Kupungua kwa bajeti na mishahara ya mabalozi na wanadiplomasia wa Israel kumewafanya maafisa hao waiandikie barua Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala huo wakitishia kujiuzulu.
Tangu mwaka 2014 baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel lilichukua uamuzi wa kupunguza bajeti ya wizara zote ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje. Kuongezeka kwa matatizo ya kiuchumi ndiyo sababu ya uamuzi huo uliochukuliwa wa baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel. Ongezeko la ukata na umaskini sasa limekuwa tatizo kubwa la kiusalama kwa Israel kwa kadiri kwamba, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Bima la Taifa la Israel iliyotolewa mwishoni mwa mwaka 2016, mtu mmoja kati ya kila Waisraeli 5 anaishi chini ya mstari wa umaskini yaani katika ukata wa kupindukia.
Kuenea kwa ukata na umaskini huko Israel kumetokana na sababu kadhaa. Ya kwanza na muhimu zaidi ni sera za kupenda vita za utawala huo wa Kizayuni ambazo zinatoa kipaumbele kwa masuala ya kijeshi badala ya kijali hali ya kimaisha ya watu wa kawaida. Mbali na gharama kubwa zinazotumiwa na utawala huo haramu katika masuala ya kivita na kununua silaha, Israel pia imeanzisha vituo zaidi ya 40 ya mafunzo ya kijeshi katika miaka kadhaa ya hivi karibuni. Sera hizo za kivita na kijeshi za Israel hasahasa kuhusiana na masuala ya magharibi mwa Asia zimepandisha juu ghara za kijeshi kwa kiwango kikubwa na kupelekea kupungua bajeti ya sekta nyingine.
Uamuzi wa Israel wa kupunguza bajeti ya wizara mbalimbali ulichukuliwa baada ya vita vya utawala huo dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza mwaka 2014 na unahesabiwa kuwa ni miongoni mwa taathira mbaya za vita hivyo.
Pamoja na sera hizo za kivita za Israel tunapaswa kutaja ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina kuwa ni miongoni mwa sababu kuu za kupunguzwa bajeti ya wizara za utawala huo. Tangu mwaka 2009 wakati Benjamin Netanyahu alipochaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Israel, nyumba zisizopungua elfu 20 za walowezi wa Kizayuni zimejengwa katika ardhi ya Ukingo wa Magharibi.
Waziri wa Ujenzi na Nyumba wa Israel, Yoav Gallant alisema Agosti mwaka 2018 kwamba, utawala huo umetumia shekel bilioni moja kwa ajili ya kupanua vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi baina ya mwaka 2015 na 2018 pekee. Gharama za masuala ya vita na zana za kijeshi na vilevile ujenzi na upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina umepelekea kupunguzwa bajeti ya wizara nyingine za utawala huo na vilevile bajeti ya masuala ya kimaisha ya watu wa kawaida. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana mabalozi na wanadiplomasia wa utawala wa Kizayuni katika nchi za nje wakatishia kujiuzulu baada ya mishahara yao kupunguzwa. Mwandishi wa mtandao mmoja wa habari wa Israel ameandika kuwa: "Katika barua yao, mabalozi na wanadiplomasia wa Israel katika nchi za nje wamesema kuwa kwa mbinu inayotumika sasa, Israel inaelekea kuangamiza mfumo wa udiplomasia na kuwa utawala pekee unaoendesha mahusiano yake ya kigeni kwa mbinu mbovu na isiyo na mpangilio."
Hii si mara kwanza kwa wanadiplomasia wa Israel kutoa malalamiko kama haya. Karibu wafanyakazi 600 wa Israel katika nchi mbalimbali duniani Agosti mwaka jana walifanya mgomo wakilalamikia kiwango kidogo cha mishahara yao. Mwaka wa kabla yake pia wafanyakazi wa balozi za Israel walifanya mgomo wakilalamikia hali hiyo hiyo.
Barua ya sasa ya kutishia kujiuzulu mabalozi na wanadiplomasia wa Israel imeandikwa baada ya baraza la mawaziri la Netanyahu kutikiswa na wimbi kubwa la machafuko na maandamano ya Wayahudi wenye asili ya Ethiopia (mafalasha) ambao wanapinga ukandamizaji na kubaguzli ndani ya jamii ya Israel.
Hatua hiyo ya mabalozi na wanadiplomasia wa Israel pia yumkini ikamtia mashakani Benjamin Netanyahu katika uchaguzii ujao wa bunge uliopangwa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇