Taasisi ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ya Solh-e Ziba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuutaka umoja huo uandae haraka mazingira ya kuchiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ili aende akatibiwe nje ya nchi.
Shirika la habari la Fars limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, barua hiyo imesema kuwa, kwa mujibu wa taarifa za kina na za uhakika za wataalamu wa asasi za kijamii na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu, hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ni mbaya hasa baada ya kupigwa risasi na wanajeshi wa Nigeria, hivyo Umoja Mataifa unapaswa kutumia uwezo wake wa kisheria na kimataifa kuandaa mazingira ya kuachiliwa huru kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu na kutibiwa nje ya nchi.
Taasisi hiyo ya haki za binadamu ya Solh-e Ziba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imegusia hisia za mamilioni ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky katika pembe mbalimbali za dunia na kusisitiza kuwa, kutishia usalama wa maisha ya kiongozi huyo kunaweza kusababisha hatari za kiusalama na uvunjifu wa amani katika sehemu mbalimbali duniani.
Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anashikiliwa na jeshi na serikali ya Nigeria tangu mwaka 2015 baada ya kupigwa risasi wakati wanajeshi wa nchi hiyo walipovamia nyumba yake mjini Zaria na kuua mamia ya Waislamu.
Sheikh Zakzaky na mkewe walijeruhiwa kwa risasi katika uvamizi huo huku watoto wawili wa kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu wakiuliwa shahidi na jeshi la Nigeria pamoja na mamia ya Waislamu wengine.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇