Shirika la Umoja wa Mataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) limesema dalili za wazi na athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi zinazongezeka kote duniani kukishuhudiwa kiwango kikubwa cha hewa chafuzi ya viwandani inayosababisha ongezeko la joto na kufikia viwango vya hatari.
Ripoti hiyo ya WMO ya maadhimisho ya 25 “ya hali ya hewa duniani kwa mwaka 2018 inatanabaisha rekodi ya kupanda kwa kina cha bahari pamoja na ongezeko kubwa la joto baharini na nchi kavu kwa miaka minne mfululizo iliyopita. Mwenendo huu wa ongezeko la joto ukekuwepo tangu mwanzo wa karne hii na unatarajiwa kuendelea.
Mkurugenzi mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema mwaka wa 2019 umeendelea kushuhudia hali mbaya ya hewa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi akitolea mfano kimbunga IDAI cha hivi karibuni ambacho kimesababisha mafuriko na uharibifu mkubwa nchini Msumbiji, Zimbabwe na Malawi. Kwa mujibu wa WMO kimbunga hicho kinaweza kuwa ni moja ya majanga hatari ya asili yaliyokatili maisha ya watu wengi kuwahi kutokea Kusini mwa Afrika.
Mwanzoni mwa mwaka huu pia kumeshuhudiwa majira ya baridi kali iliyovunja rekodi barani Ulaya , baridi isiyo ya kawaida Amerika Kaskazini na joto la kupindukia nchini Australia huku Arctic na Antactic barafu inayeyuka kwa kiwango kisicho cha kawaida.
Takwimu zilizotolewa na ripoti hiyo ndizo zinazozusha hofu kubwa kwani zinasema miaka minne iliyopita ndiyo imevunja rekodi duniani kwa kuwa kiwango cha juu cha joto ambacho kwa 2018 ni takribani nyuzi tojo 1c zaidi ya iliyokuwa kabla ya zama za maendeleo ya viwanda.
Uchafuzi wa mazingira ni sababu kuu ambayo imepelekea kuibuka mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuhatarisha maisha ya jamii ya mwanadamu. Nchi tajiri kiviwanda ndio zinazoongoza katika uchafuzi wa mazingira lakini watu wa nchi za ulimwengu wa tatu hasa barani Afrika ndio wanaokumbana na madhara ya uchafuzi huo. Rais Donald Trump wa Marekani ameiondoa nchi yake katika Mkataba wa Kimataifa wa Paris, ambao ulilenga kupunguza uchafuzi wa mazingira akisisitiza kuwa kilicho muhimu kwake ni viwanda vya Marekani vifanye kazi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇