NA PROFESA RWEKAZA MUKANDALA
Mtoto Benjamin William Mkapa, alifundishwa kupika chakula na mama mzazi Stephania akiwa mdogo. Alipokwenda shule hapo kijijini Lupaso, Ndanda na hatimaye St. Francis Pugu na Makerere, alifundishwa kupika, kufinyanga, kubuni na kuchambua mawazo na kuyaweka sawa kama msomi mbunifu na mwandishi. Kitabu hiki ni zao la mpishi wa mawazo mahiri aliyebobea. Ni kitabu cha kurasa mia tatu na kumi na tisa, katika sura ya kumi na sita. Kuna utangulizi ulioandikwa na Mheshimiwa Joaquim Chissano, Rais mstaafu wa Msumbiji, Pia kuna picha nyinge nzuri, na viambatisho viwili. Mchapaji Mkuki na Nyota wamefanya kazi nzuri sana, sikubaini kosa hata moja.
Wasilisho hili linamega simulizi hii katika sehemu kuu tatu. Kwanza tunapewa vionjo vitamu tukielezwa kuzaliwa kwake, kukua na kwenda shule. Hii ilikuwa matayarisho ya kufikia nia au azma yake ya maisha. Kisha tunaletewa mlo wenyewe (main course) uliosheheni kumbukumbu na ngano za huyo kijana sasa mtu mzima akiwa kazini, mpaka akaukwaa urais wa Tanzania. Mwisho tunaelezwa kwa ufupi maisha yake baada ya kumaliza ngwe yake ya miaka kumi ya urais.
2. KUZALIWA, MALEZI NA ELIMU
Baba yake mzazi Mheshimiwa Mzee William Matwani alikuwa mpishi msaidizi huko Mission Ndanda. Wamisionari wakambatiza, wakamfundisha kusoma, kuandika na kuhesabu, na kumfanya Katekista. Alipelekwa Lupaso, ambapo alieneza dini na kufundisha Bush school ya Wamisionari. Alimwoa Bibi Stephania Nambanga ambaye hakujua kusoma wala kuandika. Walijaliwa watoto wanne Benjamin akiwa wa mwisho. Kama ilivyo kwa kabila la Makua, Benjamin alipewa jina la ujombani, Mkapa. Mama hakuwa na muda wa kujifunza kusoma na kuandika kwani yeye ndiye alikuwa msingi wa familia, akihakikisha analima, kulisha familia, na kuwalea watoto. Alikuwa mkali lakini msikivu na mpenda haki. Wazazi hawa ndio vinara wa sehemu hii ya kwanza ya simulizi hii. Waliishi pamoja kwa uadilifu na heshima kubwa, na mapenzi ya pamoja kwa watoto wao.
Ingawa wazazi hawakwenda shule, walipenda sana watoto wao wote waende shule. Hii pamoja na kwamba Baba Matwani alikuwa na kipato kidogo lakini cha uhakika kila mwezi, kiliifanya familia ionekane iko tofauti. Hii ilipelekea wivu na hatimaye chuki kutoka kwa jamii. Wivu huu na chuki ulisababisha tukio moja baya sana ambalo Mheshimiwa Mkapa analikumbuka kwa uchungu. Mwaka 1947, kulitokea ukame mkali, basi watu wakamleta mganga wa kienyeji akaamua kuwa mama mzazi, mama yake na bibi yake ndio walikuwa wameloga na kuzuia mvua. Walipigwa na kuteswa sana hadi Padri Mzungu alipofanikiwa kuwanasua. Bibi wa mama aliaga dunia muda mfupi baada ya tukio hilo.
Kijana Benjamini na mwenzie mmoja ndiyo waliopata bahati ya kuendelea na masomo ya Sekondari, kutoka darasa la watoto 25 hadi 30. Kuchaguliwa ilikuwa bahati nasibu.
Shule ya sekondari ya Ndanda ilikuwa kilometa 60 kutoka Lupaso. Yeye na wenzie walitembea kwa miguu, bila viatu, kwa siku mbili, wakiwa wamebeba kichwani vitu vyao ambavyo vilikuwa vimefungwa katika mkeka. Baadae alipata sanduku la chuma.
Walimu wa Ndanda walikuwa wamisionari na walikazia sana sala na kazi “Ora et labora’’. Wanafunzi walipika chakula chao wenyewe. Kwa kuwa kijana Benjamini alikuwa mdogo sana alipewa kazi ya kuosha vyombo. Kawaida alivibeba vyombo kichwani mpaka mahali pa kuvioshea, na kuvirudisha. Anasema kubeba vyombo hivyo ndiyo sababu ana upara hadi leo
Mwaka 1952, akiwa na umri wa miaka 15, aliamua kwenda Seminari darasa la nane. Baada ya muda mfupi aliamua kuwa upadre haukuwa wito wake, akarudi Ndanda kuendelea na shule. Mwaka 1957, alichaguliwa kwenda St. Francis College Pugu ikiwa ni shule kuu ya Wakatoliki Tanganyika. Akiwa Pugu, kijana Benjamini alianza kupata mwamko wa kisiasa. Aliunga mkono harakati za kupata uhuru kwa kuandika barua kwa Mhariri wa Gazeti la “Tanganyika Standard” ambalo sasa ni Daily News akiunga mkono hoja ya Uhuru. Barua ilichapishwa. Ila kijana Benjamini alitumia jina bandia!
Mhe. Mkapa alishinda mitihani yake ya kujiunga Chuo Kikuu Makerere, kwa kupata daraja la kwanza, akiwa kati ya wanafunzi watatu bora katika darasa la wanafunzi 51.
Makerere alikumbana na mambo mengi mapya: Alikuwa darasani na wanafunzi wa rangi tofauti, kwa mara ya kwanza alikwenda kucheza dansi ya kisasa, alipangiwa chumba cha kulala nk.
Mwamko wake wa kisiasa uliendelea. Alijiunga na Bodi ya Wahariri ya gazeti la “Transition”; alikuwa mwanachama hai wa kikundi cha wanafunzi cha TANU, akiwa katibu na hatimaye mwenyekiti wake. Alishiriki kwenye siasa za wanafunzi hapo chuoni. Aligombea Urais na ingawa hakushinda, wanafunzi wa kike walimpigia kura nyingi si kwa sababu alikuwa na rafiki wa kike, ila kwa jinsi alivyoweza kujieleza kuliko mpinzani wake. Alikuwa ‘More articulate!’ Aliteuliwa Makamu wa Rais wa Serikali ya wanafunzi, na hatimaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la wawakilishi la wanafunzi hapo Makerere. Alihitimu masomo yake Aprili 1962, miezi minne baada ya Tanganyika kupata Uhuru. Alipata shahada ya lugha na fasihi ya kiingereza na fonetiki. Alikuwa tayari kuifukuzia nia na ndoto yake.
3. MAISHA NA KAZI
Simulizi ya maisha ya utu uzima iko katika sehemu mbili. Kwanza ni alipoanza kazi mpaka alipogombea Urais. Pili ni maisha ya Urais. Sehemu hii ya simulizi imejaa sifa heshima na upendo mwingi kwa Mwalimu. Anastaajabu kwa jinsi Mwalimu alivyoiunganisha nchi katika kupigania vita vya ukombozi wa bara la Africa. Kama wazazi wake mzee Matwani na Bibi Nambanga walikuwa mashujaa wa sehemu ya kwanza ya maisha yake, hakika Mwalimu ndiye shujaa katika sehemu hii ya pili. Anamueleza Mwalimu kama labda alitumwa na Mungu kwa makusudi (Almost divine intervention).
Akiwa mtu mzima na mhitimu wa Chuo Kikuu Makerere Mheshimiwa Mkapa alipenda kuajiliwa kwenye Wizara ya mambo ya nchi za nje: Kwanza ilishindikana lakini, baadae akaambiwa, itawezekana kama ataajiriwa kwanza kama bwana shauri mkufunzi wa Wilaya, wakati akisubiri. Kwa hiyo aliajiriwa hivyo huko Dodoma April 1962.
Baada ya miezi minne August 1962 aliitwa Dar es salaam aende kujifunza udiplomasia Columbia Marekani.
Baada ya mwaka mmoja alirudi nchini akaajiriwa wizarani. Kazi yake kubwa ilikuwa kuchukua muhtasari wa mazungumzo Waziri wake au Mhe. Rais alipopata wageni. Anamsifia kwa ujasiri pale alipovunja uhusiano na Uingereza. Wakati huu Mhe. Mkapa alitumia muda wake binafsi ama kusoma habari Radio Tanzania Dar es salam, ama kumchumbia Bi Anna.
Siku moja aliambiwa anaitwa Msasani kwa Mwalimu. Walipaita Msasani nyumbani kwa Mwalimu “The Clinic”. Mwalimu akamwambia anamteua kuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la The Nationalist. Ilibidi aende Uingereza kujifunza mambo ya magazeti kwenye magazeti ya The Mirror.
Alirudi na kuanza kazi chini ya Mwalimu kama Mhariri Mkuu, Mhe. Mkapa alikuwepo Arusha wakati wa Azimio mwenzie Nsa Kaisi ndiye aliyebuni neno la Arusha Declaration, walilitumia kwenye The Nationalist, Mwalimu akalipenda, basi hayo maamuzi yakaitwa hivyo.
Mhe. Mkapa aliruhusiwa kuhudhuria mikutano ya kamati kuu ya TANU, ambayo wakati ule ilitawaliwa na malumbano ya hoja na uchambuzi yakinifu ambao umepotea. Alihusika katika kutayarisha sera mbalimbali za chama kutokana na umahiri wake wa kumudu lugha.
Mwalimu na msaidizi wake Joan Wicken ndio walio mfundisha ujamaa na alivutiwa na msimamo wa usawa na umuhimu wa kujitegemea. Aliunga mkono wazo la Jeshi la Kujenga Taifa na akamuomba Mwalimu akamkubalia ajiunge kwa hiari. Alijiunga na kuhitimu. Siku ya kuhitimu Mwalimu alikuwa ndie mgeni rasmi. Mheshimiwa Mkapa alichaguliwa na wenzie kusoma risala na Mwalimu alicheka sana alivyomtambua kuwa ni yeye kwani alikuwa amepoteza ratili nyingi za uzito. Alikuwa slim fit. Mheshimiwa Mkapa aliitwa huko “The Clinic” Msasani mara kadhaa.
April 1972 Mwalimu alimteua kuwa Mhariri Mtendaji wa Daily NewsMuda mfupi baadaye Mwalimu alimteua kuwa Press Secretary wa Rais. Anasema huu ndio ulikuwa mwanzo wa maisha yake kama mwanasiasa.Mwaka huohuo, Mwalimu alimuagiza aanzishe Shirika la Habari Tanzania – SHIHATA na kuwa Mtendaji Mkuu wake.Mwaka 1976 akamteua Balozi huko NigeriaMwaka mmoja baadaye akaitwa tena “ The Clinic” na kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje. Hapa alikuwa kama msaidizi wa Rais kwani Mwalimu ndiye aliyeendesha mambo ya Nchi za Nje. Alifanywa pia Mbunge wa kuteuliwa .Aliteuliwa kuwa Balozi wa Canada 1982Balozi Marekani 1983 – 1984Akateuliwa waziri wa habari na utamaduni 1980 – 1982Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje tena 1984. Anabaini kuwa kwa kweli Mwalimu aliipa familia mtihani mkubwa na hii hamahama, lakini familia chini ya mama Anna walikubali na kupokea yote kwa mikono miwili
Hakika Mwalimu ndiye shujaa mkuu wa simulizi hii. Mheshimiwa Mkapa anamueleza Mwalimu kuwa:
Alikuwa jasiri, na kiongozi lazima awe jasiriAlikuwa msikivu, kamwe hakumkatiza mtu hata kama alikuwa anaeleza pumba tu.Alikuwa mtu wa msimamo, hakuyumbayumbaAlikuwa mpatanishi na mjenga madaraja kuwaunganisha mahasimu.Alikuwa communicater wa ajabuAlikuwa fundi wa kutafuta sehemu za makubaliano kati ya wanao tofautianaAlikuwa mtaalamu wa kutumia mawazo ya wengine kurutubisha na kuboresha ya kwakeAliupa umuhimu wa kipekee Umoja wa KitaifaHakupenda ukandamizaji ndio sababu hakupenda kuikalia Uganda baada ya vita 1980
Mheshimiwa Mkapa anasema “Mwalimu alikuwa mwalimu wangu kwa kila kitu”.
Alikuwa mwana demokrasia mtu aliyempenda kama mrithi wake mwaka 1985 alipokataliwa na wenzie katika kamati Kuu, Mwalimu alikubali.Alikuwa kiongozi mwenye maono – visionary, alingalia maslahi na mustakabali wa Taifa ndani na nje ya mipaka yake.
Wazazi wa Mheshimiwa Mkapa walifariki akiwa Waziri, wakiwa na furaha na faraja kwa mafanikio yake, ingawa hakuwa Padre, Daktari au Mwalimu kama baba yake mzazi mzee Matwani alivyotaka.
URAIS
Baada ya kutafakari na kushauriana na rafiki zake, Mheshimiwa Mkapa kwanza alimwambia mama Anna juu ya kugombea Urais. Mama Anna alisita kidogo ila akakubali. Pili alimueleza Mwalimu kwa barua kwani alikuwa Butiama, kisha akukutana nae ana kwa ana. Alimpa mwalimu sababu kuu nne za uamuzi wake wa kutaka kugombea.
Kwanza alitaka kurekebisha na kurejesha uhusiano chanya kati ya chama na serikali yake, na vyama vya ushirika ambao ulikuwa umefifia. Pili, alitaka kuhimarisha uhusiano na vyama vya wafanyakazi ambao walikuwa wanatishia kugoma kwa mara ya kwanza. Tatu, ilikuwa kurekebisha mahusiano mabaya na wahisani kuhusiana na kushamiri kwa rushwa. Nne, alitaka kurudisha uhusiano na mashirika ya fedha ya kimataifa ambao walikuwa wamekataa kuanzisha miradi mipya.Mwisho aliwapima hao waliokuwa wamechukua fomu akaona atajilaumu hapo baadae kama naye hata gombea.
Mwalimu alimshukuru, akamwambia hakuwaza kuwa nae angegombea, alikuwa anamfikiria mtu mwingine ambaye alikuwa anasita sita. Akamwambia hatamzuia kama amefanya uamuzi huo. Mwalimu aliwaomba watu kadhaa kumuunga mkono, Mwalimu alipenda hasa uwezo wake wa kufanya maamuzi, Mwalimu alishiriki katika kampeni ambapo Mheshimiwa Mkapa alisisitiza ilani, sio mambo binafsi. Mdahalo wa wagombea wote ambao ulirushwa mubashara ndio ulimfundisha njia ya ushindi. Ulikuwa “Game Changer” anasema.
November 23, 1995 aliapishwa kuwa Rais. Katika kuunda Baraza la Mawaziri, Mwalimu alikataa kujihusisha hakuwa muingiliaji – interventionist. Mheshimiwa hakuwa mgombea wa mtu kwa hivyo hakuna aliyetegemea fadhila.
Hali ya nchi ya uchumi ilikuwa mbaya sana lakini anasema sikuogopa, kiongozi lazima awe jasiri. Alikumbana na uzembe, kutowajibika na rushwa.
Kazi kubwa - kwanza ilikuwa kuwashawishi wahisani kuwa mambo yatabadilika. Nchi ilikuwa na madeni makubwa sana. Deni letu lilikuwa dola bilioni saba, tulisamehewa bilioni tatu, hii ilikuwa hatua kubwa sana na ilimfurahisha Mwalimu ambaye alishaanza kuumwa.
Mheshimiwa aliamini tulihitaji kujiangalia upya na kujifikiria kimkakati upya namna tulivyo kuwa tunaendesha nchi.
Mheshimiwa anasema kuwa walio iona staili yake ya “Kusema na kuelekeza” kuwa ilijaa kiburi na majivuno ilikuwa lazima kuonyesha kuwa hata tetereka.
Matokeo yake ni kwamba mapato yaliongezeka karibu mara tatu kutoka dola 612,587 mwaka 1995 kufikia dola 1,796,862 miaka kumi baadae. Fedha za kigeni ziliongezeka kutoka uwezo wa kununua bidhaa za mwezi mmoja na nusu kufikia uwezo wa kununua bidhaa za miezi mitano na theluthi moja. Riba za benki ilishuka kutoka asilimia 36% kufikia asilimia 15% mwaka 2005.
Ilianzishwa TRA kuimarisha ukusanyaji wa mapato Julai 1996.Ukaanzishwa mfumo wa VAT Julai 1998Public Service and Act pamoja na Public Procurement Regulatory Authority vilianzishwa 2001Commision for Human Rights and Good Governance ilianzishwa Julai 2001Prevention of Corruption Bureau nayo ilianzishwa, Mheshimiwa akaitwa Mr cleanRegulatory Agencies nyingine zilianzishwa nyingi ikiwa ni pamoja na Brela, EWURA, TCCRA,SUMATRA, Viwanja vya ndege,Maji safi na taka, TANROADS,na National Business Council kuhimarisha mahusiano na wafanya biashara.
Kati ya mageuzi tuliyofanya yaliyokuwa na utata sana ni kubinafsisha mashirika ya Umma, mageuzi/maboresho ya utumishi, na uuzaji wa nyumba za Serikali.
Kwa kweli mashirika ya Umma yalikuwa yanaendeshwa kwa hasara. Kuna wanaodai kuwa Mwalimu hakkupenda ubinafsishwaji na alisema hivyo hasa wakati wa mtangulizi wake. Mheshimiwa Mkapa anabaini kuwa, lakini Mwalimu hakunisema ana sijui kwa nini, ukweli ni kwamba Mwalimu alikuwa pragmatist na aliona hali halisi. Kwa bahati mbaya sikufuatilia utendaji wa mashirika Mheshimiwa Mkapa anaendelea mashirika tuliyo yaabinafsisha kama ambaavyo nilivyofanya kwa Regulatory Agencies. Pia kweli kuwa tulibinafsisha kwa watu wan je kuliko wazawa.
Pamoja na ugumu na utata wa baadhi ya mageuzi kura zake katika uchaguzi wa mwaka 2000 ziliongezeka kwa asilimia 100%. Hii kwake ilikuwa kuambiwa “Songa mbele, endelea” Na niliendelea, anasema.
Mheshimiwa Mkapa anasimulia kuwa maono yake: ni maisha ya hali ya juu, amani, utulivu na umoja, utawala bora,jamii iliyoelimika na uchumi shindani wenye uwezo wa kukua kiendelevu na mgawanyo shirikishi wa kipato. Ili kuyapata hayo ikaanzishwa
Vision 2025, MKUKUTA, MKURABITA, Mini Tiger Plan 2020, TASAF. Wengi katika Baraza la Mawaziri, kwenye Chama na Serikali hawakuviunga mkono. Lakini sasa naiona TASAF kama “High Point” ya Urais wangu, anasema Mheshimiwa Mkapa.Bima ya TaifaMageuzi katika Elimu, DEDP na SEDPMradi wa maji ziwa Victoria,
Kuhusu mahusiano ya ndani na nje, Mheshimiwa Mkapa anabaini kuwa uhusiano katika ya Bara na Zanzibar ulikuwa mgumu na tete lakini alifanikwa kutatua matatizo.
Anasema alikuwa na wasiwasi pale Rais wa Zanzibar Salmin Amour alipotaka kubadilisha sheria na kutawala kipindi cha tatu. Lakini baadae yeye na wafuasi wake wakaamua yaishe.
Zanzibar ilianza kupeperusha bendera yake.
Vifo vya watu 22 huko Pemba Januari 2001 vilinishtua na kumhuzunisha sana. Anasema “hili litaendelea kuwa doa katika Urais wangu ingawa sikuwepo lilipotokea”.
Anabaini kuwa wakati wa utawala wake, wanadiplomasia walionyesha upendeleo kwa vyama vya upinzani na kukutana nao mara kwa mara, Pia wapo walioamini walistahili upendeleo kuliko wengine.
Kwa upande wa vyombo vya habari ilibidi azoee kukosolewa, kwani waliamini alikuwa dictator ingawa alikuwa anashikilia msimamo. Anabaini kuwa alihitaji kuuza sera zake, kwa hiyo akaanzisha utaratibu wa kulihutubia Taifa kila mwezi lakini mhimili mkuu wa kupokea na kutoa mawazo na habari ilikuwa Chama chake CCM na vikao vyake mbalimbali.
Mheshimiwa Mkapa anakiri kuwa, Kabla hajawa Rais, hakujua kuwa kazi moja wapo ya Rais ni kutoa pole. Moja wapo ya mapungufu yangu ni kwamba si mwepesi wa kuonyesha hisia zangu. Mrithi wangu Rais kikwete ni mzuri sana katika hili. “Anasema Mheshimiwa Mkapa.
Mwaka 1996 mafuriko yalisababisha maafa makubwa katika Nchi.Kuzama kwa Mv bukoba kulistua na kuhuwisha sana majanga mengine mengi.Niliwahurumia wafungwa wote waliostahili kunyongwa mpaka kufa.
Anasema ingawa hakatai kukosolewa kisiasa au kisera, kukosolewa binafsi kuliumiza sana. Kwa mfano madai kwamba alimpendelea Baba mkwe wa mwanae katika kubinafsisha mgodi wa makaa ya mawe wa kiwira yalimuumiza sana.
Pia madai kuwa aliwapendelea NET GROUP solutions ltd wakati wa kubinafisha TANESCO kwa sababu ya shemeji yake kulimuumiza sana pia jambo moja lilojitokeza baada ya muheshimiwa kumaliza muda wake ni la External payment account (EPA). Mheshimiwa anaeleza kuwa, anavyoelewa urais wake haukuwa wa kwanza kuruhusu ununuzi wa madeni kama huo. Anasema kwanza alisita ila Gavana wa Benki Kuu Daud Bilali alimuelewesha na akasema watakao nunua hayo madeni walikuwa tayari kuchangia mfuko wa kampeni za uchaguzi wa CCM. Wahuni walitumia uaminifu wake kwa chama kumshawishi akubali. “Ninajisikia kuwa nilitumika na kusalitiwa. Na ukweli ni kwamba mimi binafsi sikufaidika na sikupata chochote”. Anasema Mheshimiwa Mkapa.
Kuna kukosolewa kuhusu matumizi ya anwani ya Ikulu wakati mimi na mke wangu tulipochukua mkopo NBC kununua nyumba. Ukweli ni kwamba wakati ule tulikuwa tunaishi Ikulu, tulichukua mkopo kwa mashart ya kawaida ya biashara. Kabla sijaondoka Ikulu, nilimaliza malipo ya mkopo huo na mshahara wangu wa mwisho na mafao yangu, tukapewa hati ya nyumba hiyo. Anasema Mheshimiwa Mkapa.
Kulikuwa pia na swala la RADAR ambayo ilkuwa lazima kuinunua kuimarisha ulinzi lakini manunuzi yaligubikwa na udanganyifu na hatimaye hela zilizolipwa za ziada zilirudishwa kwa Serikali.
Anafikiri ni muhimu kutazama upya suala la umiliki wa uchumi ili watu wengi zaidi wahusike. Kuendelea kushamiri kwa umiliki hasa wa viwanda na mashamba makubwa na makampuni ya Kiasia au Kihindi inaweza ikaleta wivu, na kuleta shida kubwa. Ana wasiwasi na siku za mbeleni kwani umaskini uenda bega kwa bega na uvunjifu wa amani. Lazima tujiulize kama tunajikita katika utulivu na amani.
Anamalizia kwa kutoa ushauri kwa viongozi wa wakati ujao (future).
Onyesha nia na bidii kwa majukumu upewayo.Uwe tayari kuwashirikisha wengine katika mawazo, mafanikio, matatizo na upimaji utekelezaji, consult more.Usifanye kazi kwa kukurupuka na kutotabirikaFuata na tii sheria na taratibuUwe tayari kusikilizaMtafute mlezi (mentor) kama mimi nilivyokuwa na Mwalimu.
Katika sehemu anabainisha umuhimu wa mke wake mama Anna Mkapa. Mapema kabisa katika ukurasa wa 83. Mheshimiwa anampa saluti mama Anna kwamba yeye ndiye gundi iliyo shikilia familia. Anakiri kuwa yeye Mheshimiwa Siyo mtu rahisi kuishi naye na anamshukuru kwa kuwa mtu wa subira na uwezo mkubwa. Amevumilia mengi wakati wa safari za mara kwa mara, kutokuwepo nyumbani mara nyingi na ndiye alibeba mzigo wa kuwalea watoto wao wawili.
4. KUSTAAFU
Sehemu ya tatu naya mwisho ya simulizi hii, ni maisha ya mheshimiwa baada ya kustaafu Urais.
Kwanza Mheshimiwa ametumika sana Kimataifa katika nyadhifa na Taasisi mbalimbali ingawa hapendi kusafiri, Taasisi hizo ni pamoja na
Club de Madrid, The African Wildlife Foundation, Investment Climate Facility for Africa, UN Iniative “Delivering as One”UNCTAD, Panel of Environment Persons, UN Commission on the Legal Empowerment of the Poor, Mwenyekiti wa Seventh Centre tangu 2006, Trustee wa the Aghakhan University na The Mkapa Foundation
Kote huku amejichanganya na watu wenye akili nyingi.
Pili, amehusika sana katika upatanisho wa migogoro huko South Sudan, Congo Mashariki, na Kenya.
Mheshimiwa Mkapa, anamalizia simulizi hii kwa kugusia mambo kadhaa.
Kwanza, anaona Rais mstaafu anathaminiwa zaidi uongozi na uwezo wake Kimataifa zaidi kuliko nyumbani, jambo ambalo hata Mwalimu aliliona. Mara nyingi huitwa kwenye hafla ambapo anakuwa kama Ua au pambo ukutani, lakini natakiwa kwenye kazi muhimu na nyeti za kitaifa.Pili, anaongelea umuhimu wa kuanzishwa kwa Baraza dogo kama sehemu ya Bunge kupitia miswada iliyopitishwa na Bunge kabla ya utekelezaji.Tatu, anazungumzia kukosekana kwa itikadi na fikra pevu za kina juu ya mustakabali wa Taifa letu. Inabainishwa kuwa tunahitaji ukombozi wa pili, Kisiasa, Kiuchumi, Kiutamaduni. Tunahitaji kama Taifa, na mtu mmoja mmoja kuona aibu kuwa ombaomba. Tunahitaji kujitegemea na kuthamini uendelevu (sustainability) wa maendeleo.Nne, anagusia mwendo wa goigoi katika kuimarisha Jumuia ya Afrika Mashariki (EA). Sioni juhudi kubwa, naona siasa tu, watu wamepoteza picha kubwa – Big Picture. Tano, anagusia Uongozi. Anabainisha kuwa uongozi bora ni kipaji au karama na sayansi pia. Unazaliwa na karama hizo lakini unajifunza pia. Nia yaani commitment ni muhimu. Kiongozi bora ni lazima awe mfano wa kuigwa katika utendaji kazi wake, uaminifu na uadilifu.
Anatilia mkazo swala la ongezeko la vijana na kwamba hakuna sera, ya namna ya kushughulikia ongezeko kubwa la watu. Anagusia pia suala la siasa halaiki yaani Populism na athali zake.
Kuhusu siasa na demokrasia, anabainisha kuwa CCM bado kinajiona kama bado kipo kwenye siasa za chama kimoja, Kunahitajika more political interaction na engagement.
Mheshimiwa anaendelea kuwa, uwepo wa vyama vingi vya siasa unadhoofisha demokrasia. Watu wanaingia katika siasa kusaka manufaa ya kiuchumi sio kwa nia tukufu ya kuwatumikia watu na taifa. Wafanya biashara wanasaka na kulinda maslahi, wasomi hutafuta kusafiri na posho, Wabunge wachache wanajali maslahi ya jimbo, wengi wanapenda safari za nje. Hakuna interaction ya Wabunge kuhusu sera na utekelezaji wake.
Mwisho Mheshimiwa anajiuliza kama tutaweza kudumisha amani na umoja wetu kama Taifa. Anagusia kuibuka hapa na pale viashiria vya ukabila, udini, na ukanda.
Mwisho kabisa Mheshimiwa Mkapa, anamalizia kwa kusema; Nitamuachia Mungu wangu na nyinyi kuamua ni tofauti gani nimeifanya humu duniani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇