Kwa miongo kadhaa sasa nchi hizo zimefanya juhudi kubwa kwa ajili ya kulifanya eneo la Mashariki ya Kati kuwa soko lao kubwa la silaha. Suala hilo ndilo limemfanya Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani kuonyesha ukosoaji wake mkali. Kiongozi huyo wa Kikristo anaamini kwamba Ulaya na Marekani zimehusika sana katika kufanya mauaji makubwa dhidi ya raia hususan watoto wa Syria, Yemen, Iraq na Afghanistan kutokana na hatua zao za uuzaji silaha. Akizungumza Jumamosi na wahadhiri na wanafunzi wa Chuo cha San Carlo mjini Milan, Papa Francis alisema: "Wamagharibi wanaunda silaha ili watu wengine wauane wao kwa wao, na lau kama si uuzaji silaha huo basi nchi kama vile Afghanistan, Yemen na Syria zisingeshuhudia vita. Nchi zinazounda na kuuza silaha zinatakiwa kuwa na utu na kuwaza namna ambavyo watoto na familia wanaangamia na kupata mateso." Papa alikuwa akiashiria vita vya sasa katika eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) kama vile vita vya ndani nchini Syria, ambapo Wamagharibi wakiongozwa na Marekani wamekuwa na nafasi kubwa katika kuvichochea na kuviibua, au kama vile vita vya Yemen ambapo pia Wamagharibi kwa kuiunga mkono moja kwa moja Saudi Arabia kupitia muungano wake vamizi, wamekuwa wakiiuzia Riyadh aina mbalimbali za silaha zinazotumika katika vita hivyo.
Kwa mujibu wa Sergey Syberibov, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Russia: "Marekani na Uingereza wanapata faida kubwa katika vita vya Saudia nchini Yemen."Wakati huo huo, mauzo ya silaha yanayofanywa na Wamagharibi, yamepelekea kuibuka ushindani wa umiliki silaha na kushtadi mizozo katika eneo la Mashariki ya Kati. Ukweli ni kwamba hatua za Wamagharibi katika uuzaji wake silaha kwa nchi washirika wao ndani ya eneo la Mashariki ya Kati inazingatia malengo mawili. Mosi ni kwamba, serikali za Magharibi, zinanufaisha kwa kiwango kikubwa sekta ya viwanda vyao vya silaha ambapo zinaajiri maelfu ya raia wao katika sekta hiyo kutokana na mauzo ya silaha nje ya nchi. Kuendelea na kuongezeka uzalishaji wa silaha umezifanya nchi hizo pia kustawi kiuchumi. Wakati huo huo Wamagharibi na katika utekelezaji wa siasa zao kuelekea kuzilinda tawala vibaraka wao, wanauza moja kwa moja silaha hizo kwa tawala hizo kwa ajili ya kuzitumia kukandamiza malalamiko ya wananchi kwa ajili ya kuzibakisha madarakani tawala tajwa. Kwa kuzingatia hali hiyo, nchi za Magharibi, si tu kwamba zimefumbia macho ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu ndani ya nchi washirika wao katika eneo la Mashariki ya Kati, bali hazizingatii pia jinai na mauaji ya kutisha yanayosababishwa na mauzo yao ya silaha kwa nchi washirika wao kama vile Saudi Arabia na Imarati ambazo hadi leo zinatekeleza mauaji ya kinyama nchini Yemen.
Katika uwanja huo Jeremy Corbyn, Kiongozi wa chama cha Labour nchini Uingereza sambamba na kukosoa vikali nafasi ya London katika kuiuzia silaha Saudia katika vita inavyoendesha nchini Yemen amesema: "Serikali ya Uingereza inatakiwa kusitisha haraka mauzo yake ya silaha kwa Saudia ili kuhitimisha mateso ya Wayemen." Licha ya kutolewa ripoti mbalimbali na asasi za haki za binaadamu kuhusiana na ukubwa wa jinai na mauaji ya raia nchini Yemen na kadhalika uharibifu wa makazi na idara za kiraia za nchi hiyo unaofanywa na ndege za kivita za Saudia na washirika wake na pia kukosolewa kila mara serikali ya Riyadh kutokana na ukiukaji wake mkubwa wa haki za binaadamu hususan baada ya mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud, lakini baadhi ya serikali za Magharibi hususan Marekani na Uingereza, bado zimeendeleza mahusiano yao ya karibu na utawala huo wa kifalme sambamba na kuendelea kuiuzia silaha ambazo zinatumika katika kufanya jinai na mauaji dhidi ya raia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇