Na Benny Mwaipaja, WFM, Washington DC
TANZANIA imeunga mkono uamuzi wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika-AfDB wa kutaka kuongezewa mtaji ili iweze kutekeleza majukumu yake ya
kutoa mikopo kwa nchi wanachama wa benki hiyo kwa lengo la kuchochea zaidi
maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano wa 7 wa magavana wa
ambao ni Mawaziri wa Fedha kutoka nchi 54 wanachama wa Benki hiyo,
Mjini Washington DC, Marekani, Waziri wa Fedfha na Mipango, Dkt. Philip Mpango
ameeleza kuwa AfDB imefanya mambo makubwa nchini Tanzania ndio sababu inaunga
mkono kusudio hilo.
Amesema kuwa Benki hiyo imeipatia Tanzania mabilioni ya shilingi
kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa
miundombinu ya barabara, kilimo, nishati na maji.
Benki inataka kuongezewa mtaji kwa asilimia 200 kutoka wastani
wa UA bilioni 67.69 hadi UA 191.89 (kutoka dola za Marekani 94.76 hadi dola
bilioni 268.6 ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na kijamii ya nchi wanachama
hususan katika ujenzi wa reli, barabara, usafiri wa anga, tehama, bandari,
uzalishaji na usambazaji wa nishati.
"Wakati umefika ili twende haraka zaidi, mitaji sehemu
nyingine imepungua, pendekezo la kuongeza mtaji wa benki hii ni jema na matokeo
ya miradi inayofadhiliwa na Benki hii yanaonekana katika nchi zetu za kiafrika
kwa sababu benki hii iko Afrika na inaijua Afrika tofauti na benki
nyingine" alisisitiza Dkt. Mpango
Uamuzi wa nchi za Kiafrika zenye hisa katika Benki ya Maendeleo
ya Afrika ya kutaka Benki hiyo iongezewe mtaji ulitolewa wakati wa mkutano wa
Magavana wa Benki hiyo mjini Rome, Italia, baada ya mahitaji ya nchi wanachama
ya kutafuta mikopo kwenye taasisi hiyo kuongezeka.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇