LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 18, 2019

KUONGEZEKA MATATIZO YA KIUCHUMI; KUANZA MAANDAMANO NCHINI ZIMBABWE

Mandamano hayo yamekabiliwa na ukandamizaji wa polisi na wanajeshi wa nchi hiyo ambapo makumi ya watu wamejeruhiwa na wengine wengi kutiwa nguvuni. Washiriki wa maandamano hayo ambayo yaliitishwa na chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change MDC, walilaani ubadhirifu wa mali ya umma na uongozi mbaya wa kisiasa na kiuchumi unaoonyeshwa na Rais
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe
. Mandamano hayo tayari yalikuwa yamepigwa marufuku na serikali.
Kabla ya kufanyika maandamano, Paul Nyathi, Msemaji wa Polisi ya Zimbabwe alisema: Kutokana na kuwa maandamano ya wapinzani wa serikali yatasababisha machafuko, wale wote watakaoshiriki maandamano hayo watakuwa wamekiuka nidhamu ya umma na kuchukuliwa kuwa wahalifu. Hivyo watakabiliwa kwa mujibu wa taratibu za kiusalama na sheria.
Hali ya uchumi wa Zimbabwe ni mbaya mno. Siasa za uchumi zilizotekelezwa na rais aliyeng'olewa madarakani Robert Mugabe, zimeongeza sana ughali wa maisha, ukosefu wa ajira na umasikini nchini humo. Hii ni katika hali ambayo baada ya kupinduliwa Mugabe mwaka 2017 na kuingia madarakani Mnangagwa, wananchi wengi wa nchi hiyo walitarajia kwamba hali yao ya kiuchumi ingeboreka. Mara tu baada ya kuingia madarakani, Mnangagwa aliahidi kuandaa nafasi za ajira, kufanya marekebisho ya kiuchumi, kuimarisha uhusiano na nchi za kigeni, kuvutia uwekezaji na kuboresha miundombinu ili kuimarisha uchumi wa Zimbabwe. Lakini baada ya kupita zaidi ya mwaka mmoja sasa si tu kwamba siasa zake hazijasaidia lolote katika kuboresha uchumi huo bali zimeuharibu zaidi.
Kuhusu hilo, David Beasley, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP anasema: Wazimbabwe wapatao milioni 5 ambao ni karibu thuluthi moja ya jamii yote ya watu milioni 16 wa nchi hiyo wanahitajia msaada wa dharura wa chakula na karibu nusu ya watu wa nchi hiyo wanakaribia kukumbwa na baa la njaa.
Uhaba wa mkate na umeme pamoja na kiwango cha juu cha ughali wa maisha ni mambo ambayo yamewakasirisha sana watu wa nchi hiyo. Hivyo uamuzi wa serikali kuongeza bei ya mafuta umewakasirisha hata zaidi wananchi hao na kuwasukuma mitaani kufanya maandamano dhidi ya serikali. Wakati huo huo uzembe wa serikali katika kufanya marekebisho ya kisiasa nchini pia kumewachochea wapinzani wa kisiasa na hasa wafuasi wa Movement for Democratic Change MDC kujiunga na waandamanaji mitaani.
Polisi ya Zimbabwe ikikandamiza maandamano ya hivi karibuni
Licha ya kuwepo ukandamizaji wa polisi na marufuku ya serikali dhidi ya kufanyika maandamano hayo, lakini chama hicho kinasisitiza kwamba kitaendelea kuandaa maandamano kama hayo katika wiki zijazo. Hii ni katika hali ambayo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa huko mjini Geneva Uswisi, ameitaka serikali ya Zimbabwe izungumze na wapinzani na kutoyakandamiza maandamano yanayofanyika kwa njia ya amani.
Hata kama kulikuwepo na shaka kuhusu kuimarika uchumi wa Zimbabwe tokea Mnangagwa aingie madarakani, lakini wengi nchini humo waliyatazama mabadiliko hayo ya uongozi kuwa tukio muhimu ambalo lingesaidia kuimarisha mustakbali wa nchi hiyo ambayo wakati mmoja lilikuwa koloni la Uingereza na kukabiliwa na uongozi mbaya kwa miongo kadhaa. Lakini kwa sasa wananchi wengi wa nchi hiyo wamekata tamaa kuhusiana na uwezekano wa kuboreka uchumi wao na hivyo wanataka mabadiliko mengine ya msingi ya kisiasa yafanyike ili kuimarisha mazingira ya kiuchumi na kisiasa ya nchi hiyo. Kwa kadiri kwamba katika maandamano ya hivi karibuni, baadhi ya washiriki walisikika wakipiga nara kwa maslahi ya chama cha upinzani kilichoshindwa katika uchaguzi na kusikitishwa na hali mbaya ya uchumi wa nchi. Kwa maelezo hayo wiki zinazokuja zitakuwa wiki muhimu sana kwa mustakbali wa nchi hiyo ambayo wakati mmoja ilikuwa ikiitwa 'kapu la chakula' la bara la Afrika.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages