Msajili
wa Hazina, Athumani Mbuttuka akitoa hotuba yake katika hafla ya kupokea
Gawio la Serikali iliyofanyika, Ikulu Chamwino, jijini Dodoma leo.
Picha na Othman Michuzi.
Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii
MSAJILI
wa Hazina Athumani Mbuttuka amesema kwa sasa wanajivunia kuongeza
kiwango cha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi kutoka katika kampuni,
taasisi, na mashirika ya umma yanayotokana na gawio, michango ya
asilimia 15, na mapato ya Taasisi na Mashirika ya Umma, marejesho ya
mtaji uliozidi, na ziada ya mwisho wa mwaka.
Mafanikio
hayo yametokana na utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk.John Magufuli
aliyoyatoa mwaka 2018 wakati wa mashirika, taasisi na kampuni mbalimbali
zikitoa gawio kwa Serikali.
Mbuttuka
amesema hayo leo Ikulu ya Chamwino Mjini Dodoma wakati wa Taasisi,
Mashirika na Kampuni mbalimbali zikabidhi gawio kwa Serikali ambapo
hundi hizo zimepokelewa na Rais Dk.Magufuli.
Amefafanua
kuwa hundi ambazo zimepokelewa zinajumuisha Mapato ya Mwaka wa Fedha
unaoishia Juni 31 mwaka 2019 na kwamba katika kipindi cha miaka mitano,
makusanyo ya mapato kutokana na uwekezaji kwenye mashirika ya umma na
kampuni ambazo Serikali ina hisa yameongezeka kufikia Sh.trilioni 1.05
mwaka 2018/19 kutoka Sh.bilioni 161.04 mwaka 2014/15, ikiwa ni ongezeko
la asilimia 552.
Ameongeza
katika makusanyo hayo, Sh. bilioni 683.23 ya makusanyo yote kwa mwaka
ulioishia Juni 30, 2019 yalipitia katika Akaunti ya Msajili wa Hazina na
Sh.bilioni 370.59 ziliwasilishwa moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa
Serikali kutoka Michango ya Mamlaka ya Bandari Tanzania, Bodi ya Michezo
ya Kubashiri, Mamlaka ya Anga Tanzania; na Shirika la Maendeleo ya
Mafuta na Petroli Tanzania.
Amesema
kuwa mapato hayo yanatokana na gawio, michango ya asilimia 15 na huduma
za jamii. ongezeko hili la mapato limechangiwa na maelekezo yako
thabiti kwa Mashirika na Taasisi za Umma katika kuimarisha makusanyo na
kupunguza matumizi yasiyo na tija; ukusanyaji wa maduhuli kwa mfumo wa
kieletroniki [GePG],
Aidha,
Udhibiti wa Matumizi; na kuongeza usimamizi wa Mashirika ya Umma na
Makampuni yanayomilikiwa kwa hisa chache na Serikali. Masuala mengine ni
ufuatiliaji wa kina na mapitio ya mikataba ya wanahisa, mikataba ya
kimenejimenti na mikataba ya misaada ya utaalamu katika makampuni
yanayomilikiwa kwa hisa chache na Serikali.
Pia,
ufuatiliaji wa matumizi kwa Mashirika na Taasisi za Umma, mapitio ya
sera za gawio, kutoa miongozo kwa bodi za wakurugenzi, kupitia
mipango-mkakati na mipango ya biashara, na kuingia mikataba ya utendaji
na Bodi za Wakurugenzi za Mashirika ya Umma.
Amesema
kuwa ulipaji wa gawio umeimarika zaidi kwenye mashirika ambayo Serikali
inamiliki hisa zaidi ya asilimia 50 ambapo rejesho la mtaji limeendelea
kukua kutoka asilimia 1.5 mwaka 2014/15 hadi asilimia 7.21 mwaka
2018/19 ikilinganishwa na kampuni zinazomiliki hisa chini ya asilimia
50, ambapo rejesho la mtaji limeongezeka kutoka asilimia 5.3 mwaka
2014/15 hadi asilimia 6.64 mwaka 2018/19. Hali hii inaonesha ufanisi
katika Mashirika ya Umma una imarika.
"Idadi
ya Kampuni na Mashirika yanayotoa gawio na kuchangia katika Mfuko Mkuu
wa Serikali ni ndogo ikilinganishwa na idadi iliyopo na ukubwa wa sekta.
Kampuni na Mashirika 40 kati ya 81 yaliyopaswa kutoa gawio yameshindwa
kutokana na kujiendesha kwa hasara au kuwa na mtaji mdogo,"amesema.
Amebainisha
kazi ya kurekebisha Mashirika na Makampuni wanayoyasimamia inaendelea.
Hadi kufikia mwezi Juni 2019, mashirika 15 yaliunganishwa na kuwa
mashirika 6 na shirika moja lilitenganishwa na kuwa mashirika mawili.
Ameongeza
lengo kubwa la kuunganisha au kutenganisha mashirika hayo ni
kuipunguzia Serikali gharama na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma
kwa wananchi.
Wakati
huo huo, amesema kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina, Wizara ya Fedha na
Mipango pamoja na ESRF inaendelea kufanya tathmini ya kina kwa mashirika
yote ya biashara kwa lengo la kubaini hatua stahiki za kuchukua ili
kuboresha utendaji wake kwa ujumla.
Pia
amesema Wizara ya Fedha na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) zinaratibu
zoezi la uhakiki wa mali za umma nchi nzima ambapo mpaka kufikia Juni
30, 2019 idadi ya mali 531 zilikuwa zimetambuliwa na kurejeshwa kwenye
mikoa 10 iliyopitiwa.
Amesema
kati ya mali zilizorejeshwa kuna majengo (337), viwanja (140), mashamba
(10), maghala (41) na mali zingine (3). Aidha, katika mali
zilizobainika kuna kampuni mbili Songwe Water Company Limited na Liquid
Storage Company Ltd ambazo Serikali inamiliki kwa asilimia 100 na 40
mtawalia na zoezi hili bado linaendelea.
Vilevile,
hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2019 OMH ilikuwa imerejesha viwanda 31
vilivyothibitika kutofanya kazi na taratibu za kisheria zinaendelea
katika hatua mbalimbali.
Amesema
wazi kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina inakabiliwa na changamoto ambazo
zikipata ufumbuzi inaweza kuboresha zaidi ukusanyaji wa mapato. Kuhusu
changamoto amesema kuwa mojawapo ni mfumo hafifu wa TEHAMA wa utoaji
taarifa na ufuatiliaji, changamoto za Sheria ya Msajili wa Hazina,
ongezeko la mahitaji ya watumishi wenye utaalamu na uzoefu wa kazi, na
kukosekana kwa Mfuko wa Fedha za Uwekezaji.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇