Mkutano huo wa kilele wa mwaka huu hata hivyo utakwenda kinyume na utamaduni wake kwa kutokuwa na taarifa ya pamoja baada ya kumalizika kwake. Mwenyeji wa mkutano huo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesema hatua hiyo inalenga kuwaepushia wakuu wa nchi na serikali kujiepusha na mivutano itakayotokana na kutokubaliana na pia kuepusha kuzianika wazi tofauti zitakazojitokeza baina yao.
Ni wazi kuwa Marekani haikubaliani na Rais Macron na viongozi wengine juu ya masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa, na wakati huo huo maoni ya Rais Donald Trump juu ya biashara ya kimataifa na maamuzi yake ya kuzitoza ushuru zaidi bidhaa kutoka nchi washirika wa Marekani sawa na maadui zake yamesababisha mkwaruzano na washirika wake wa karibu.
Mkutano wa viongozi hao wa ulimwengu wa nchi za G7 bila shaka utagonga vyombo vya habari.
Rais Donald Trump leo Jumapili atafanya kikao na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, kabla ya ufunguzi rasmi wa mkutano G7. Trump na Johnson wanakutana kwa mara ya kwanza kama viongozi, na wanatarajiwa kuzungumzia mpango wa biashara kati ya nchi zao baada ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya.
Macho yote yatakuwa kwa Boris Johnson ambaye anahudhuria mkutano wa kwanza wa kimataifa tangu alipoingia madarakani mnamo mwezi Julai kwa ahadi ya kuiondoa Ungereza kutoka kwenye Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na kurudisha hadhi ya taifa lake.
Mazungumzo ya waziri mkuu huyo wa Uingereza na Rais wa Tume wa Ulaya Donald Tusk baadaye leo yanaweza kuwa ya mvutano baada ya viongozi hao kukwaruzana hapo siku ya Jumamosi juu ya nani atakaye laumiwa ikiwa Uingereza itaondoka kutoka Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano.
Kikao cha kwanza cha G7 kinatarajiwa kuangalia masuala ya uchumi wa kimataifa, biashara na usalama.
Baada ya chakula cha mchana, marais, mawaziri wakuu na viongozi wa mashirika ya kimataifa wanaohudhuria mkutano huo wa kilele wa G7 watajadili juu ya ukosefu wa usawa ulimwenguni. Washindi wa Tuzo ya Amani Nobel Denis Mukwege na Nadia Murad watawasilisha mada juu ya maswala ya usawa wa kijinsia.
Baadae viongozi wanaohudhuria kutoka bara la Afrika watahutubia. Masuala kuhusiana na eneo la Sahel yaliyokubaliwa na wingi wa makundi ya kijihadi yatapewa kipaumbele maalum.
Vyanzo:/DPA/AFP
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇