Serikali ya Korea Kaskazini imesema kuwa, hatua ya Washinton ya kurefusha vikwazo kwa muda wa mwaka mmoja dhidi ya Pyongyang ni kielelezo cha uhasama wa wazi wa nchi hiyo.
Pyongyang imesema hayo ikijibu hatua ya Washington ya kurefusha vikwazo vyake dhidi yya Korea Kaskazini na kuongeza kuwa, kitendo hicho kinaonyesha uhasama wa juu na ni changamoto ya wazi kwenye mapatano ya kikao cha kihistoria cha nchi mbili kilichofanyika mwaka jana nchini Singapore.
Hivi karibuni Rais Donald Trump wa Marekani alitoa amri sita kwa ajili ya kuiwekea vikwazo miradi ya makombora na nyuklia ya Korea Kaskazini kwa muda wa mwaka mmoja zaidi. Kabla ya hapo pia, Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini iliitaja hatua hiyo ya Washington kuwa ni sawa na tangazo rasmi la hatua za uhasama za Marekani dhidi ya Pyongyang.
Duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Trump na Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini, ilifanyika Juni 2018 nchini Singapore ambapo pande mbili zilitiliana saini makubaliano kadhaa. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Kim Jong-un alikubali kwamba, nchi yake itaangamiza silaha za nyuklia na mkabala wake Washington nayo ilitakiwa kuidhaminia nchi hiyo usalama wake. Hata hivyo muda mfupi baadaye Trump alirefusha vikwazo vya mwaka mmoja dhidi ya nchi hiyo, suala ambalo lilikosolewa vikali na serikali ya Pyongyang.
Baada ya hapo viongozi wa nchi mbili walikutana nchini Vietnam Februari mwaka huu. Hata hivyo sera za kupenda makubwa za Washington zilipelekea kuvunjika kwa mazungumzo hayo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇