Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeandika
historia nchini ya kuwa taasisi ya kwanza kukabidhiwa jengo
la ofisi yake na Wakala ya
Majengo Tanzania (TBA) kwenye mji wa Serikali uliopo Mtumba jijini Dodoma, kwa ajili ya kuanza kutoa huduma rasmi kwa wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi
na utawala bora.
Historia hiyo imeandikwa na Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kufuatia jengo hilo kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt Mstaafu George Mkuchika kwa ajili ya kuanza kutoa huduma rasmi kwa wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.
Katika hafla ya kuzindua na kukabidhi jengo hilo Waziri Mkuchika alikata utepe kuashiria uzinduzi wa
huduma zitakazoanza kutolewa na ofisi yake kuanzia Aprili 2,
2019 katika jengo hilo lililopo kwenye
mji wa Serikali jijini Dodoma.
Mkuchika amesema ofisi yake imetekeleza kwa vitendo agizo la ujenzi wa ofisi katika mji wa serikali, na
hatimaye kuandika historia ya kuwa taasisi ya kwanza kukamilisha ujenzi wa
awamu ya kwanza na kuongeza kuwa, anaamini
kwamba, ofisi yake ndio itakuwa ya kwanza kutoa huduma kwenye ofisi za wizara zinazojengwa katika mji huo wa
Serikali.
Mkuchika amesisitiza kuwa, kuanzia tarehe 02 Aprili, 2019 yeye Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Naibu Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora na kurugenzi za Utawala Serikalini, Uendelezaji Sera na
Taarifa za Utumishi na Mishahara kwa pamoja wataanza kutoa huduma katika ofisi
hizo.
‘Kuanzia Aprili 2, mtumishi au mwananchi mwenye uhitaji wa kumuona Waziri,
Naibu Waziri,Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu afike katika ofisi za Utumishi
mtumba ili aweze kuhudumiwa" amefafanua Waziri Mkuchika.
Ameeleza kuwa, baada ya ofisi yake kuhamia, anaamini kwamba,
ndani ya mwezi mmoja ujao wizara nyingi zitakuwa zimehamia rasmi na hatimaye
wananchi na watumishi kutoka katika maeneo mbalimbali nchini watahitaji huduma ya usafiri kuja kwenye mji
wa serikali ili kupata huduma, hivyo
ametoa wito kwa mara nyingine tena kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri jijini
Dodoma kuchangamkia fursa hiyo.
Aidha, katika kuwawezesha watumishi
wa ofisi yake kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa karibu na ofisi iliyojengwa,
Mhe. Mkuchika alitumia fursa hiyo kuwapatia hati za viwanja watumishi ambao
ofisi imewarahisishia mchakato wa kununua viwanja vya serikali vilivyopo mtumba
katika mji wa serikali ili watumishi hao wawe na makazi bora yatakayowawezesha
kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Mkuchika ametoa rai kwa watumishi wote wa umma waliohamia jijini Dodoma, kuhakikisha wanajipatia viwanja
vilivyopimwa na serikali na kujenga nyumba bora ili kuishi kwa staha na kulinda
hadhi ya kuwa watumishi wa umma.
Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa ameishukuru Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kukamilisha ujenzi kwa wakati
na kwa kiwango bora na hatimaye kukabidhi ofisi rasmi ili ziweze kutoa huduma
kwa wananchi.
Dk. Mwanjelwa amewashukuru na kuwapongeza watumishi wote wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora kwa ushirikiano waliouonesha kwa menejimenti tangu mwanzo wa ujenzi mpaka ofisi imekamilika
na kuwataka kuendelea na utamaduni huo wa ushirikiano.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Dk. Laurean Ndumbaro amewashukuru watumishi wote wa ofisi yake kwa
kushiriki kikamilifu katika kufanikisha ujenzi huo na amewapongeza watumishi
hao kwa kutenga muda wao ili kushiriki katika zoezi la upandaji miti kwenye
ofisi hiyo lililofanyika wakati ujenzi ukiendelea.
Awali, akiwasilisha taarifa fupi ya ujenzi wa Ofisi hiyo ya Utumishi, Mkurugenzi wa Ujenzi,
Wakala ya Majengo Tanzania (TBA), Bw. Hamphrey Kilo amesema, ujenzi ulianza rasmi
mnamo Disemba 26, 2018 na kutarajiwa kukamilika Machi 22, 2019,
tarehe ambayo ndio wamekabidhi jengo ambalo kwa mujibu wa mkataba, kazi zote
zilizoanishwa zimekamilika kwa kiwango bora.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika akikata utepe kuzindua rasmi ofisi yake iliyojengwa kwenye mji wa Serikali jijini Dodoma kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi. Naibu Waziri, Dk. Mary Mwanjelwa na Katibu Mkuu-Utumishi, Dkt. Laurean Ndumbaro wameshiriki tukio hilo.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dk. Mary Mwanjelwa wakifurahia uzinduzi wa ofisi yao iliyojengwa kwenye mji wa serikali jijini Dodoma, mara baada ya Mhe. Mkuchika kuzindua ofisi hiyo.
Mwonekano wa jengo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililozinduliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika (Mb) mara baada ya TBA kulikabidhi jengo hilo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika (Mb) akizungumza na watumishi na vyombo vya habari mara baada ya kuzindua rasmi ofisi yake iliyojengwa kwenye mji wa Serikali jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Mkuchika (Mb) akiwa kwenye ofisi yake iliyopo kwenye mji wa Serikali jijini Dodoma mara baada ya kuizindua.
Mkurugenzi wa Ujenzi, Wakala ya Majengo Tanzania (TBA), Hamphrey Kilo akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika mara baada ya kumkadhi waziri huyo jengo hilo lililopo kwenye mji wa serikali jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika (Mb) akimkabidhi hati ya kiwanja mtumishi wake Bi. Zena Makaye, mara baada ya waziri huyo kuzindua rasmi ofisi yake iliyojengwa kwenye mji wa Serikali jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika (Mb) akimkabidhi hati ya kiwanja Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi yake Bw. Peter Mhimba, mara baada ya waziri huyo kuzindua rasmi ofisi yake iliyojengwa kwenye mji wa Serikali jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George H. Mkuchika akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa ofisi yake mbele ya ofisi aliyoizindua ambayo imejengwa kwenye mji wa Serikali jijini Dodoma. Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na Katibu Mkuu-Utumishi, Dkt. Laurean Ndumbaro ni miongoni mwa waliojumuika katika picha hiyo. Imetumwa kwetu na JAMES KATUBUKA MWANAMYOTO,
AFISA HABARI, OFISI YA RAIS-UTUMISHI,
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇