Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene ameagiza waliobainika kusafirisha vyuma chakavu ambavyo ni miundombinu ya majitaka na maji safi wachunguzwe kujua walikovitoa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Pia ametahadharisha kuwa yeyote atakayekutwa amebeba, kuhifadhi, kuuza au kusafirisha vyuma chakavu bila kibali, atakuwa ametenda kosa la kisheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Simbachawene ametoa agizo hilo jana ofisini kwake jijini Dodoma ambapo ameagiza Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuichukulia hatua Kampuni ya Press Freight Tanzania Ltd (Wakala wa usafirishaji) kwa kusafirisha makontena ya chuma chakavu mali ya kampuni ya Eco Steel ambayo hayakuwa na kibali na ilisafirisha makontena hayo baada ya katazo alilotoa na kusisitiza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Alisema kuwa katika makampuni nane yaliyokuwa yanamiliki makontena 147 yaliyokuwa Dar es Salaam yalipokaguliwa, makampuni manne 177 yalisema uongo kwani yaliweka vitu visivyoruhusiwa kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya kusafirishwa nje na havijulikani wamevitoa wapi.
“Kwa kampuni ya Eco steel Limited na Mahavir Implex Tanzania Limited ambazo zilikiuka agizo langu la kusafirisha taka hatarishi nje ya nchi, naagiza taasisi zilizowapa leseni yaani Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira wazifutie leseni kwani wamekiuka sheria ya mazingira ya vibali vya kukusanya na kusafirisha taka hatarishi ndani ya nchi, vile vile kwa mamlaka niliyonayo sitatoa leseni kwa kampuni hizo kwa ajili ya kufanya biashara hiyo hata kile kinachoruhusiwa,” alisisitiza.
Hata hivyo alizitaka kampuni nne zilizodanganya ambazo zilikuwa na mapungufu madogo kwenda NEMC kwa ajili ya kufuata utaratibu kwa kulipa faini na kuanza upya mchakato wa kupata kibali cha Waziri cha kusafirisha nje ya nchi taka hatarishi.
Pia ameagiza kampuni manne yaliyokutwa na makosa kulipa faini ya sh. 460,000 kwa kila kontena lililokaguliwa na wataalamu pia mengine yenye makossa kulipa faini iliyopangwa kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004.
Aidha Waziri huyo alisisitiza kuwa biashara zote za ukusanyaji wa vyuma chakavu kwa mtu mmoja mmoja kwa ngazi za chini zitasimamiwa na Serikali za Mitaa huku akiagiza utekelezaji huo kuanza mara moja.
Itakumbukwa jumla ya makontena 142 yanayomilikiwa na makampuni tofauti yalifanyiwa ukaguzi na taarifa kuwasilishwa na Timu ya kitaifa ya ukaguzi Oktoba 16, 2019 na kuwa taarifa ilionesha uwepo wa ukiukwaji wa sheria na kanuni zinazosimamia na kudhibiti taka zenye madhara nchini na mkataba wa kimataifa wa Basel unaoruhusu udhibiti wa usafirishaji wa taka zenye madhara na taka nyingine baina ya nchi na nchi ambazo Tanzania ni mwanachama.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇