Mshauri wa Waziri wa Ulinzi wa serikali ya Abdrabbuh Mansur Hadi, rais aliyejiuzulu na kutoka nchi wa Yemen, amekiri kwamba umri wa kisiasa wa serikali hiyo umefika ukingoni na kusema: Hakuhitajiki tena harakati ya Ansarullah kwa ajili ya kufuta kabisa serikali hiyo bali wanamgambo wanaosaidiwa na Imarati wamekamilisha jukumu hilo.
Februari mwaka 2012 Abdrabbuh Mansur Hadi alishika madaraka kama rais wa muda wa Yemen. Iliamuliwa kuwa Hadi ambaye awali alikuwa makamu wa aliyekua rais wa Yemen, Abdullah Saleh, angeongoza nchi hiyo kwa kipindi cha mpito cha miaka miwili na kutayarisha mazingira ya kuitishwa chaguzi za rais na bunge na hatimaye kuundwa serikali mpya. Hata hivyo baada ya kumalizika miaka hiyo miwili chaguzi hizo hazikuitishwa na badala yake Abdrabbuh Mansur Hadi alirefusha kinyume cha sheria utawala wake kwa kipindi kingine cha miaka miwili. Katika kipindi hicho na kutokana na kwamba Mansur Hadi alichukua madaraka kwa uungaji mkono wa Saudia na Marekani, utegemezi wa Yemen kwa nchi za kigeni uliongezeka zaidi. Ni katika mazingira hayo ndipo watu wa Yemen wakiongozwa na harakati ya Ansarullah wakaanzisha harakati ya upinzani hapo mwaka 2014 ambayo ilimlazimisha Abdrabbuh Mansur Hadi kujiuzulu na kutoroka mjini Sana'a.
Miongoni mwa dalili na ishara za kumalizika umri wa kisiasa wa Abdrabbuh Mansur Hadi na serikali yake kibaraka kwa Saudia ni kuimarika zaidi Baraza Kuu la Siasa lililoundwa na Ansullah katika mji mkuu wa Yemen, San'aa na hata kutumwa mabalozi katika baadhi ya nchi kama wawakilishi wa Yemen. Hii leo hakuna tena mjadala wa kutupiliwa mbali harakati ya Ansarullah, na kinyume chake, harakati hiyo ndiyo sababu kuu ya kumalizika mapema umri wa kisiasa wa Abdrabbuh Mansur Hadi na kibaraka huyo wa Saudi Arabia.
Dalili na ishara ya pili ni kuimarika nafasi ya Baraza la Mpito la Kusini linaloungwa mkono na Imarati. Baraza hilo liliundwa mwaka 2017 baada ya kushadidi hitilafu baina ya Imarati na Abdrabbuh Mansur Hadi, na Meja Jenerali Aidarus Qassem al-Zoubaidi gavana wa Aden aliyekuwa ametimuliwa na Mansur Hadi akapewa jukumu ya kuongoza baraza hilo. Kwa utaratibu huo eneo la kusini mwa Yemen kivitendo likawa na serikali mbili tofauti na hatua kwa hatua Baraza la Mpito la Kusini likaimarika zaidi siku baada ya siku na hatimaye tarehe 10 Agosti likafanikiwa kuwashinda waungaji mkono wa Abdrabbuh Mansur Hadi na kutwaa ikulu ya Rais mjini Aden.
Ishara ya tatu ni mazungumzo yanayofanyika baina ya Saudi Arabia na Baraza la Mpito la Kusini. Saudia inaiunga mkono serikali iliyojiuzulu ya Abdrabbuh Mansur Hadi na chama cha al Islah, lakini pande hizo mbili sasa zimepigwa mweleka na kushindwa na wapiganaji wa Baraza la Mpito la Kusini. Abdrabbuh Mansur Hadi anaitaka Riyadh iendelee kumsaidia na kumuunga mkono lakini Saudia imekhitari kufanya mazungumza na mahasimu wake walioko chini ya mwavuli wa Baraza la Mpito la Kusini. Mazungumzo hayo yanafanyika huku mapigano ya niaba baiya na makundi yanayosaidiwa na Saudia na yale yanayofadhiliwa na Imarati yakipamba moto na kupanuka zaidi katika maeneo ya kusini mwa Yemen.
Ishara hizo zote na kimya cha Abdrabbuh Mansur Hadi mkabala wa yanayojiri ni kielelezo kwamba, umri wa kisiasa wa rais huyo wa zamani wa Yemen na serikali yake umefika ukingoni. Kwa kutilia maanani ukweli huo shirika la habari la Reuters limemnukuu afisa mmoja wa Yemen akisema: Abdrabbuh Mansur Hadi amepoteza nafasi yake muda mrefu huko nyuma na atatupiliwa mbali kama tambara bovu baada ya kukamilika mchakato wa nani atakayechukua nafasi yake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇