Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma. Julius Mtatiro, ametatua mgogoro wa muda mrefu kati ya jeshi la polisi na bodaboda wa wilaya hiyo.
Mgogoro huo uliibuka juzi Ijumaa na kupelekea polisi wakabiliane na vijana wa bodaboda na kuwapiga mabomu ya machozi na kuwakamata.
Mtatiro aliahirisha ziara ya kikazi wilayani Songea na kurejea Tunduru moja kwa moja, akaitisha kikao cha dharura katika kituo cha polisi na viongozi wa bodaboda na kuamuru bodaboda zote zilizoshikiliwa na vijana wote walioshikiliwa, waachiwe mara moja, jambo ambalo lilitekelezwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya siku hiyo hiyo ya Ijumaa.
Jana Jumamosi. Mtatiro aliitisha kikao kikubwa zaidi kikiwahusisha bodaboda wote wa Tunduru ili kusikiliza na kutatua kero zao. Katika majumuisho kikao hicho kilikubaliana polisi waache kuwapiga vijana wa bodaboda katika oparesheni za kipolisi, DC Mtatiro amepiga marufuku tabia ya polisi kukimbizana na bodaboda wachache watovu wa nidhamu na badala yake amewataka polisi wachukue namba za pikipiki husika na kisha kumuita mmiliki na dereva na kuwachukulia hatua za kisheria kwa sababu kufukuzana kumekuwa kukileta ajali mbaya.
DC Mtatiro amewaonya vijana wa bodaboda na kuwataka wafuate sheria, wakisimamishwa na polisi wasimame na kutoa ushirikiano na amewataka polisi wasitumie nguvu bila sababu, akiwapa mfano wa tukio la Ijumaa la Mabomu na kulielezea kama halikuwa na uzito wa kupiga mabomu na kuwaumiza vijana.
DC Mtatiro amewakumbusha polisi kuwa, Dkt. Magufuli, Rais wa Tanzania hataki kuona vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa, wananyanyaswa na kupigwa maana ni vijana hao ndiyo watakaoipigia kura CCM na kuirejesha madarakani na kwamba kuwanyanyasa kunaenda kinyume na malengo ya CCM ya kuwalinda vijana.
Katika mkutano huo, DC Mtatiro alifanya mazungumzo ya moja kwa moja kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Kangi Lugola (MB) kumuomba ufafanuzi juu ya maelekezo yake ya makosa ambayo polisi hawapaswi kuyatumia kuwakamata madereva wa bodaboda na bodaboda zao.
Mhe. Waziri Kangi Lugola alifafanua kuwa yeye hajasema bodaboda wasio na helmet, waliobebana "mishikaki" na wanaotenda makosa mengine wasiadhibiwe na kwamba alichosema ni kutaka polisi wawatoze faini (ya kulipa ndani ya siku 7) au kuwaonya bodaboda wote wanaokutwa na makosa ya helmet, kukosa leseni au mishikaki na kuwa polisi wasiwakamate madereva hao, abiria wao au bodaboda zao ikiwa wamewakuta na makosa hayo.
Katika simu hiyo ambayo ilikuwa inasikilizwa na wananchi wote kupitia vipaza sauti, Waziri Kangi aliwataka wananchi wa Tunduru kumtumia sana Mtatiro kutatua kero zao na kujiletea maendeleo haraka kwa sababu ya misimamo ya DC Mtatiro, weledi wake, uthubutu na kiu yake ya kuwasaidia wanyonge.
DC Mtatiro ameagiza sheria za barabarani zifuatwe lakini vijana wa Tunduru wasinyanyaswe na kuumizwa kwa sababu yoyote ile, jambo ambalo limekubaliwa na pande zote - polisi na madereva bodaboda.
Kikao cha DC Tunduru, Polisi na madereva wa bodaboda kimemalizika kwa amani sana na pande zote zikashikana mikono na kufurahi pamoja huku vijana wa Tunduru wakimpongeza sana DC huyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇