MKUU
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti amewashukia vikali baadhi
ya wanasiasa Wilayani Simanjiro wanaowagawa wananchi katika makundi ya
uchaguzi wa serikali za mitaa kwa tiketi ya CCM ili wapate nafasi ya
kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa ubunge 2020.
Mkuu
huyo wa Mkoa wa Manyara Mnyeti aliyasema hayo jana katika kijiji cha
Narakauo Kata ya Loiborsiret kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku
tano wilayani Simanjiro.
"Mwisho
wa wanasiasa uchwara wa wilaya ya Simanjiro wanaotumia nafasi ya
makundi na kugawa wananchi ili wapite katikati yao na kupata ubunge
imefika mwishoni," alisema Mnyeti.
Alisema
anataka kuona Simanjiro mpya moja yenye wananchi wenye kutaka maendeleo
na siyo kugawanywa na baadhi ya wanasiasa uchwara wanaogawa wananchi
kwa maslahi yao ya kutaka kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2020.
Alisema
yeye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa ndiyo sababu wakafuta
mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa ndani ya CCM wilayani
Simanjiro na kuagiza uanze upya kwa lengo la kuondokana na ubabaishaji.
"Wananchi
wa wilaya ya Simanjiro hivi sasa wanataka maendeleo hawahitaji tena
siasa uchwara zisizo na muelekeo wenye manufaa kwao kwa kutumia nafasi
ya uchaguzi wa serikali za mitaa," alisema Mnyeti.
Mkuu
wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula aliwataka wananchi wa
eneo hilo kutowachagua viongozi wanaojihusisha na uuzaji wa ardhi ili
kuepusha migogoro ya ardhi.
Mhandisi
Chaula aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kutumia nafasi hiyo vizuri ya
uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwaondoa madalali wa kuuza ardhi na
kuondokana na migogoro ya ardhi.
"Mkitumia
makosa kwa kuchagua madalali wa ardhi baadaye msije ofisini kwangu
kunisumbua kwani mtakuwa mmewachagua wenyewe na vijana wa sasa wanasema
itakula kwenu," alisema mhandisi Chaula.
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizindua madarasa matatu
ya shule ya msingi Loong'swani kata ya Terrat Wilayani Simanjiro.
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa
Kata ya Terrat kwenye ziara yake ya siku tano wilayani Simanjiro jana.
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti (wapili kushoto) Mkuu wa
Wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula (kushoto) wakipiga makofi
baada ya kukagua nyumba ya kisasa ya mfugaji wa kijiji cha Narakauo
Isaya Mongele, kulia ni Diwani wa Kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga
Mardadi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇