LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 19, 2019

MAJARIBIO MAPYA YA MKOMBORA LA KOREA KASKAZINI

Kim Jong-un Kiongozi wa Korea Kaskazini ameripotiwa kushuhudia jaribio la kombora hilo jipya. Hilo ni jaribio la kwanza kufanywa na nchi hiyo tokea kufanyika vikao viwili vya mazungumzo ya kiongozi huyo wa Korea Kaskazini na Rais Donald Trump wa Marekani mwezi Juni mwaka 2018 huko Singapore na mwezi Februari mwaka huu huko Hanoi, mji mkuu wa Vietnam. Kuendelezwa siasa za vikwazo za Marekani dhidi ya Korea Kaskazini sambamba na kufanyika mazungumzo ya nchi mbili, Korea Kusini kuendelea kununua silaha na duru mpya za maneva za kijeshi za Marekani na washirika wake katika Rasi ya Korea, kuliipelekea Korea Kaskazini kutangaza wiki kadhaa zilizopita kwamba ingeanzisha tena majaribio yake ya makombora iwapo mwenendo huo wa kichochezi wa Marekani haungesimamishwa. Majaribio hayo ya kombora jipya la Korea Kaskazini yametekelezwa katika hali ambayo White House ilikuwa imetoa jibu hasi kwa matamshi ya Kim Jong-un aliyeipa Marekani muhula wa kufikia mwishoni mwa mwaka huu iwe imechukua hatua za kuokoa mazungumzo ya nchi mbili na kuyazuia yasivunjike kabisa.
Trump akikutana na Kim Jong-un
Majaribio hayo mapya ya kombora la Korea Kaskazini yamethibitisha wazi kwamba nchi hiyo haiko tayari kuipa Marekani fursa nyingine ya kuvuruga na kutoheshimu mapatano yaliyofikiwa na pande mbili  kama ilivyofanya katika duru ya kwanza ya mazungumzo ya Singapore. Kwa maujibu wa mazungumzo hayo, Marekani ilitakiwa kusimamisha kwa muda vikwazo inavyotekeleza dhidi ya Korea Kaskazini huku nchi hiyo ikitakiwa kusimamisha majaribio yake ya makombora, hadi wakati wa kufikiwa mapatano ya mwisho kuhusiana na kuondolewa kabisa silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea. Licha ya kuwa Korea Kaskazini iliheshimu mapatano hayo kwa kusimamisha majaribio yake ya makombora lakini Marekani ilikiuka mapatano hayo na kuendelea kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya nchi hiyo ya Asia. Mbali na hayo, baadhi ya hatua za Marekani katika eneo zikiwemo za kufanya maneva za kijeshi na baadhi ya washirika wake wa eneo ni jambo lililoifanya Korea Kaskazini kufikia natija hii kwamba baada ya kushiriki kwenye mazungumzo ya miezi 9, Marekani inatekeleza kwa nguvu zake zote siasa za kutaka kuhodhi kila kitu kwa madhara ya Pyongyang, ambayo ilikuwa imesimamisha  majaribio yake yote ya makombora na kuanza kuharibu taasisi zake za nyuklia. Jenny Town, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Marekani anasema hivi kuhusiana na mazungumzo ya viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini: Kutofikiwa mapatano yoyote katika mazungumzo hayo kuna maana kwamba tumepoteza nishati yote iliyopatikana katika mwenendo wa kukurubiana nchi hizi nwaka uliopita na kila kitu kuanza kuporomoka. Mtazamo wa kutaka kuhodhi kila kitu bila shaka hautakuwa na tija kwa sababu pande zinazoshiriki mazungumzo huwa hazina imani na upande wa pili.
Mvutano wa Marekani na Korea Kaskazini kuhusu majaribia ya makombora ya Pyongyang
Hatua ya viongozi wa Korea Kaskazini ya kufanya tena majariobio ya makombora mapya imethibitisha wazi kuwa licha ya kuwa wanayatathmini mazungumzo na watawala wa Marekani kwa ajili ya kumaliza mzozo wa Rasi ya Korea kuwa chanya lakini wanaamini kuwa kuvunjika kwa mazungumzo hayo sio mwisho wa dunia na wamerejea kwa haraka katika hali iliyokuwepo kabla ya kuanza mazungumzo yao na Trump. Uzoefu mpya wa mazungumzo ya Korea Kaskazini na White House umethibitisha kwa mara nyingine kuwa katika uhusiano na nchi nyingine za dunia, Marekani hujiona kuwa bwana wa wenzake na hivyo kuwa na mtazamo wa kibeberu katika kufuatilia maslahi yake na kwamba ni lazima iushinde upande inaofanya nao mazungumzo. Pamoja na hayo lakini uamuzi wa Pyongyang kuanzisha tena majaribio yake ya makombora ya balistiki umetoa ujumbe huu kwa Marekani kwamba nchi huru na zinazojitawala hazitakubali tena kushiriki kwenye mazungumzo kama hayo ya kudhalilishwa na kushidwa na Marekani.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages