Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua kongamano la
Uwekezaji na Biashara Mtwara kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu cha
Mtwara, Novemba 1, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi
ya washiriki wa Kongamano la Uwekezaji na Biashara Mtwara,
wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozindua Kongamano
hilo kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu cha Mtwara, Novemba 1, 2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
MKURUGENZI MTWARA ACHUKULIWE HATUA-MAJALIWA
* Ni baada ya kumtoza mwekezaji sh. milioni 31 za kuendesha vikao
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema mtu yoyote anayekwaza wawekezaji nchini
atachukuliwa hatua kali, hivyo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwaamchukulie
hatua Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara, Bw. Maisha Selemani
Mtipa baada ya kumtaka mwekezaji alipe sh. milioni 31.6 kwa ajili ya
gharama za vikao ili aweze kupatiwa eneo.
Ametoa
agizo hilo leo (Ijumaa, Novemba 01, 2019), wakati akifungua Kongamano
la Uwekezaji na Maonesho ya Biashara mkoa wa Mtwara lililofanyika kwenye
Viwanja vya Chuo cha Ualimu Mtwara. “Yoyote anayekwaza uwekezaji nchini
kwa kuwasumbua wawekezaji tutamshughulikia kabla ya kuwasumbua
wawekezaji.”
Amesema
Bw. Mtipa amemwandikia barua mwekezaji wa kampuni ya MBR Internation
Company Limited akimtaka alipe sh. milioni 31.6 kwa ajili y a kulipa
kamati mbalimbali zikiwemo sh. milioni 1.95 kwa kamati ya Menejimenti ya
Halmashauri.
Waziri
Mkuu amesema “fedha nyingine sh. milioni 2.27 kwa kamati ya kugawa
ardhi ya wilaya, sh. milioni 4.43 kamati ya Uchumi Ujenzi na Mazingira,
Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango sh. milioni 5.14 na sh milioni 17.79
Baraza la madiwani ili wagawane tu, huu ni utaratibu wa wapi? huku ni
kufukuza na kukwaza wawekezaji.”
Waziri
Mkuu amesema Serikali imeshaondoa tozo zaidi ya 150 zilizokuwa
zinakwaza wawekezaji kupata uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini,
hivyo haitaki kusikia mahali popote panawekwa tozo zenye kuwakwaza
wawekezaji. Amesema hatua zitakazochukuliwa kwa Bw. Mtipa ziwe fundisho
kwa halmashauri zote nchini.
Mapema,
Waziri Mkuu alizungumzia uuzwaji wa korosho na kuagiza kwamba mfumo
uliotumika katika mnada wa kwanza wa uuzwaji wa zao la korosho
uliofanyika jana (Alhamisi, Oktoba 31, 2019) ndio unaopaswa kuendelea,
hivyo ameagiza wahusika wausimamie vizuri ili usiingie dosari.
Alisema
Serikali ilibaini changamoto katika uuzwaji wa mazao mengine ya pamba
na kahawa ya uwepo wa watu ambao wananunua mazao nje ya mfumo kama
kangomba, hivyo ni muhimu wakadhibitiwa ili fedha zote ziende kwa
wakulima.
Pia
Waziri Mkuu aliagiza maandalizi yawe yanakwenda pamoja na msimu kama
suala la magunia wasiachiwe watu wa ushirika pekee bali Wakuu wa Mikoa
na Wilaya nao washiriki katika kutatua tatizo hilo ili minada ifanyike
kikamilifu.
Pia
chama kikuu cha ushirika pamoja na vyama vya msingi wazuie kuwepo kwa
makato ya hovyo ambayo yalishaondolewa na Serikali ili kuhakikisha
mkulima haumizwi kwa kupunguzwa kwa malipo yake.
Amewataka
viongozi hao wasimamie mtiririko wa fedha kutoka kwa wafanyabiashara
kwenda kwa mkulima na wahakikishe zinaingizwa katika akaunti za
wakulima. Pia sheria ya ununuzi isimamiwe baada ya mnunuzi kupewa zabuni
anatakiwa alipe ndani ya siku nne. “Sheria hii itaondoa watu wa kati na
kumwezesha mkulima kulipwa fedha zake kwa wakati.”
Kwa upande wake,
Mkuu wa Mkoa amesema amesema wanunuzi wote wametakiwa wahakikishe
wakulima wanalipwa kwa wakati. “Bei ya chini katika mnada wa korosho
uliofanyika Mtwara ilikuwa sh. 2,409 na bei ya juu ilikuwa 2,559 na hali
inaonesha uhitaji wa korosho duniani ni mkubwa kutokana na ubora wake.”
Amesema
chama cha ushirika cha TANECU waliingiza sokoni tani 13,000 huku
mahitaji yakiwa ni tani 40,000 na chama cha ushirika cha MAMCU
walipelela sokoni tani 7,000 na mahitaji yalikuwa tani 22,000 hivyo
wafanyabiashara wengi jana walikosa korosho.
Akizungumziakuhusu
kilimo cha zao la korosho, Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa mkoa
wa Mtwara kuwa wasibweteke kwani mikoa mingine nayo imeanza kulima
korosho, hivyo waweke mikakati mizuri ili zao la korosho liendelee kuwa
zao kuu la biashara kwa mkoa.
Amesema
Serikali kwa upande wake, itaendelea kuweka mazingira rafiki na
miundombinu wezeshi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje
kuwekeza mkoani Mtwara.
“Tusisahau
kuwaMkoa wa Mtwara ni korosho na korosho ndiyo mkoa. Hili
linadhihirishwa na usemi wa wenyeji kuwa korosho ni dhahabu ya kijani.
Mtwara ndiyo mzalishaji mkubwa wa korosho Tanzania, huzalisha zaidi ya
asilimia 65 ya korosho zote nchini.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaasa wawekezaji wote kwamba waondoe
hofu kuhusu kuwekeza Mtwara kwa sababu mkoa wa Mtwara wa sasa ni tofauti
na Mtwara ile waliyokuwa wanaisikia zamani, uchumi wake unakuwa.
Waziri
Mkuu amesema ushiriki wao kwenye kongamano hilo unaonesha utayari
walionao katika kuiunga mkono Serikali kwa lengo la kuwaletea maendeleo
na kujenga Tanzania ya Uchumi wa Viwanda ambayo wote wanaitamani.
Kongamano
hili na mengine yaliyofanyika kwenye mikoa mbalimbali ni utekelezaji wa
agizo la Waziri Mkuu alilolitoa wakati anafungua Kongamano la tatu la
uwezeshaji wananchi kiuchumi jijini Dodoma Juni 18, 2018, ambapo
aliagiza mikoa yote kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa.
“Niendelee kusisitiza tena kwa mikoa ambayo bado haijatekeleza agizo hili la kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji ifanye hivyo mapema.”
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu amesema licha ya Serikali kuwekeza kwa kiwango
kikubwa kwenye miradi ya kijamii katika Mkoa wa Mtwara, pia imewekeza
kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inachochea kukua kwa uchumi
kwa haraka.
Waziri
Mkuu ameitaja miradi hiyo ni pamoja na upanuzi wa uwanja wa ndege na
bandari ya Mtwara; ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mtwara hadi
Nanyumbu mpakani na Msumbiji; ufufuaji na ujenzi wa viwanda vya kubangua
korosho.
Miradi
mingine ni ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Songea kwa ajili ya
kusafirisha makaa ya mawe kutoka Mchuchuma na chuma kutoka Liganga na
kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia na vyanzo vingine.
Ufunguzi
huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji)
Angellah Kairuki, Waziri wa Kilimo Josephat Hasunga, Waziri wa Viwanda
na Biashara, Innocent Bashungwa,Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi,
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme na watendaji wengine wa
Serikali.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇