Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu Rais Mhandisi Joseph Malongo
(katikati) akizungumza wakati wa kikao na Wabunge wa Kamati ya Bunge la
Ujerumani ya Mazingira, Uhifadhi Maliasili na Usalama wa Nyuklia kilichofanyika
Ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Jijini Dodoma. Wengine pichani kushoto ni
Naibu Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi wa Mazingira Profesa
William Mwegoha.
Wabunge wa Kamati ya Bunge la Ujerumani ya Mazingira,
Uhifadhi Maliasili na Usalama wa Nyuklia ukiwa katika kikao na Ofisi ya Makamu
wa Rais kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Jijini Dodoma.
Kiongozi wa Ujumbe
huo Mhe. Sylvia Kotting-Uhl (katikati) akizungumza walipokutana na
Ofisi ya Makamu wa Rais Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu Rais Mhandisi Joseph Malongo akiwa na Kiongozi wa Wabunge wa Ujerumani Mhe. Sylvia Kotting-Uhl mara baada ya kumalizika kwa kikao
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu Rais Mhandisi Joseph Malongo
akibadilishana mawazo na wabunge wa Kamati ya Bunge la Ujerumani ya Mazingira,
Uhifadhi Maliasili na Usalama wa Nyuklia walipowasili katika Ofisi ya Makamu wa
Rais Jijini Dodoma.
Lulu Mussa na Robert
Hokororo
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu
wa Rais Mhandisi Joseph Malongo amesema azma ya Serikali ya ujenzi wa bwawa
kubwa la kufua umeme la Julius Nyerere iko pale pale na ujenzi wake unaendelea
kwa kasi huku suala la hifadhi ya mazingira likizingatiwa.
Akizungumza na Wabunge wa
Kamati ya Bunge ya Mazingira, Uhifadhi wa Maliasili na Usalama wa Nuklia kutoka
Ujerumani Mhandisi Malongo amesema Tathmini ya Athari kwa Mazingira imefanyika
na kuonyesha kuwa ujenzi huo ni salama kwa mazingira.
“Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza mradi huu kwa
kutumia fedha zake kutoka vyanzo vya ndani.
Mradi huu utachukua eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 1,250
ambalo ni sawa na asilimia tatu (3%) tu ya eneo lote la pori la akiba selous
lenye ukubwa wa kilomita za mraba 50,000.” Malongo
alisisitiza.
Mhandisi Malongo amesema kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 kifungu cha 81, mradi
huu umefanyiwa tathimini ya athari kwa mazingira ili kubaini matokea hasi na
chanya na kuweka mipango ya kudhibiti madhara na kuboresha utekelelezaji wake.
Amesema
kuwa kiwango cha umeme cha megawati 2,100
kitaongezeka kwenye gridi ya Taifa kwa maendeleo ya shughuli za kiuchumi na
kijamii ikiwa ni pamoja na maendeleo ya viwanda na kupunguza uzalishaji wa
gesijoto duniani, pamoja na uwepo wa fursa za kilimo cha umwagiliaji na uvuvi
ulioboreshwa katika uwanda wa chini kutokana na usimamizi na udhibiti wa
mtiririko wa maji
Katika hatua nyingine Mhandisi Malongo amewafafanulia
wabunge hao mafanikio yaliyopatikana katika katazo la matumizi ya mifuko ya
plastiki hapa nchini lililoanza kutekelezwa Juni Mosi na kusema kuwa katika
kipindi cha miezi mitatu kampeni hiyo imeonyesha mafanikio kwa kiasi kikubwa
kwani imepokelewa kwa mtazamo chanya na wanachi ikiwa ni jitihada za
kushirikisha taasisi mbalimbali na wadau kwa ujumla.
Akiongea kwa niaba ya wenzake kiongozi wa ujumbe huo Mhe.
Sylvia Kotting-Uhl ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa mageuzi makubwa
yanayofanyika katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano na kuahidi
ushirikiano na nchi yake katika kujenga uwezo katika nyanja za kusimamia na
kudhibiti taka za kielektroniki, Uzalishaji wa Umeme wa jua na kutoa mwaliko
kwa ujumbe wa Tanzania kutembelea Ujerumani kujifunza zaidi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇