Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha kusainiwa makubaliano ya maelewano baina ya marais wa Uganda na Rwanda, yanayolenga kurejesha uhusiano wa pande mbili katika hali ya kawaida.
Kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wa katibu mkuu siku ya Ijumaa, Stephane Dujarric amesema Guterres, ametoa wito kwa pande mbili kutekeleza makubaliano kwa nia njema, kwa mtazamo wa kurejesha uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya mataifa jirani na kwa maslahi ya amani, utulivu na maendeleo endelevu katika kanda.
Taarifa pia imesema katibu mkuu ametambua umuhimu wa jukumu la rais Joao Lourenco wa Angola na rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kuwezesha kusainiwa kwa makubaliano hayo.
Jumatano wiki hii Marais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda walisaini makubaliano ya amani katika mji mkuu wa Angola, Luanda yenye lengo la kumaliza uhasama na mzozo uliopo kati ya mataifa hayo mawili jirani.
Marais hao walifikia makubaliano hayo katika mkutano wa pili huko Luanda mbele ya marais wa Jamhuri ya Kidmeokrasia ya Kongo , Angola na Kongo Brazaville waliokuwa wapatanishi katika mgogoro huo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, makubaliano hayo sasa yanaandaa uwanja wa kufunguliwa tena uhusiano wa kibiashara baina ya pande mbili huku Rwanda ikiahidi kufungua mpaka wake.
Mnamo Machi mwaka huu katika hotuba kwenye mkutano wa kitaifa, Rais wa Rwanda Paul Kagame alielezea kuwa chimbuko la mgogoro baina ya nchi yake na Uganda ni la tangu miaka 20 iliyopita ambapo Uganda ilitaka kuangusha utawala wake.
Huku nyuuma kila moja kati ya nchi mbili hizo imekuwa ikikanusha tuhuma za upande wa pili na hata baadhi ya maafisa wa serikali hizo kuonyesha kwamba, hakuna mzozo na mgogoro wowote baina ya nchi mbili hizo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇