LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 18, 2019

TANZANIA YANG'ARA UMOJA WA MATAIFA UTEKEAJI SDGs

Na Saidina Msangi, WFM, New York, Marekani
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) amewasilisha ripoti ya Tanzania kwa mara ya kwanza ya Mapitio ya Hiyari ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu katika Mikutano ya Jukwaa la Juu la Kisiasa la Ngazi za Mawaziri chini ya Umoja wa Mataifa inayofanyika New York nchini Marekani.

Akiwasilisha ripoti hiyo Waziri Mpango ameeleza kuwa Tanzania imefanikiwa katika utekelezaji wa malengo 17 yaliyoamuliwa kutekelezwa na nchi zote ulimwenguni ili kuondokana na umasikini na kuharakisha maendeleo katika nyanja zote.

Akizungumzia lengo namba nne lenye kuangazia elimu jumuishi na bora kwa wote, Dkt. Mpango ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza ambao wana mwaka mmoja wa elimu ya awali kwa asilimia 95.6 mwaka 2018 ambayo ni juu ya makadirio ya asilimia 87.5 ifikapo mwaka 2020.

Aidha, wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza wameongezeka kwa asilimia 17.4 ikiwa ni kutokana na mafanikio ya elimu bure chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Pia Dkt. Mpango aliongeza kuwa Tanzania imefanikiwa katika maeneo ya utoaji huduma bora za afya, uongozi bora na amani ya nchi kwa ujumla.

Ripoti hiyo imepokelewa vizuri  katika Jukwaa hilo la Umoja wa Mataifa ambapo nchi zilizotoa maoni kuhusu ripoti hiyo ikiwemo Kenya zimepongeza juhudi zilizofikiwa na Tanzania katika utekelezaji wa malengo endelevu.

“Malengo haya ndio dira ya maendeleo na yanaunganika na mipango yetu ya maendeleo kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanaendana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, na MKUZA kwa upande wa Zanzibar hivyo ni lazima tutekeleze malengo haya kwa bidii,” alisema Waziri Mpango.

Dkt. Mpango ametoa wito kwa Jumuiya ya Umoja wa Mataifa na nchi zenye utaalamu kuisaidia Tanzania katika matumizi ya teknolojia ili kuweza kufikia azma ya malengo endelevu upande wa utunzaji wa mazingira.

Waziri Mpango amewashukuru wadau wote, sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali kwa ushiriki wao katika kuandaa ripoti hiyo kwa kiwango kizuri. Aidha ametoa wito kwa taasisi na sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa rasilimali fedha na utaalamu zitumike kwa ajili ya kushughulikia utekelezaji wa malengo endelevu.

Tanzania imeungana na nchi zote duniani katika utekelezaji wa malengo 17 yaliyoazimishwa  miaka minne iliyopita  ikiwa ni mkakati wa kufikia  ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu.

Mikutano hiyo yenye kauli mbiu uwezeshaji wa watu na kuhakikisha ujumuishwaji na usawa imekutanisha nchi mbalimbali ambazo zimetuma wawakilishi kutoka Serikalini na Sekta binafsi, inatoa fursa kwa nchi kuweza kutathmini mafanikio, changanoto na mambo ya kujifunza katika kuelekea utekelezaji wa malengo 17 ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages