Rais Kagame ameitoa kauli hiyo baada ya kuwasha mwenge wa kumbukumbu katika eneo maalum la kumbukumbu ya mauaji ya kimbari mjini Kigali, ambako zaidi ya watu 250,000 wanaaminika wamezikwa, wengi wao wakiwa ni kutoka jamii ya Watusti. Rais Kagame na mkewe Jeannette Kagame waliweka pia mashada ya maua kwenye eneo hilo.
''Mwaka 1994 hapakuwa na matumaini isipokuwa giza, lakini leo mwanga unaangaza kutoka eneo hili. Rwanda imekuwa tena familia moja,'' amesema Rais Kagame.
Akizungumza katika kituo cha mikutano cha mjini Kigali, Rais Kagame amesema miili na akili zao bado zimejawa na makovu, lakini hakuna hata mtu mmoja aliye peke yake, kwani wameungana tena kuonesha umoja wao.
Amebainisha kuwa Wanyarwanda wamebeba mambo mazito bila hata ya kulalamika, hatua ambayo imewaunganisha zaidi kuliko kabla na kwamba kilichotokea miaka 25 iliyopita, hakitatokea tena.
Viongozi mbalimbali wa kimataifa wanahudhuria kumbukumbu hiyo ya miaka 25 ya mauaji ya kimbari ambayo yaliushangaza ulimwengu. Viongozi hao ambao pia wameweka mashada ya maua ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Charles Michel, viongozi wa Chad, Jamhuri ya Kongo, Djibouti, Niger, Canada, Ethiopia pamoja na wawakilishi kutoka katika Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya.
Rais Kagame amezindua siku 100 za maombolezo zikiwa zinaakisi siku kama hizo ambapo mauaji yaliendelea tangu yalipoanza Aprili 7, mwaka 1994.
Mauaji yalianza baada ya ndege ya rais kudunguliwa
Mauaji ya kimbari nchini Rwanda yalianza siku moja baada ya ndege iliyokuwa imembeba Rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana kudunguliwa mjini Kigali Aprili 6, mwaka 1994 na kumuua kiongozi huyo kutoka kabila la wengi la Wahutu.
Watutsi walio wachache walishutumiwa kwa kuidungua ndege hiyo na hatimaye waiganaji wenye msimamo mkali wa Kihutu wakaanzisha mauaji dhidi ya Watutsi huku wakisaidiwa na jeshi, polisi pamoja na wanamgambo.
Kumbukumbu hizo zitaendelea hadi usiku ambapo Rais Kagame ataongoza mkesha utakaofanyika kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa Amahoro, ambao jina lake linamaanisha 'amani. Uwanja huo ulitumiwa na Umoja wa Mataifa wakati wa mauaji ya kimbari kuwahifadhi na kuwalinda maelfu ya Watusti ili wasiuawe. Watu wapatao 30,000 watahudhuria mkesha huo na kuwasha mishumaa kuwakumbuka wahanga.
Imeelezwa kuwa katika miaka ya nyuma kumbukumbu hizo zilikuwa zikisababisha machungu na maumivu makali kwa baadhi ya watu, huku wengi wao wakiangua vilio, wakitetemeka, wakipiga kelele au hata kuzimia katikati ya mkesha huo wa kumbukumbu. Bado imekuwa vigumu kwa waathirika kadhaa kusamehe, kutokana na miili ya wapendwa wao kutojulikana ilipo na pia wauawaji wengi kuwa huru.
Wakati huo huo, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ametaka kila Aprili 7 kuwa siku ya kumbukumbu ya ''mauaji ya kimbari ya Watusti'' nchini Rwanda. Katika taarifa yake fupi aliyoitoa leo siku ambayo mauaji yalianza, Macron ameelezea mshikamano wake na watu wa Rwanda. Kumbukumbu hiyo pia inafanyika leo Jumapili mjini Paris, ingawa Macron haudhurii.
Wakosoaji wamesema kuwa Ufaransa iliiunga mkono kwa kiasi kikubwa serikali iliyokuwa ikiongozwa na Wahutu ambayo wafuasi wake walifanya mauaji ya kimbari, huku baadhi yao wakisema wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa Rwanda walihusika katika mauaji hayo, madai ambayo Ufaransa imeyakanusha.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema mauaji ya kimbari ya Rwanda yanapaswa kuchukuliwa kama onyo kwa vizazi vijavyo. Akizungumza mjini Berlin, Maas amesema jumuia ya kimataifa haikuona ishara ya tahadhari ya mauaji ya kimbari mwanzoni mwa mwaka 1994, lakini amesema mauaji hayo yaliweza kuzuiwa kutokana na hatua zilizochukuliwa.
''Wote tuna wajibu wa kuizingatia kumbukumbu na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha tukio kama hili halijirudii tena,'' alifafanua Maas. Aidha, ameyaelezea mauaji ya kimbari kama ''uhalifu usioelezeka.''
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇