Indonesia kuwekeza Tanzania
Dodoma, 20 Novemba 2019
Mkutano
wa Jukwaa la Viwanda kati ya Tanzania na Indonesia utafanyika kwenye
Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro jijini Dar Es Salaam tarehe 21
Novemba 2019. Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa
(Mb) anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika mkutano huo ambapo kampuni
kubwa 21 za Indonesia zinazojihusisha katika masuala ya ujenzi wa
miundombinu na usafirishaji; kilimo; usindikaji vyakula; utengenezaji wa
nguo, vifaa tiba na madawa ya binadamu; na uchimbaji wa madini na
taasisi zinazosimamia masuala ya uwekezaji Tanzania (TIC, TPSF, CTI,
TCCIA) zitashiriki katika mkutano huo.
Jukwaa
hilo linatarajiwa kuwa fursa muhimu kwa jumuiya ya wafanyabiashara,
wenye viwanda na wadau mbalimbali wa Tanzania na Indonesia kubadilishana
mawazo, uzoefu na ujuzi pamoja na kuweka mikakati ya kushirikiana
katika sekta ya viwanda kwa faida ya pande zote mbili.
Kutoka
na nchi ya Indonesia kuwa ni kubwa kiuchumi Kusini-Mashariki mwa Asia
na ipo nafasi ya 16 katika kundi la nchi 20 tajiri zaidi duniani (G20),
na uwepo wa fursa nyingi za uwekezaji nchini, ni dhahiri kuwa kongamano
hilo litakuwa na matokeo mazuri katika kuunga mkono juhudi za Serikali
ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda
ifikapo mwaka 2025.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇