Rais wa Senegal, Macky Sall ambaye alishinda muhula wa pili katika uchaguzi wa hivi karibuni amemtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuzindua mageuzi ya uongozi, yanayojumuisha kufuta wadhifa wa Uwaziri Mkuu.
Waziri MKuu wa nchi hiyo, Mahammed Boun Abdallah Dionne ambaye hivi karibuni aliteuliwa tena na Rais Sall kuendelea kushikilia wadhifa huo amesema kwa mujibu wa amri ya rais wa nchi hiyo, lengo la mageuzi hayo ni kuleta mfumo wa utawala ulioko karibu zaidi na wananchi, ili kuharakisha mchakato wa mabadiliko yatakayokuwa na taathira.
Kwa mujibu wa dikrii iliyosomwa na Rais Sall kupitia televisheni ya dola, Dionne ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jamhuri, nafasi ambayo anatazamiwa kuendelea kuishika mara tu mchakato wa kufuta Ofisi ya Waziri Mkuu utakapokamilika.
Waziri Mkuu wa Senegal ambaye binafsi haoenekani kupinga mageuzi hayo, amesema mabadiliko hayo ya uongozi yatasaidia pia kuondoa suitafahamu katika mzunguko na uenezaji wa taarifa za serikali.
Rais Macky Sall wa Senegal alishinda tena kiti cha urais kwa kuibuka na ushindi wa asilimia 58 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa mwezi Februari mwaka huu.
Sall mwenye umri wa miaka 57 alianza siasa akiwa mwanachama wa chama kilichokuwa kikiongozwa na Wade cha Senegalese Democratic Party (PDS) na kisha baina ya mwaka 2004 na 2007 akawa Waziri Mkuu wake, kabla ya kuwa rais wa nchi hiyo mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇