Wawakilishi wa Iran, Harakati ya Ansarullah ya Yemen na nchi nne muhimu za Ulaya wamekutana na kusisitiza kuhusu umuhimu wa kumaliza vita haribifu vinavyoendelea dhidi ya Yemen.
Ujumbe wa Iran ukiongozwa na msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya maalumu ya kisiasa Ali Asghar Khaji, wawakilishi wa Ansarullah wakiongoziwa na msemaji wa harakati hiyo Mohammad Abdul-Salam pamoja na mabalozi wa nchi za Ulaya za kundi la EU/EU4 yaani Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia, wamefanya mkutano wa pande tatu hapa Tehran kujadili matukio ya hivi karibuni nchini Yemen.
Katika kikao hicho, washiriki wamewasilisha mitazamo ya nchi zao kuhusu hali nchini Yemen na hasa kuhusu masuala ya kisiasa na kibinadamu. Pande zote tatu katika kikao hicho cha Jumamosi zimebainisha masikitiko yao kutokana na hali mbaya nchini Yemen ambayo imepelekea kuuawa na kujeruhiwa makumi ya maelefu ya Wayemeni na kuharibiwa miundo msingi ya nchi hiyo.
Hali kadhalika washiriki katika kikao hicho wamesisitiza kuwa mgogoro wa sasa wa Yemen unapaswa kutatuliwa tu kwa njia za kidiplomasia huku wakisisitiza ulazima wa misaada ya kibinadamu kuwafikia watu wa Yemen.
Baada ya kikao hicho cha Tehran, wajumbe wa Iran, Yemen na Ulaya wametoa wito wa utekelezwaji kikamlifu mapatano yaliyofikiwa mjini Stocholm Sweden mwaka 2018 ili kuandaa mazingira ya kumalizwa mgogoro wa Yemen.
Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ikishirikiana na UAE zilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasiopungua 16,000 wasio na hatia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇