Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa Waethiopia zaidi ya16,000 wanafariki kila mwaka kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.
Aidha ripoti hiyo imeongeza kuwa, karibu Waethiopia 16,000 huambukizwa Ukiwmi kila mwaka.
Taasisi ya afya ya umma ya Ethiopia imesema, watu wapatao laki 4.5 wa nchi hiyo wanapewa matibabu ya ARV ili kupunguza makali ya ugonjwa wa ukimwi .
Kuanzia mwaka 2016, Ethiopia imejitahidi kutimiza lengo la kuzuia vifo vya watu zaidi ya nusu milioni kutokana na ugonjwa huo na kupunguza maambukizi mapya kabla ya mwaka 2020, ikiwa ni sehemu ya mpango wa miaka mitano wa maendeleo na mageuzi GTP-II.
Kwa mujibu wa wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2018, idadi ya watu wenye virusi vya Ukimwi wanaopatiwa dawa imeongezeka zaidi kote duniani. Kulingana na ripoti hiyo watu milioni 21.7 wanaogua maradhi hayo duniani kote wanatumia dawa hizo.
Lengo la Umoja wa Mataifa ni kuwawezesha asilimia 90 ya watu wenye virusi vya ukimwi,kujua hali zao hadi mwaka wa 2020. Takriban asilimia 90 miongoni mwao wanapaswa kupatiwa dawa za kudumaza makali ya virusi vya ukimwi, ARV na dawa za kuzuia kabisa kulipuka kwa ugonjwa huo mwilini.
Licha ya kufanyika juhudi kubwa za utafiti katika kipindi cha miaka zaidi ya 30 mpaka sasa haijapatikana dawa ya kutibu maradhi ya UKIMWI. Hata hivyo katika eneo la mashariki na kusini mwa Afrika idadi ya vifo imepungua kwa asilimia 42 kati ya mwaka 2010 na 2017. Asilimia 53 ya watu wenye virusi vya ukimwi duniani wanaishi katika sehemu hiyo ya Afrika.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇