NA IMMACULATE MAKILIKA- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa ni lazima kutekeleza masuala mbalimbali aliyoyaahidi Watanzania wakati akiingia madarakani mwaka 2015, ambayo yanalenga kuwaletea wananchi maendeleo.
wakati alipokuwa akizindua mji wa Serikali uliopo katika kata ya Mtumba jijini Dodoma, Rais Magufuli alisema kuwa aliamua kutimiza ahadi ya Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyoitoa mwaka 1973 ya kulifanya jiji la Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.
Rais Magufuli alisema “Nataka yote tuliyoyaahidi tuyatekeleze, nataka ofisi hizi nzuri tulizojenga ziwe na watu, na zianze kutoa huduma kwa wananchi”
Alisisitiza, “ jukumu langu lilikuwa kutekeleza ahadi ya Mwalimu Nyerere, na nilipata nguvu baada ya kukumbuka kuwa ziko nchi nyingi tu duniani ikiwemo nchi za Afrika kama Nigeria na Cote d’Ivoire ambazo zilihamisha makao makuu ya nchi yao katika kipindi kifupi, nataka kuwahakikishia na mimi nakuja Dodoma kwa sababu hakuna kinachonichelewesha”
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa Serikali inaendelea kukamilisha mifumo na ujenzi wa miradi mbalimbali kwa ajili ya kutoa huduma kwa watumishi wa umma ambao watahamia na kufanya kazi katika majengo hayo ikiwa ni pamoja na kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wanaofika katika mji huo wa Serikali, ikiwa ni sambamba na kuboresha jiji la Dodoma.
Alitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa barabara itakayogharimu bilioni 500 kwa mkopo wa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) itakayojengwa kutokea Mtumba, Veyula na Nala ambayo ina urefu wa kilomita 4.
Vile vile amesema, serikali inaendelea na ujenzi wa uwanja wa ndege mkubwa na wa kimataifa unaogharimu bilioni 400 pia inafanya maandalizi ya ujenzi wa Bandari kavu kwa vile jiji la Dodoma lina kituo kikuu cha reli ya kisasa (SGR).
Katika jitihada za Serikali za kuliboresha jiji la Dodoma ambalo ni Makao Makuu ya nchi, Serikali imepanga kujenga shule ya sekondari ya kisasa itakayogharimu shilingi bilioni 13na Chuo cha mafuzo (VETA) kitakachogharimu shilingi bilioni 18. Ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha hospitali ya Benjamini Mkapa ambayo imeanza kutoa matibabu ya kibingwa.
Aidha, Rais Magufuli alilipongeza Jeshi la Wananchi kwa kujenga majengo hayo ya mji wa Serikali, pamoja na kushiriki katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali ikiwemo ukuta wa Mererani uliopo Arusha, ambapo amempandisha cheo msimamizi wa miradi hiyo ya ujenzi Kanali Charles Mbuge pamoja na kutoa ajira kwa vijana walioshiriki katika ujenzi huo.
Rais Magufuli, “Kanali Mbuge atakuwa Brigedia kuanzia leo, nataka ufanyike utaratibu wa kumuongezea vyeo ufanyike na aendelee na hii kazi. Tuwe na kikosi cha ujenzi na kiongozwe na Mbuge ili kusaidia kufanya maajabu katika nchi hii, nawapongeza Jeshi la Wananchi, kwani mnafanyakazi nzuri”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amempongeza RaisMagufuli kwa uamuzi wake wa kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma kwani uamuzi huo utasaidia kusogeza huduma kwa wananchi, pamoja na kusaidia ukuaji wa uchumi katika mikoa iliyopo katikati ya nchi.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu Jenista Mhagama, alisema kuwa katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano miradi mbalimbali imetekelezwa katika jiji la Dodoma ikiwemo uzalishaji umeme megawati 48, huku mahitaji halisi yakiwa megawati 28.
Akitaja baadhi ya miradi mingine inayoendelea kutekelezwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za mzunguko ndani ya Dodoma yenye urefuwa kilomita 39 pamoja na kituo cha afya katika mji wa Serikali kitakachogharimu bilioni 4.5.
Awali Rais Magufuli alizindua jengo la ofisi zake, pamoja na nyumba 41 za wafanyakazi wa Ikulu vilivyopo Chamwino jijini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, akiteta jambo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwenye uzinduzi wa mji wa Serikali eneo la Mtumba, jijini Dodoma Aprili 13, 2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akitoa taarifa ya Serikali kuhamia Dodom, kwenye uzinduzi wa mji wa Serikali eneo la Mtumba, jijini Dodoma Aprili 13, 2019. Mgeni rasmi alikua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli. (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU).
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇