Wanafunzi watatu wa kike wameuawa na watu wengine 20 wamejeruhiwa katikka shambulio lililofanywa na ndege za kivita za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika mji mkuu wa Yemen, Sana-a.
Ndege za kivita za muungano huo wa kijeshi wa Saudia leo zimeshambulia eneo la Sa'awan katika mji mkuu wa Yemen, Sana-a, ambapo kwa mujibu wa vyombo vya habari kombora moja la ndege hizo limelenga eneo jirani na skuli ya Ar-Raaya na kuua wanafunzi watatu wa kike.
Ndege za kivita za utawala wa Aal Saud vilevile zimeshambulia kitongoji cha Kataf mkoani Sa'dah kaskazini mwa Yemen.
Habari nyingine kutoka Yemen inaeleza kwamba, jeshi na vikosi vya kujitolea vya nchi hiyo katika medani ya "tisa" ya mjini Sana-a vimeshambulia ngome za muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia na kuua mamluki kadhaa wa muungano huo vamizi.
Saudi Arabia, ikishirikiana na waitifaki wake kadhaa wa eneo, ilianzisha vita dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuurejesha madarakani utawala kibaraka na tiifu kwa Riyadh.
Nchi kadhaa za Magharibi, hususan Marekani na Uingereza zinaupatia muungano huo vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia silaha na zana za kisasa za kijeshi pamoja na misaada ya kilojistiki na kiintelijensia.
Hadi sasa maelfu ya raia wa Yemen wameuliwa na maelfu ya wengine wamejeruhiwa, mbali na mamilioni wanaotilika kwa maradhi, njaa na kupoteza makazi yao.
Aidha sehemu kubwa ya miundomsingi ya Yemen imeteketezwa, huku mzingiro uliowekwa na Saudia dhidi ya nchi hiyo masikini ukiwakosesha raia maji safi na salama ya kunywa, chakula na huduma za afya.../
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇