Wabunge wa Ethiopia, jana Jumamosi, Agosti 24, 2019 walipasisha sheria mpya ya uchaguzi katika kipindi hiki ambacho uchaguzi mkuu nchini humo unatarajiwa sana kufanyika mwakani, 2020.
Wabunge wameitisha kikao cha dharura cha kujadili muswada wa sheria hiyo ambayo mchakato wake ulianza tangu Waziri Mkuu mpya, Abiy Ahmed alipoingia madarakani mwezi Aprili 2018.
Shirika la Taifa la Utangazaji la Ethiopia lilitangaza jana kuwa, sheria hiyo mpya inayohusiana na usajili wa vyama vya siasa na uchaguzi imepasishwa kwa kauli moja na Bunge.
Hata hivyo mtandao wa habari wa Addis Standard umesema kuwa, kifungu kilichopendekezwa kwenye sheria hiyo kwa ajili ya kutoa upendeleo maalumu kwa wanawake, kimekataliwa na wabunge hao. Kifungu hicho kilikuwa kinataka wanawake wapewe nafasi zaidi ya kushinda na sio kushindana kura kwa kura na wanaume.
Muungano tawala wa Ethiopia EPRDF mara kwa mara umekuwa ukisisitizia ulazima wa kufanyika uchaguzi katika muda uliopangwa.
Hivi sasa viti vyote vya Bunge la Ethiopia vimo mikononi mwa muungano huo tawala unaoongozwa na Waziri Mkuu, Abiy Ahmed.
Wapinzani katika nchi hiyo ya pili kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika nao wametoa mwito huo huo wakihimiza kupasishwa marekebisho yote ya uchaguzi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ambayo hivi sasa imezongwa na machafuko ya kikabila na ukosefu wa amani na usalama.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇