*Yasema upinzani wamechungulia mapema wameona hawana nafasi ya kushinda, ndio maana wamejitoa
Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya jamii.
WAKATI
Vyama vya siasa upande wa upinzani nchini vikiwa vimetangaza kujitoa
kwa kutoshiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu wa 2019
unaotarajia kufanyika Novemba 24, Chama Cha Mapinduzi(CCM) kimesema
kinatambua umuhimu na thamani ya uchaguzi huo, hivyo kitashiriki
kikamilifu huku kikitoa rai kwa Serikali kutoyumbishwa na yoyote.
Pia
CCM imeeleza kwa kina hatua mbalimbali za mchakato za uchaguzi huo
ambazo zimefanyika na katika hatua kadhaa muhimu vyama vya upinzani
vimeshiriki hatua kwa hatua na cha kushangaza baada ya kuchukua fomu na
kuzirejesha wametangaza kutoshiriki kwa kutoa sababu ambazo imedai sio
za msingi wowote.
Akizungumza
leo Novemba 13 mwaka 2019, mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Haumphrey
Polepole ameeleza pamoja na mambo mengine uchaguzi huo wa Serikali za
Mitaa unaendeshwa kwa sheria, kanuni na miongozo na hatua mbalimbali za
uandaaji wa kanuni na miongozo vyama vya upinzani walipata nafasi ya
kushiriki.
"Tunazo
kanuni ambazo sote tumeshiriki kwa kuweka maoni yetu tangu mwanzo , ipo
kanuni imeeleza kwa kina mchakato wa uchaguzi lakini kama haitoshi
kanuni hiyo imewekewa muongozo wa vijiji na mitaa kuhusu uchaguzi
utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.Kama haitoshi kanuni na muongozo
umeweka kalenda ikiwemo ya kutoa tarehe ya siku ya kufanyika uchaguzi na
sote tumeshiriki, ukaja mchakato wa kufuatilia uchaguzi wwote
tukashiriki, ikaja hatua ya majina na mipaka ya vijiji na kisha
yakafanyika mambo mengine.
"Ukaja
mchakato wa uandikishaji wa upigaji kura lakini zoezi hilo, pia lipo
katika uchaguzi wa serikali ya mtaa lakini misingi ni mmoja tu
kuandikisha kwenye daftari la mpiga kura na wakati huo huo kuhamasisha
wapiga kura kujiandikisha.Sheria inazuia wanasiasa kutoa elimu ya mpiga
kura na sisi CCM tumejizuia katika hilo.Hivyo tulitumia mikutano ya
ndani na CCM kuandaa wanachama wetu kwa kutumia taasisi za kimuundo
ambazo tunazo ndani ya Chama.
"Wenzetu(vyama
vya upinzani) wakavunja utaratibu kwa kwenda hadharani pamoja na
kutumia mitandao ya kijamii na maeneo mengine. Hata hivyo tuliamua kukaa
kimya maana ni kawaida yao.Hilo likapita na kisha ikaja hatua ya
kukagua orodha ya wapiga kura, sote pamoja na wapinzani tukamaliza
hilo.Nataka kueleza kitu hapa mwaka 2014 wenzetu walitufanyia uhuni
walihamisha wapiga kura kutoka kitongoji kimoja kwenda kingine na
wakifika huko wanapiga kura,"amesema.
Polepole
ameongeza kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu wa Serikali za mitaa
tumekuwa makini kwa kuhakikisha wanaopiga kura ni watu wa eneo
husika.Baada ya kupita hatua zote hizo, CCM waliamua kuingia katika
mchakato wa ndani wa kupata wagombea wao kwa kufuata tararibu za Chama,
ambapo wamehakikisha demokrasia inatumika kwa kila mtu kupata haki
inayostahili.
"Hapo
tuliangalia nani anaweza kusimama kwa niaba ya CCM.Mchakato huo
umefanyika katika ngazi mbalimbali na kwa umakini mkubwa, CCM tunatambua
umuhimu wa uchaguzi huu na hivyo tumejiandaa vya kutosha ikiwa pamoja
na kutoa elimu kuandaa watu wetu kuhakikisha sheria, kanuni na muongozo
wa uchaguzi unafuatwa,"amesema Polepole.
Amesema
kwa bahati mbaya wenzao wa upinzani hawakuwa na mchakato wa kupata
wagombea wao , hivyo CCM na upinzani wakaja kukutana tena tarehe 29
wakati wa kuchukua fomu za kugombea."Tuliwauliza wenzetu vipi mchakato
wa ndani wao hakuwa na majibu zaidi ya kuchukua fomu tu.Mchakato wa
ndani kwa CCM ilikuwa nafasi tosha ya watu kujinoa, hivyo haikuwa tatizo
kujaza fomu.Huenda wenzetu walikuwa wanataka kuchukua wale ambao
wataondoka CCM baada ya kumalizika kwa mchakato wetu wa ndani, lakini
safari hii hilo hakuna wote waliopata nafasi na waliokosa tumebaki
wamoja".
Amefafanua
kwamba, baada ya CCM kubaki wamoja, upinzani ndipo ulipoanza mizengwe
na wakawa wa kwanza kwenda kulalamika ili kuonesha wanaonewa wakati
kabla ya hapo hatua zote walishiriki kikamlifu na kuongeza sheria iko
wazi kwa wale ambao watakuwa na matatizo ya fomu zao na wanahisi
wameonewa wanayo nafasi ya kukata rufaa, lakini wapinzani waliamua
kujitoa badala ya kufuata taratibu za kisheria.
"Wakati
hawa wenzetu wanabwaga manyanga wapo waliokuwa wamechukua fomu, wengine
majina yao yamepitishwa na wengine wamekata rufaa na sheria iko wazi
ukihisi umeonewa kata rufaa lakini wenzetu kabla ya hatua ya kukata
rufaa wakawekwa mpira kwapani.Kumekuwa na matamko kadhaa
yametokea.Chadema ,ACT Wazalendo, NCCR-Mageuzi wametangaza kujitoa na
hata Chama cha Hashim Rungwe nacho kimetangaza kujitoa.Huyu Rungwe
sijawahi kuona uongozi wake wa taifa, sijawahi kuona kikao chao cha
halmashauri kimekaa, hata takwimu zao za uchaguzi uliopita chama cha
Rungwe hakikuambulia kitu.
"Hatukumuona
akienda kuchukua fomu, kurejesha fomu, hakukwenda kukata rufaa, lakini
baada ya vyama vya upinzani kuanza kujitoa naye Rungwe akaita waandishi
wa habari kujitoa, niliuliza kajitoa katika nini?Maana hakuwepo.Baada ya
hapo wameanza kutoa matamko mbalimbali na hapa nasisitiza katika hilo
tulitoa msisitizo kwa Serikali isiyumbe kwenye jambo hilo maana hilo ni
jambo la kisheria na katika sheria sote tulikubaliana na ndio maana
tulishiriki mpaka kuchukua fomu.
"Mtu
akikosea masuala ya sheria, sheria ni msumeno, na ukikosea katika sheria
haina huruma , sisi tunawashukuru sana wana CCM na Watanzania kwa
kutuunga mkono.Tuliamua kupeleka jeshi la wanasheria na mawakili nchi
nzima kwa ajili ya kutoa elimu pamoja na kusaidia mchakato wa kujaza
fomu ambalo ni hatua ya kisheria, wenzetu walishindwa kujaza majina,
wadhamini, namna ya kuandika majina sawasawa kwa mujibu wa tangazo la
serikali kijiji kinaitwajwe, na hayo yote wenzetu hawakuwa nayo maana
hawakujiandaa na mchakato wa uchaguzi,"amesema Polepole.
Hata
hivyo amesema kwa takwimu zilizopo vyama vya upinzani ambao wamechukua
fomu ni ndogo ukilinganisha na ya CCM na hata ya waliorudisha fomu nao
ni ndogo, kwa maana hiyo CCM kabla hata yauchaguzi kufanyika tayari
imeshapata asilimia za ushindi na katika maeneo mengine hakuna hata
mpinzani mmoja aliyechukua fomu kwa ajili ya uchaguzi huo."Hadi sasa
tunavyoongea kuna mitaa tumaeshachukua maana wenzetu hawapo kabisa
huko.Na hii ndio imewatisha na kuamua kuweka mpira kwapani maana ushindi
wetu hautakuwa wa sunami bali ni ushindi kama wa upepo wa kisulisuli
maana ndio habari ya mjini".
Ameeleza
katika uchaguzi wa Serikali za Mtaa CCM wanakwenda wakiwa na ushahidi
ambao unaonekana kwa macho na kwa vitendo kutokana na kazi kubwa
iliyofanywa na Rais Dk.John Magufuli ya kuboresha maisha ya watu kwa
kujenga miundombinu ya huduma muhimu za Watanzania na wanatambua kuwa
kupitia uchaguzi huo wanataka kupata Wana CCM makini ambao watapata
nafasi ya kushinda na kisha kushirikiana na Serikali katika kuleta
maendeleo ya wananchi.
"Kutokana
na mambo makubwa yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais
wetu Dk.Magufuli wale watu wa upinzani wamefanya uungwana na hivyo
wameona mwaka huu ushindi utakuwa ni wa kisuli suli, na hivyo wameamua
kuweka mpira kwapani.Tunaishukuru Serikali katika hili kutoyumba,
imebaki na msimamo wake , hawa wenzetu ukitoa mwanya ndipo wanakuja na
mambo mengine mengi yakiwemo ya kutaka kuongozewa muda,"amesema.
Hata
hivyo ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa TAMISEMI kuhakikisha wanaandaa
taarifa za mchakato wa uchaguzi huo na kwa lugha ya Kingereza kwani
kinachofanywa na upinzani wanaandika taarifa za uongo na kupeleka kwa
mataifa ya Ulaya kuonesha wanaonewa, hivyo TAMISEMI nayo ikiandika kwa
lugha ya Kingereza hakutakuwa na sehemu ya kuongopa kuhusu uchaguzi na
kila kitu kitakuwa wazi.
"Katika
kipindi hiki cha uchaguzi tunafahamu kuna mambo mengi yanayofanyika
kuna watu wachache wasioitakia mema nchi yetu, hivyo watataka kutumia
nafasi hii kutuvuruga.Tunatambua ushirikiano wetu na mataifa mengine
lakini katika mambo ya ndani ni vema wakaheshimu mikataba iliyopo ya
nchi mmoja kutoingilia nchi nyingine kwa mambo yake ya
ndani,"amesisitiza.
Hata
hivyo amesema sio vizuri kutoa siri ya uchaguzi, lakini ameeleza ambavyo
CCM wamejipanda katika uchaguzi kwa kila idadi ya wanachama ambao
wamewekwa kusimamia uchaguzi huo na kufanya kampeni ambapo kwa idadi yao
inatosha kabisa CCM kuifanya ishinde na hilo hawana shaka nalo na
kuongeza kinachoonekana upinzani wanataka kucheza mchezo wa kombolela
lakini wao wamejipanga imara na uchaguzi huo ni muhimu, hivyo hawatakuwa
na mchezo wa aina yoyote.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇