Msemaji wa vikosi vya Hizbullah nchini Iraq Sayyid Ja'afar al-Husseini sambamba na kulaani vikali, hatua ya uhasama ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH nchini Iran katika orodha ya makundi ya kigaidi, amesisitiza kwamba jeshi hilo la Iran daima limesimama pamoja na mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) katika kufelisha njama chafu za Washington.
Sayyid Ja'afar al-Husseini ameongeza kwamba kufuatia hatua hiyo muqawama wa Iraq daima utasimama bega kwa bega na jeshi hilo la Walinzi wa Mapinduzi nchini Iran kwa ajili ya kukabiliana na aina yoyote ya njama za mabeberu katika eneo hili. Kabla ya hapo pia Msemaji wa vikosi vya Hizbullah nchini Iraq alinukuliwa akisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, waliokuwa waungaji mkono pekee kwa taifa la Iraq katika kukabiliana na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS).
Wakati huo huo Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Al-Nujaba nchini Iraq ametoa radiamali kali kufuatia hatua hiyo ya kiuhasama ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH nchini Iran na amebainisha kwamba hatua hiyo ya Washington haitakuwa na taathira yoyote kwa makundi ya muqawama wa Kiislamu nchini Iraq na wala kwa jeshi hilo la Iran. Akibainisha kwamba uamuzi huo wa Trump ni sehemu ya hatua chafu za Marekani katika kuiwekea vikwazo vya upande mmoja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Hashim al-Musawi amesisitiza kwamba Iraq kamwe haitofuata vikwazo vya upande mmoja vya Washington dhidi ya Iran. Jumatatu ya jana Trump kupitia taarifa iliyosambazwa na White House aliliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH nchini Iran katika orodha ya makundi ya kigaidi hatua ambayo imeendelea kulaaniwa ndani na nje ya Marekani. Inafaa kuashiria kuwa, jeshi hilo la SEPAH limekuwa na nafasi kubwa sana katika kuendesha mapambano makali dhidi ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati kama vile genge la Daesh (ISIS) Jab'hatu Nusra, Jaishu al-Sham na mengineyo.
Katika uwanja huo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH nchini Iran na kupitia ombi rasmi la nchi za Iraq na Syria lilituma wataalamu wake wa ushauri kwa ajili ya kuyatokomeza makundi hayo, suala ambalo limekuwa likiwakera mno viongozi wa Marekani, utawala haramu wa Kizayuni, Saudia, Imarati na nchi nyingine za Magharibi kufuatia njama zao chafu kufelishwa na jeshi hilo la Iran.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇