Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema kuwa, elimu ya wakimbizi iko hatarini na inaonesha kuwa kadiri watoto wakimbizi wanavyozidi kukua ndivyo vikwazo vya kupata elimu vinavyozidi kuongezeka.
Msemaji wa UNHCR Bi Melissa Fleming amesema kuwa, “Ni asilimia 63 tu ya watoto wakimbizi ambao wanapata bahati ya kwenda shule ya msingi ikilinganishwa na asilimia 91 kimataifa. Hali ya wakimbizi hao inakuwa mbaya zaidi wakati wanapofika umri wa kusoma masomo ya sekondari kwani ni asilimia 24 tu ya wakimbizi ndio hupata fursa hiyo ikilinganishwa na asilimia 84 kimataifa.”
Bi Fleming ameongeza kuwa, “Vikwazo kwa elimu kwa wakimbizi vinazidi kuongezeka kadiri wanavyozidi kukua. Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema, “Shuleni ni mahali ambapo wakimbizi wanapatiwa fursa ya pili. Tunawaangusha wakimbizi kwa kutowapa fursa ya kukuza stadi na maarifa wanayoyahitaji kuwekeza katika mustakabali wao.”
Melissa Fleming ameongeza kuwa, “Vikwazo kwa elimu kwa wakimbizi vinazidi kuongezeka wanavyozidi kukua na jambo hilo linatengeneza mzunguko usiokuwa na mwisho. Usipokuwa na watoto katika shule za sekondari, hawataweza kupata elimu ya juu hata kama ingekuwepo.”
UNHCR vile vile imeelezea kusikitishwa sana na hali hiyo ikisema kuwa, kupungua kwa kasi uandikishaji wa watoto wa wakimbizi kati ya shule za msingi na sekondari, ni matokeo ya moja kwa moja ya kutokuweko ufadhili wa kutosha kwa elimu ya wakimbizi.
Shirika hilo la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa limetoa mwito kwa serikali, sekta binafsi, mashirika ya elimu na wachangiaji kuufadhili kifedha mkakati mpya unaolenga kuhamasisha na kusogeza karibu elimu ya sekondari kwa wakimbizi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇