Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza kuitetea Korea Kusini katika mzozo unaoendelea kati ya nchi hiyo na Japan.
Shirika rasmi la Habari la Korea Kaskazini KCNA limetangaza radiamali ya serikali ya Pyongyang kufuatia vizingiti vilivyowekwa na Japan kwa baadhi ya bidhaa zake zinazoingizwa Korea Kusini, kutokana na mgogoro wa kidiplomasia wa zamani kati ya nchi hizo, ambapo nchi hiyo imeikosoa vikali serikali ya Tokyo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Korea Kaskazini imeituhumu pia Japan kuwa inadhoofisha amani na usalama katika Rasi ya Korea.
Mzozo kati ya Seoul na Tokyo ulianza mwaka uliopita baada ya Mahkama Kuu ya Korea Kusini kutoa hukumu ambayo inayalazimisha mashirika ya Japan kuwalipa fidia wahanga wa eneo la Korea waliotumikishwa kwa lazima katika kipindi cha vita. Katika radiamali yake kufuatia hukumu hiyo, serikali ya Japan nayo iliziwekea vizingiti baadhi ya bidhaa zake za kiteknolojia zinazosafirishwa kwenda Korea Kusini na zinazotumika katika viwanda vya nchi hiyo. Kadhalika serikali ya Tokyo ilitangaza kwamba vizingiti hivyo viliwekwa kutokana na kile ilichosema ni sehemu ya vifaa hivyo kutumwa Korea Kaskazini, na hivyo kukiuka vikwazo vya Marekani na Umoja wa Mataifa ilivyowekewa serikali ya Pyongyang. Serikali ya Korea Kusini imeitaja taarifa hiyo ya Japan kuwa isiyo na msingi wowote.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇