KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bashiru Ally, akimkabidhi muonekano wa gazeti la Uhuru la Kijani Mwenyekiti wa Bodi ya Uhuru Media (UMG) Rodrick Mpogolo. wakati wa hafla ya uzinduzi wa Uhuru la Kijani, katika Ukumbi wa Kamati Kuu ya CCM, Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma. Picha na Halima Kambi. Picha zaidi BOFYA HAPA
Na Faustine Gimu Galafoni, Dodoma.
Gazeti la Uhuru limepiga hatua nyingine mpya katika historia yake tangu kuanzishwa mwaka 1961, kwa kuzindua toleo maalum la 'Uhuru ya Kijani' ambalo litakuwa mahsusi kuandika kwa kina habari za CCM .
Uzinduzi huo ambao ulifanyika katika Ukumbi wa Kamati Kuu ya CCM, Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma, ulihudhuriwa na mawaziri, wabunge, Spika wa Bunge Job Ndugai na Viongozi wa Uhuru Media wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) Rodrick Mpogolo na Mkurugenzi Mkuu wa Uhuru Media Ernest Sungura, ulifanywa na Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally.
Akizungumza Dk.Bashiru alisema toleo hilo maalum litatumika kujenga na kuimarisha Chama na yeye atakuwa na ukurasa wake ambao atakuwa anazungumzia kuhusu urithi na kufafanua kuwa ukurasa huo kutakuwa na mambo matano ikiwemo haki na tunu za taifa.
“Kuna mjadala kuhusu tunu za Taifa kulikuwa na mjadala hata kwenye Bunge la Katiba ambapo moja ya tunu ni lugha ya Kiswahili, na gazeti hili litatumika kukuza Kiswahili,”alisema.
Awali, Spika wa Bunge Job Ndugai, alipongeza kuanzishwa kwa toleo la gazeti hilo la 'Uhuru la Kijani' akisemai kuwa litasaidia kufikisha habari kwenye matawi kwa sababu kukosekana kwa habari kwenye matawi kumekuwa ni unyonge mkubwa.
“Gazeti lina habari za muhimu na za kuelimisha, jambo hili ni jema nakuahidi sisi wabunge tutatoa kila aina ya ushirikiano, tutachukua nakala kwa idadi ya matawi, kata, na wilaya na limekuja wakati muafaka maana tunaelekea kwenye uchaguzi,”alisema.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇