mkurugenzi wa NAKUA NA TAIFA LANGU, Jessica Mshama amesema lengo la
mafunzo hayo ni kuwapa elimu ya kujitegemea watu wenye ulemavu ili
kuepukana na dhana ya kwamba walemavu wote ni ombaomba.
Amesema
Serikali ya awamu ya tano imepiga hatua kwenye maendeleo hivyo wao kama
wadau wana kila sababu ya kusaidia Rais Magufuli katika kufikia uchumi
wa kati ifikapo mwaka 2025.
" Mhe
Waziri tunashukuru kwa kufungua na kufunga mafunzo haya. Tunakuahidi
kuwa Taasisi yetu itaendelea kutoa mafunzo haya Nchi nzima lakini pia
kuwatafutia masoko ya bidhaa wanazotengeneza hawa wahitimu.
Tayari
Dodoma tushatoa elimu kwa watu 300 hapa Chamwino na Wilaya ya Chemba,
tutaenda Kongwa, Mpwapwa na Wilaya zingine. Lakini lengo letu ni kuona
tunawainua kiuchumi walemavu na wanawake nchini," Amesema Jessica.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata hiyo, Kenneth Yindi ameishukuru Serikali na
Taasisi hiyo kwa kutoa mafunzo hayo ambayo anaamini yataenda kubadilisha
mtazamo na fikra za wananchi wa Kata ya Buigiri.
Amesema
mafunzo hayo yamewasaidia kuweza kujitambua na kutengeneza bidhaa
mbalimbali ambazo zitakua na nembo ya Buigiri jambo ambalo litasaidia
Kata yao kukua kimaendeleo na kuvutia watu kuja kuwekeza na hivyo
kuongeza mapato ndani ya Halmashauri yao.
"
Hakika tunaipongeza Taasisi ya NAKUA NA TAIFA LANGU kwa kuendesha
mafunzo haya, wametoa kiasi cha Sh Milioni Tatu za ueneshaji sambamba na
walimu wawili, huu ni uzalendo mkubwa waliouonesha kwetu na tuwaombe
waendelee kushirikiana na Serikali yetu ili kufikia kundi kubwa la watu
wenye uhitaji," Amesema Yindi.
Mmoja
wa wahitimu wa mafunzo hayo, John Masaka ameishukuru Serikali kwa
kuendelea kushirikiana na wadau wa Maendeleo katika kufanikisha
inawakomboa wananchi wake na kuahidi kutumia mafunzo hayo vizuri ili
kujipatia kipato na kuepukana na dhana ya kwamba watu wa Dodoma ni
ombaomba.
Pamoja
na kuwakabidhi vyeti vya kuhitimu Naibu Waziri Ikupa alifungua pia Soko
la Buigiri kwa ajili ya walemavu hao na kumtaka Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Chamwino kuwaongezea kiasi cha Sh Milioni Tatu ili waweze
kukuza mitaji yao.
Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Mhe
Stella Ikupa akikata utepe kuashiria kufungua Soko la Buigiri ambapo
litatumika na watu wenye ulemavu waliomaliza mafunzo ya Ujasiriamali.
Mkurugenzi
wa Taasisi ya NAKUA NA TAIFA LANGU, Jessica Mshama akizungumza na
wahitimu wa mafunzo hayo ambayo Taasisi yake imekua ikiendesha. Kushoto
ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Stella Ikupa.
Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Mhe
Stella Ikupa akisikiliza maelezo ya mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya
Ujasiriamali katika Kata ya Buigiri wilayani Chamwino ambalo baadhi ya
bidhaa wanazozitengeneza ni pamoja na Siagi ya Karanga na Ubuyu.
Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Stella Ikupa akizungumza na
wahitimu wa mafunzo ya Ujasiriamali wilayani Chamwino, Dodoma.
Diwani
wa Kata ya Buigiri, Kenneth Yindi akizungumza na wahitimu wa mafunzo
hayo ya Ujasiriamali wapatao 200 ambao ni Walemavu na Wanawake.
Naibu
Waziri Stella Ikupa akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo ya
Ujasiriamali yaliyotolewa na Taasisi ya NAKUA NA TAIFA LANGU katika Kata
ya Buigiri Wilayani Chamwino.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇