Vikosi vya muqawama vya Palestina vimefanikiwa kutungua ndege isiyo na rubani ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kuwa, askari wa Kikosi cha Abu Ali Mustapha, ambalo ni tawi la kijeshi la harakati ya muqawama ya Popular Front for the Liberation of Palestine (PFLP) wametungua drone hiyo ya Wazayuni mashariki mwa mji wa Khan Yunis, katika Ukanda wa Gaza jana jioni.
Jeshi la utawala haramu wa Israel halijatoa tamko lolote kuhusiana na kutunguliwa kwa ndege yake hiyo isiyo na rubani ya ujasusi katika anga ya Gaza, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Itakumbukwa kuwa, Jumatatu iliyopita, harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas ilitungua drone nyingine ya utawala pandikizi wa Israel mashariki mwa mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, siku moja baada ya jeshi katili la Israel kuanzisha mashambulizi ya anga katika ukanda huo ambao uko chini ya mzingiro.
Aidha siku chache zilizopita, makombora ya ulinzi wa anga ya harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah yameitungua na kuiteketeza ndege isiyo na rubani ya ujasusi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye anga ya kitongoji cha al Adisah mkoani An-Nabtiyyah kusini mwa Lebanon, siku chache baada ya droni nyengine ya Israel kutunguliwa katika eneo la Ramiyah kusini mwa Lebanon.
Utawala ghasibu wa Israel umekuwa ukitumia droni katika hujuma na mapambano ya kukabiliana na harakati za muqawama wa Kiislamu huko Palestina na Lebanon.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇