Rais wa Afrika Kusini amesema nchi hiyo kamwe haitaruhusu uchumi wake uvurugwe na kurejeshwa nyuma kutokana na vita vya kibiashara vya Marekani, vilivyochechewa na wivu.
Cyril Ramaphosa aliyasema hayo jana Ijumaa katika Kongamano la Uchumi na Teknolojia na kubainisha kuwa, nchi hiyo haitakubali uchumi wake ukose kuimarika kutokana na vita vya kibiashara kati ya Marekani na China.
Rais wa Afrika Kusini ameeleza bayana kuwa, "Kabla ya kwenda Mkutano wa G20 mwishoni mwa wiki iliyopita, kampuni kadhaa za mawasiliano ziliniandikia waraka zikinitaka niingilie kati."
Amesema mashirika hayo yalimwambia kuwa, "mkwaruzano wa kibiashara kati ya Marekani na China unatuathiri. Sisi tunataka kwenda katika mfumo wa 5G, na kampuni ya Huawei ndiyo inayoweza kutupeleka huko, lakini Marekani hivi sasa inaiadhibu kampuni hiyo."
Cyril Ramaphosa amesema: "Katu hatutaruhusu uchumi wetu uvutwe nyuma kwa kuwa kuna vita ambavyo Marekani inapigana na ambavyo vimezaliwa kutokana na wivu wao wenyewe."
Hivi karibuni, Wizara ya Biashara ya China ilisisitizia udharura wa kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya mashirika ya nchi hiyo likiwemo la Huawei.
Msuguano wa kibiashara wa China na Marekani ulianza tarehe 8 Machi 2018, baada ya Trump kuzipandishia ushuru wa forodha bidhaa za China.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇