Wizara ya Afya ya Uganda imesema kuwa msichana mmoja mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amepatikana na virusi vya Ebola nchini Uganda. Wizara hiyo imesema kuwa, msichana huyo mwenye umri wa miaka 9, aliwasili nchini Uganda akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ingawa hata hivyo haikumtaja jina lake.
Wizara ya Afya ya Uganda aidha imesema kuwa, msichana huyo aliyegunduliwa kuwa na ugonjwa wa Ebola aliwasili katika eneo la mpakani la Mpondwe, kwenye mpaka wa DRC na Uganda Jumatano wiki hii kutafuta msaada wa matibabu katika mji wa Bwera, Wilayani Kasese, Kusini Magharibi mwa Uganda.
Kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi Agosti 28 nchini DRC, kesi 3004 za maambukizi ya virusi vya Ebola zilikuwa zimeshathibitishwa huko Kongo DR huku watu 1998 wakifariki dunia baada ya kuambukizwa virusi vya Ebola.
Kwa upande wake Bi Irene Nakasita, afisa wa mawasiliano wa shirika la Msalaba Mwekundu nchini Uganda amesema: "Msichana huyo alikaguliwa na kuchukuliwa vipimo na timu yetu inayosimamia eneo la mpaka wa Mpondwe. Wakati alipokuwa akifanyiwa vipimo, alionekana na dalili za virusi vya Ebola na aliondolewa mara moja sehemu hiyo."
Itakumbukwa kuwa mwezi Juni, watu watatu kutoka familia moja walifariki dunia nchini Uganda baada ya kuambukizwa virusi vya Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇