Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon, Bw. Kasara Naftal
akionyesha medali ambayo washiriki wote watakaomaliza mbio hizo
watapatiwa.
Mtendaji wa Idara ya Mawasiliano ya mbio za Rock City Marathon,
Bw. Samwel Gisayi (Wa pili kushoto) akizungumzia usajili wa washiriki wa
mbio hizo, mapema leo katika mkutano na waandishi wa Habari.
Muwakilishi wa washiriki wa mbio za Rock City Marathon, Bw. Frank
R. Mtweve akionyesha medali tofauti watakazopatiwa washindi wa mbio
hizo.
Ikiwa
zimebaki wiki mbili kabla ya kufanyika kwa mbio za Rock City Marathon
jijini Mwanza, wadau mbalimbali wanaotarajia kushiriki katika mbio hizo
wameonyesha kufurahishwa na zawadi zitakazotolewa kwa washindi na
washiriki ikiwemo medali na fedha taslimu zaidi ya Sh Mil 30.
Mbio
hizo zilizojinyakulia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi zinatarajiwa
kufanyika Octoba 20 mwaka huu kwenye Viunga vya Jengo la Biashara la
Rock City Mall huku wadau mbalimbali wakiwemo viongozi waandamizi
serikalini akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella wakitarajia
kushiriki katika mbio hizo.
Akizungumza
leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa mbio hizo kutoka kampuni ya
Capital Plus International (CPI), Bw. Kasara Naftal amesema pamoja na
medali washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume na wanawake
watajinyakulia sh. Mil 4 kila mmoja, sh.mil
2/- kwa washindi wa pili na sh. Mil 1/- kwa washindi wa tatu, huku
washindi wanne hadi kumi na tano nao pia wakiibuka na zawadi za medali
na pesa taslimu.
Kwa
upande wa mbio za Kilomita 21, Bw Kasara alisema pamoja na medali
washindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh. Mil 2/-
kila mmoja, sh. Mil 1/- kwa washindi wa pili na sh. Laki 7/- kwa
washindi wa tatu huku pia washindi wanne hadi wa kumi na tano wakiibuka
na zawadi za pesa taslimu na medali kila mmoja.
“Kuhusu
mbio za kilomita tano ambazo zitahusisha washiriki kutoka mashirika na
taasisi mbalimbali (corporates) tunatarajia kwamba zitaongozwa na Mkuu
wa Wilaya ya Nyamagana Dk Philis Nyimbi sambamba na washiriki wenye
ulemavu wa ngozi yaani albino ambapo zawadi za fedha taslimu zitatolewa
kwa washindi watatu wenye ualbino pekee.” Alisema.
Bw
Kasara aliongeza kuwa kwa washindi wa mbio za kilomita mbili na nusu
zitakazohusisha watoto wenye umri kati ya miaka 7 hadi 10 watapatiwa
fedha taslimu.
Mbio
hizo zilizoanzishwa miaka kumi iliyopita zinatarajiwa kupambwa
naburudani mbalimbali ikiwemo ngoma za asili sambamba na maonesho ya
waadau mbalimbali wakiwemo wadhamini wa mbio hizo ambao ni pamoja na
kampuni za TIPER, Pepsi, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la
Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA).
Wadhamini
wengine ni pamoja na kampuni ya uwakili ya Lis Law Chambers &
Consultants, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Taasisi ya Taifa
ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), CF Hospital, Metro FM,
Mwanza Water, Pigeon Hotel, Cask Bar, Kampuni ya Usafi ya SDN na Kampuni
ya Ulinzi ya Garda World.
Akizungumzia
usajili wa mbio hizo Bw. Samwel Gisayi kutoka idara ya mahusiano ya
mbio hizo alitoa wito kwa washiriki kuendelea kujisajili kupitia vituo
na mawakala wa mbio hizo katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma,
Pwani na Arusha
‘’Kwasasa
usajili wa mbio hizo unaendelea kupitia vituo mbalimbali katika mikoa
ya Mwanza (Rock City Mall, Pasiansi Afro Twist Gym), Dodoma (Shabiby Bus
Terminal), Dar es Salaam (Shamo Tower, Imalaseko Super Market (Posta),
Heleana Fashion – Dar Free Market), Arusha pamoja na Bagamoyo mkoani
Pwani.’’
“Pia usajili unaweza kufanyika kwa njia ya mtandao kupitia website yetu ya Rock City Marathon ambayo ni www.rockcitymarathon.co.tz’’
Naye
muwakilishi wa washiriki Bw. Frank R. Mtweve alielezea kufurahishwa
kwake na zawadi zinazotolewa na waandaaji wa Rock City Marathon.
“Rock
City Marathon ndio mbio pekee hapa nchini ambazo zinatoa zawadi kubwa
kuliko na washiriki wake wote watakaomaliza mbio kupata medali. Na pia
ndizo pekee ambazo zinashirikisha watu wenye ulemavu wa ngozi
(Albinism).” Alisema
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇