Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, Wapalestina wasiopungua 120 wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika maandamano ya 71 ya "Haki ya Kurejea' yaliyofanyika jana katika Ukanda wa Gaza.
Maandamano hayo ya jana yalifanyika kwa kaulimbiu ya "Tumeitika Ewe Aqsa".
Askari wa Kizayuni walitumia risasi moto, mabomu ya kutoa machozi na gesi ya sumu kuwakandamiza Wapalestina walioshiriki kwenye maaandamano hayo.
Maandamano hayo yalifanyika sambamba na kumbukumbu ya mwaka wa 50 ya jinai iliyofanywa na maghasibu wa Kizayuni ya kuuchoma moto msikiti wa Al Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu.
Maandamano ya amani ya "Haki ya Kurejea" yalianza tarehe 30 Machi 2018 kwa mnasaba wa Siku ya Ardhi huko Ukanda wa Gaza na hadi sasa yangali yanaendelea.
Hadi sasa nchi nyingi duniani ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na jumuiya mbalimbali za kimataifa zimelaani jinai hizo za utawala wa Kizayuni.
Maandamano ya Wapalestina yanayofanyika kila mwaka katika maadhimisho ya Siku ya Ardhi yanakumbusha uamuzi uliochukuliwa na utawala wa Kizayuni tarehe 30 Machi 1976 wa kupora ardhi za Wapalestina.
Kwa kupora ardhi hizo na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, utawala haramu wa Israel umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Wapalestina na kuyapa sura ya Kizayuni ili kuweza kuyadhibiti na kuyahodhi kikamilifu maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇