Wakazi wa mji wa Beni wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia wamefanya maandamano ya kushinikiza kuondoka nchini humo wanajeshi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO.
Maandamano hayo yalifanyika jana Ijumaa katika barabara za mji huo wa mashariki mwa nchi. Maafisa wa usalama wa Kongo DR walitumia risasi hai na mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika wilaya ya Boikene.
Waandamanaji hao wanawatuhumu askari wa MONUSCO kuwa wameshindwa kuwadhaminia usalama wao, na kwa msingi huo hawapaswi kuendelea kuwa nchini humo.
Meya wa mji wa Butembo, Sylvain Kanyamanda amesema maafisa wa polisi wamewatia mbaroni waandamanaji kadhaa kwa kuzusha ghasia na kufunga barabara muhimu za eneo hilo.
Maandamano hayo yamefanyika siku chache baada ya watu 21 wakiwemo maafisa usalama kadhaa kuuawa, huku wengine wanne wakijeruhiwa, mbali na watoto kadhaa kutekwa nyara katika mashambulizi mawili ya wanamgambo wa ADF usiku wa Jumanne iliyopita.
Aidha hujuma hizo za ADF zilifanyika siku chache baada ya vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutangaza habari ya kuwaangamiza wapiganaji 25 wa kundi hilo la wanamgambo katika mji wa mashariki wa Beni, ulioko katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇